Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jordan: Wageni wenye kamba mguuni Kombe la Dunia 2026

Muktasari:

  • Hii ni hatua ya kihistoria inayoweka Jordan kwenye ramani ya soka la dunia, baada ya miaka mingi ya mapambano.

AMMAN, JORDAN: KWA mara ya kwanza kabisa katika historia yao, timu ya taifa ya Jordan maarufu kama Al Nashama (Mashujaa) itaungana na Uzbekistan nayo kutoka Asia kushiriki Kombe la Dunia 2026 huko Amerika Kaskazini ambapo ni Marekani, Cadana na Mexico watakuwa wenyeji wa fainali hizo.

Hii ni hatua ya kihistoria inayoweka Jordan kwenye ramani ya soka la dunia, baada ya miaka mingi ya mapambano.

Safari ya Jordan kwenda Kombe la Dunia haikuwa kwa kubahatisha, bali ni matokeo ya mabadiliko makubwa waliyoyafanya.


MIAKA YA MWANZO (1953–1996)

Timu ya taifa ya Jordan ilicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwaka 1953 nchini Misri, ambapo ilikabiliwa na kipigo cha mabao 3–1 dhidi ya Syria.

Hii ilikuwa hatua ya mwanzo kabisa ya Jordan kujitambulisha katika ramani ya soka la kimataifa, wakati ambapo timu ilikuwa bado katika kipindi cha kujijenga na kupata uzoefu.

Katika miaka iliyofuata, Jordan iliendelea kushiriki katika mechi za kirafiki na mashindano ya kikanda.

Jaribio lao la kwanza la kufuzu Kombe la Dunia lilikuwa katika mchakato wa kufuzu kwa michuano ya 1986. Hata hivyo, timu ilishindwa kufuzu, ikimaliza kampeni hiyo bila mafanikio.

WAKATI WA KUJIJENGA (1997–2007)

Kipindi cha kati ya  1997 hadi 2007 kilikuwa hatua muhimu ya mabadiliko kwa soka la Jordan ambapo timu ilianza kuonyesha ukuaji katika ushindani wa kikanda na kimataifa.

Chini ya kocha Mohammad Awad, Jordan ilipata mafanikio makubwa kwa kushinda Arab Games mara mbili, 1997 mjini Beirut na 1999 mjini Amman. Mafanikio haya yaliweka msingi wa kujiamini kwa kizazi kipya cha wachezaji wa Jordan.

Baada ya hapo, Jordan ilimuajiri kocha wa Serbia Branko Smiljani, ambaye aliongoza timu kushinda mechi mbili katika hatua ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia 2002. Hata hivyo, timu ilishindwa kusonga mbele hadi hatua inayofuata ya mchujo.

Jordan pia ilifika nusu fainali ya Arab Cup 2002, jambo lililoonyesha maendeleo ya kiwango cha timu katika mashindano ya kikanda.

Mafanikio makubwa zaidi ya kipindi hiki yalikuja chini ya kocha wa Misri Mahmoud El-Gohary ambaye aliisaidia Jordan kufuzu kwa mara ya kwanza katika AFC Asian Cup 2004. Katika mashindano hayo, Jordan ilifanya vizuri na kufika robo fainali, ambako ilitolewa na Japan.

Licha ya kutolewa, kipindi hicho kilishuhudia Jordan ikipanda hadi nafasi yake bora kabisa katika viwango vya FIFA, ikiwa katika nafasi ya 37 duniani. Hata hivyo, timu ilishindwa tena kufuzu Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani.

Katika mashindano ya WAFF Championship ya 2004 na 2007, Jordan ilimaliza katika nafasi ya tatu 2004 na kufika nusu fainali tena 2007. Baada ya mechi tano za kufuzu AFC Asian Cup 2007, El-Gohary alistaafu ukocha na nafasi yake kuchukuliwa na Mreno Nelo Vingada ambaye aliendelea kuiongoza timu lakini Jordan ilishindwa tena kufuzu fainali za mashindano hayo.


NYAKATI MUHIMU

Katika kipindi cha kati ya 2008 hadi 2015, soka la Jordan liliingia katika hatua mpya ya maendeleo na mafanikio, mara nyingi ikitajwa kama ‘ufufukaji wa soka la Jordan.’

Kipindi hiki kilishuhudia timu ya taifa ikipiga hatua muhimu katika mashindano ya kikanda na kimataifa, licha ya changamoto za kufuzu Kombe la Dunia.

Chini ya kocha Mreno Vingada, Jordan ilionyesha uimara mkubwa katika michuano ya West Asian Football Federation (WAFF), ambapo ilimaliza kama washindi wa pili 2008.

Hata hivyo, timu ilishindwa kufuzu Kombe la Dunia la 2010 nchini Afrika Kusini, jambo lililoibua mabadiliko ya kiufundi.

Baada ya hapo, timu ilichukuliwa na kocha Mwisraeli, Adnan Hamad ambaye alikuwa na uzoefu mkubwa katika soka la Asia.

Chini ya uongozi wake, Jordan ilianza kujijenga upya na hatimaye ikafuzu kwa Kombe la Mataifa ya Asia (AFC Asian Cup) la 2011.

Katika mashindano hayo, Jordan ilionyesha uwezo mkubwa kwa kufika hadi robo fainali, kabla ya kutolewa na Uzbekistan kwa kipigo cha 2–1.

Katika mwaka 2011, Jordan pia ilimaliza kama washindi wa pili katika Michezo ya Kiarabu (Arab Games) iliyofanyika Qatar, ishara ya maendeleo yake katika ukanda wa Kiarabu.

Mwaka 2013, Jordan ilijikuta ikikosa nafasi ya moja kwa moja kufuzu Kombe la Dunia, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lake la kufuzu. Hata hivyo, timu ilionyesha mapambano makubwa katika hatua ya mchujo dhidi ya Uzbekistan kwa tiketi ya mchujo wa inter-confederation. Baada ya mechi mbili zenye ushindani, Jordan iliibuka mshindi kwa mikwaju ya penalti 9–8, hatua iliyowapa nafasi ya kusonga mbele, ingawa hatimaye walishindwa na Uruguay kwa jumla ya mabao 5–0, hivyo kukosa tiketi ya Kombe la Dunia la 2014.

Baadaye, kocha Ray Wilkins aliteuliwa 2014 na aliiongoza timu kwenye Kombe la Mataifa ya Asia la 2015. Hata hivyo, Jordan ilitolewa katika hatua ya makundi baada ya kushindwa na Iraq na Japan huku ikipata ushindi dhidi ya Palestina.


JORDAN ILIVYOJIPATA

Juni 2023, kocha Mmorocco Hussein Ammouta aliteuliwa kuinoa timu ya taifa ya Jordan. Chini ya uongozi wake, Jordan ilianza kuonyesha kiwango cha juu na mapema 2024 ilifanya historia kwa kufika fainali ya kwanza kabisa ya Kombe la Mataifa ya Asia (AFC Asian Cup).

Katika safari hiyo ya kihistoria, Jordan ilionyesha ubora mkubwa wa kiufundi na kimbinu. Iliwatoa Iraq kwa mabao 3–2 katika mchezo mgumu ulioshuhudia mabao mawili ya dakika za majeruhi, kabla ya kuibuka na ushindi dhidi ya Tajikistan 1–0 na baadaye kushangaza wengi kwa kuifunga Korea Kusini mabao  2–0 katika hatua ya mtoano.

Hatimaye, Jordan ilifika fainali lakini ikapoteza kwa wenyeji Qatar kwa mabao 3–1, ingawa safari hiyo iliweka historia mpya ya soka la nchi hiyo.

Baada ya mafanikio hayo, Jordan ilipanda katika viwango vya FIFA na kufikia nafasi ya 70 duniani, ikiwa ni nafasi yake bora zaidi tangu  2014. Mwaka 2024, kocha Ammouta aliondoka kwa sababu za kifamilia na nafasi yake kuchukuliwa na Jamal Sellami ambaye alisaini mkataba wa miaka mitatu kuendeleza mradi wa timu hiyo.

Hatua kubwa zaidi ilitokea Juni 5,  2025 ambapo Jordan ilifuzu Kombe la Dunia 2026 kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya kuifunga Oman kwa mabao 3–0 ugenini.

Huu ulikuwa ushindi wa kihistoria ulioweka Jordan katika ramani ya soka la dunia.

Desemba 2025, chini ya kocha Sellami, Jordan iliendelea kufanya vyema na kufika fainali ya kwanza ya Kombe la Arab bila kupoteza mechi yoyote katika hatua za awali. Walipata ushindi dhidi ya UAE 2–1, Kuwait 3–1, Misri 3–0, Iraq 1–0 na Saudi Arabia 1–0, kabla ya kupoteza fainali kwa Morocco kwa mabao 3–2.

Baada ya mafanikio hayo ya kihistoria, Mfalme Abdullah II alimpa kocha Sellami uraia wa Jordan, kama ishara ya kuthamini mchango wake mkubwa katika mafanikio ya timu ya taifa.


MATUMAINI YAO

Musa Al-Taamari ndiye sura ya kizazi kipya cha soka la Jordan na mchezaji anayebeba matumaini makubwa ya taifa hilo kuelekea Kombe la Dunia 2026. Nyota huyo anayekipiga katika klabu ya Stade Rennais FC nchini Ufaransa ameendelea kuthibitisha ubora wake katika moja ya ligi ngumu zaidi barani Ulaya, Ligue 1.

Al-Taamari alianza kuvutia wengi tangu alipokuwa akicheza katika ligi za Mashariki ya Kati kabla ya kuhamia Ulaya ambako aliendelea kukua na kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea Jordan.

Uwezo wake wa kucheza pembeni, kutengeneza nafasi na kufunga mabao umemfanya kuwa silaha muhimu kwa timu ya taifa ya Jordan. Mara nyingi ndiye mchezaji anayebadili mchezo katika dakika muhimu kutokana na kasi yake na uwezo wa kuwapita mabeki mmoja baada ya mwingine.

Katika timu ya taifa ya Jordan, Al-Taamari tayari amecheza mechi 90 za kimataifa na kufunga mabao 24, takwimu zinazomweka miongoni mwa wafungaji bora wa taifa hilo. Alikuwa mmoja wa mastaa walioibeba Jordan hadi fainali ya Kombe la Asia 2023, safari iliyoshangaza bara la Asia na kuifanya Jordan kutazamwa kama nguvu mpya ya soka la Mashariki ya Kati.  Wageni hao katika Kombe la Dunia wapo kundi J pamoja na Austria, Argentina na Algeria.