JICHO LA MWEWE: Upande mwingine wa Fei na Dube unaochanganya zaidi

KUNA yule mwandishi aliyewahi kutuambia ‘Pesa zako zinanuka’. Ni kweli ukisoma kitabu chake unagundua kwamba zipo pesa ambazo zinanuka. Lakini kuna mwingine aliyewahi kuandika kitabu akatuambia ‘Pesa ni kila kitu’.

Tumuamini nani? Sijui. Ni simulizi ya rafiki zetu wawili kutoka Tanzania na Zimbabwe. Fei Toto na rafiki yake, Prince Dube. Wapo katika siku za mwisho mwisho kukaa katika timu moja. Muda si mrefu wataachana katika mataa.

Fei alianzisha zogo mwaka jana. Akaachana na timu yake kipenzi. Yanga. Yaliyo nyuma ya pazia ni kwamba alikwishaahidiwa kitita kikubwa cha pesa kutoka kwa matajiri ya Azam. Akanunuliwa na gari la kifahari akaenda zake kujichimbia Zanzibar akipisha vurugu zilizoendelea kupitia jina lake.

Kifupi ikawa pesa ndio chanzo cha kila kitu. Kutoka katika klabu yenye mashabiki wengi nchini. Klabu yenye mataji mengi nchini. Klabu ambayo wakati huo na hadi sasa ipo katika moto wake. Klabu ambayo wakati Fei anaiacha ilikuwa katika mwendo wa kuelekea katika fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kila kitu akaacha nyuma yake na kwenda Azam ambako alipewa pesa nyingi. Mwanadamu anataka nini zaidi? Pesa. Mwanasoka anataka nini zaidi? Pesa. Hapo Fei alikuwa anatupa ujumbe kwamba ‘pesa ni kila kitu’. Uamuzi wa kibinadamu unakubali kwamba Fei alikuwa sahihi.

Ni mara ngapi tumeona wanasoka wa zamani wakiishi maisha ya tabu? Mara nyingi. Huwa tunawapiga vijembe kwamba hawakutumia nyakati zao vema. Kwamba unapokuwa na ndugu yako anacheza soka ungependa awe kama Fei.

Subiri kwanza. Inachanganya kidogo. Kuna raia kutoka Zimbabwe amekuja na mawazo tofauti. Prince Dube. Nasikia akili na mawazo yake ameyapeleka katika klabu ya Yanga. Sina uhakika sana, lakini hivi ndivyo ninavyopenyezewa.

Simba na Al Hilal ya Sudan wameweka pesa nyingi mezani kwa Azam wakitaka huduma ya Dube. Hata hivyo, inadaiwa Dube anataka kucheza Yanga. Tunachanganyikiwa hapa. Ana mapenzi na Yanga au? Je Yanga wana pesa kuliko familia ya Said Salim Bakhresa?

Ni wazi kwamba Dube amekuja nchini kutafuta pesa. Sidhani kama kuna yeyote kati ya Simba na Yanga anayeweza kushindana pesa na familia ya Bakhresa. Kwa miaka minne aliyokaa Azam naambiwa kwamba Dube alikuwa Mtoto wa Mfalme haswa.

Naambiwa kwamba achilia mbali kuwa mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi, lakini Azam ilimpangia Dube nyumba mbili kwa ajili ya kumridhisha. Nyumba moja maeneo ya Tabata na nyingine ilikuwa maeneo ya Mbande kule Tabata ili siku za mazoezi aweze kufika mazoezini mapema.

Leo anakataa vyote hivi na kutaka kucheza Yanga. Kisa? Inaweza kuwa kutokana na shamrashamra ambazo zipo Yanga kwa sasa. Timu ya Wananchi. Wachezaji wanafanywa kuwa wafalme. Watoto wa mjini wanadai kwamba timu ina ‘vibe’.

Ukicheza Yanga na Simba unapendwa. Unatukuzwa. Jina lako linaimbwa zaidi mtaani. Kama mabao ambayo Dube amewafunga Simba katika miaka ya karibuni angewafunga akiwa amevaa jezi ya Yanga basi si ajabu jina lake lingeimbwa kama la Fiston Mayele. Hii ndio raha ya kuchezea timu ya mjini.

Watazame Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula na John Bocco. Walikuwa wachezaji bora tangu wakiwa na Azam, lakini wakaimbwa zaidi wakiwa na Simba. Baada ya kufika Simba ndio watu wakagundua kwamba Nyoni alikuwa mchezaji sio wa kawaida. Kwamba alikuwa na akili kubwa uwanjani. Mbona hawakuiona hii akili akiwa na Azam?

Nadhani kuna kundi la wachezaji wa Azam huwa wanazitamani Simba na Yanga kimya kimya. Dube naye ameingia katika mtego huu. Haionekani kama amejali sana pesa linapokuja suala la yeye kutaka kwenda Yanga. Amejali ‘vibe’ zaidi.

Kama tatizo lingekuwa pesa angeweza kuonyesha dalili zote za kutaka kubakia klabuni Azam ili aongezewe pesa. Kwa sasa halitaki jambo hilo na badala yake inaonekana anataka tu kucheza katika klabu ambayo ina mashabiki wengi na ina kelele mjini.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba ametoka katika nchi ambayo kwa sasa raia wake wamepigika kwa shida. Hakuna dola, hakuna mafuta, hakuna unga, hakuna chochote. Zimbabwe. Juu ya kila shida lakini sasa hivi anaamua kuchagua ‘vibe’ kuliko pesa.

Na hapo hapo tunajikumbusha kwamba Fei aliamua kuchagua pesa kuliko ‘vibe’. Lakini vile vile ukipima uwezekano wa kupata mataji unagundua kwamba Yanga ina uwezekano mkubwa wa kupata mataji na kushiriki michuano ya kimataifa kuliko Azam. Hata hivyo, mawazo ya Fei yalikuwa tofauti na tunavyofikiria.

Hii inatukumbusha jinsi mwanadamu alivyo. Na tuna mifano mingi ambayo hata Ulaya wachezaji wanaamua kama hivi. Muda si mrefu Kylian Mbappe atakwenda zake Real Madrid ya Hispania. Inatajwa kwamba akienda Real Madrid basi mshahara wake utapungua.

Hata hivyo, Mbappe ameamua kufuata mataji na klabu yenye ‘vibe’ zaidi kuliko PSG. Madrid haiwezi kushindana na pesa na PSG kwa sasa, lakini Mbappe amekuwa na mawazo tofauti. Anataka timu ambayo itampa uhakika wa kushinda mataji.

Sijui ni lini tutawaelewa wanasoka. Ni kama inavyotuchanganya kumuelewa mwanadamu wa kawaida. Wakati mwingine anataka pesa, wakati mwingine anataka shamrashamra zaidi ya pesa. Hiki ndicho kinachoonekana kwa Fei na Dube. Kifupi Fei alikuwa anataka kwenda aliko Dube, lakini na Dube naye alikuwa anataka kwenda aliko Fei. Ni nadra sana kwa mapenzi na pesa kukaa sehemu moja.