Job na uhalisia wa soka la rafiki zetu Brazil

Dickson Job kwa sasa ndiyo habari ya mjini. Kisa, hajaitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichosafiri hadi Azerbaijan kwa ajili ya mechi za kirafiki za kalenda ya Fifa kwa michuano rasmi na leo itacheza dhidi ya Bulgaria kabla ya kucheza dhidi ya Mongolia Jumatatu, Machi 25.

Sababu kubwa ya kutoitwa Stars anaitaja Kocha wa timu hiyo, Hemed Moroco, Job alikataa kucheza akitokea benchi kwenye mchezo wa suluhu dhidi ya DR Congo kwenye Fainali za Afcon 2023, Ivory Coast kwenye kundi lao F.

Hata hivyo, beki huyo wa Yanga bado hajazungumza chochote kuhusu hilo na stori hii inatusafirisha hadi Amerika ya Kusini kwa marafiki zetu Brazil hasa linapokuja suala zima la taifa lao, kuanzia kwa wachezaji hadi viongozi.

Tofauti na mataifa mengi ikiwamo Tanzania, Brazil maisha yao kwa kiasi kikubwa ni soka. Kila utakapoenda ndani ya taifa hilo ni soka. Waliofika huko wanakuambia, huwezi ukatembea mita 100 au 200 bila kuona au kusikia soka.

Wapo watakaokuwa wanaongelea soka na wanaocheza. Kwa kifupi, soka ndio utambulisho wao mkubwa. Ni ardhi iliyobarikiwa sana vipaji vya soka vinavyotamba duniani.

Kingine, ni heshima kubwa kuchezea tiumu ya taifa. Kuitwa timu ya taifa ni fahari. Hakuna anayeitwa akakataa utaonekana msaliti.

Ni vigumu kusikia mchezaji wa Brazil amekataa kwenda kucheza michuano ya Copa America kwa sababu anataka kuweka umakini kwenye klabu yake.

Pia kucheza Ulaya sio kwa sababu tu ya pesa, ni kuwa maarufu kwani kwenye ligi yao pia kuna pesa na mfano mzuri ni kwa Neymar aliyeanza kuwa tajiri kabla hata hajaingia Ulaya.

Kuonyesha pesa sio tatizo kwenye ligi hiyo, mwaka 2010 hadi 2011, alinunua boti kwa kutumia zaidi ya Sh10 bilioni, wakati huo akiwa anaichezea Santos ya Brazil.

Ndio maana haikuwa ajabu kwa Willian, Andreas Perreira kuondoka England na kurudi Brazil licha ya umri mdogo waliokuwa nao, wao wanaamini nyumbani kwao ni sehemu salama zaidi, haijalishi wanacheza wapi, lakini jambo la kwanza ni taifa lao na utaifa wao.

Timu ya taifa inapotangazwa mubashara kwenye runinga, utawaona wamekaa sebuleni na familia zao wakifuatilia kusikia majina yao kama yameitwa na wasikiapo huonyesha hisia na hata kulia kwa furaha.

Ni vile tu wanaishi na utamaduni wao, mapenzi yao pia huwa hayaishii kwenye soka, bali hata kwenye tamaduni kama sherehe za asili, kuna wakati Neymar alikuwa akisemwa sana kila ukifika muda wa sherehe za Samba alikuwa akijivunja na kurudi Brazil kwa ajili ya sherehe hizo. Ni utamaduni wa nchi yao.

Turudi kwa Job. Inawezekana kuna mengi yamejificha nyuma yake. Afrika mchezaji kukataa kucheza mechi au kuondoka kambini kwenye timu ya taifa ni kawaida. Matukio ni mengi. Hata kwa viongozi wa mashirikisho wameshazoea. Kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, Brazil, Kevin Prince Boateng na Suleiman Muntari waliondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ghana na katika moja ya mahojiano ya Boateng alisema sababu kubwa ni wajibizana na viongozi wa shirikisho hilo kuhusu masilahi yao.

Haishangazi. Ni mambo yaliyozoeleka Afrika. Ni rahisi sana kwa  wachezaji kukataa mwaliko wa timu ya taifa kushiriki Afcon, kisha akakubali kushiriki Kombe la Dunia. Ni kawaida.

Wabrazil hawawezi kufanya hivi, hakuna rekodi ya mastaa wa Brazil kukataa kwenda kucheza Copa America. Hiyo ni fahari yao. Wako tayari hata kuchoma sindano za maumivu kama wanamajeraha, ili tu wasikose nafasi ya kuichezea timu ya taifa. Ni wazalendo.

Uzalendo wao hauishii kwa wachezaji tu, hata viongozi wao, kwenye maisha yangu sijawahi kusikia wachezaji wa Brazil wakilalamika kuhusu bonasi za timu zao za taifa, labda kwa sababu wana pesa sana, wasijali hata hizo bonasi, lakini ukweli, hata viongozi wao pia wanachukulia umakini wa hali ya juu jambo lolote la taifa lao.

Huku kwetu Afrika, kesi za bonasi utazisikia kila baada ya michuano fulani, kama sio kwa timu moja basi hata mbili. Ndiyo maisha yetu.

Baadhi ya wachezaji wachache wanaoamua kulalamika hadharani, hujikuta kwenye hatari na kufungiwa, hili ni aghalabu kuliona sehemu kama Amerika Kusini, kule kwenye waliochanganyikiwa kwa soka.