JICHO LA MWEWE: Simba bila Chama, Yanga bila Aziz Ki

YANGA walikuwa wanashangilia nini wakati Clatous Chotta Chama na Stephane Aziz Ki walipofungiwa kwa kosa moja? Ilinishangaza kidogo. Yanga walionekana kutokerwa na adhabu zilizotolewa. Simba waliinamisha vichwa chini.

Yakanijia maswali. Ina maana Chama ni bora kuliko Aziz Ki? Ukweli ni huo. Mpaka sasa Chama ni bora kuliko Aziz Ki. Amezoea ligi yetu. Ameiweka mfukoni. Aziz Ki bado hajaizoea ligi yetu. Bado hajatuliza kichwa. Kuna wakati anataka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Anataka kuthibitisha ubora wake.

Aziz Ki anabebwa na matukio yake bora uwanjani hasa katika mechi kubwa. Pambano la Ngao ya Jamii ile pasi yake kwa bao la kwanza la Fiston Mayele ilikuwa bora sana. Baadaye akampiga tobo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ halafu akapiga pasi kwa Mayele lakini ni Mayele akashindwa kuitendea haki pasi.

Ikaja tena mechi dhidi ya Simba ya Ligi Kuu. Lile bao lake la kusawazisha la mpira wa faulo litakumbukwa milele. Ni kama tunavyolikumbuka la Bernard Morrison dhidi ya Simba.

Kuna aina ya mabao huwa yanakumbukwa milele kutokana na umuhimu wake, achilia mbali ubora wake.

Halafu akaja kufunga bao ambalo Yanga hawatakuja kulisahau zaidi. Dhidi ya Club Africain ugenini. Bao ambalo limewafanya Yanga wasubiri ratiba ya Makundi ya Shirikisho Afrika. Nje ya hapo Aziz Ki hajafanya maajabu makubwa kama yale aliyokuwa anafanya akiwa na ASEC Mimosas. Sishangai. Kuna wachezaji huwa wanaingia wakiwa wa baridi halafu baadaye wanaondoka wakiwa wa moto na wanaacha historia kubwa nyuma yake. Mpaka leo natazamia Aziz Ki afanye makubwa siku za usoni pindi atakapotulia na kuuelewa mpira wetu.

Lakini kama unamlinganisha na Chama basi utagundua Chama yupo mbali na ameshafanya makubwa. Ndani yake ana mabao ya kumbukumbu ambayo ni mengi lakini ana viwango vingi vya ubora ambavyo ameviacha. Licha ya kila kitu inaonekana pia Simba haiendi bila ya yeye. Anasimama kuwa kila kitu kuliko Aziz Ki alivyo na Yanga.

Lakini kama tukiweka suala hili la ukweli Chama yupo mbali kwa Aziz Ki kuna jambo jingine ambalo linasimama nyuma yake. Yanga ina timu pana ambayo inawapa jeuri nje ya Chama kuliko ambavyo Simba ilivyo na timu nje ya Chama. Jambo hili limedhihirika katika mechi tatu ambazo Chama na Aziz Ki walikuwa nje.

Yanga haina shida. Nafasi ya Aziz Ki atacheza Fei Toto pale mbele na hakuna kitakachoharibika. Hata wakati huu ambao Aziz Ki amekuwa akihusika katika matukio muhimu bado Fei amekuwa staa mkubwa Yanga. Kuna mambo mengi ambayo Fei anayafanya huku Aziz akiwa ndani ya uwanja.

Lakini hapohapo hata kama Fei Toto asipokuwepo uwanjani pale mbele anaweza kucheza fundi Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ na maisha yakaendelea. Hapa ndio maana Yanga haikuona tatizo sana wakati Chama na Aziz Ki walipofungiwa. Tatizo liliangukia kwa Simba ambayo haina mbadala kama Chama akiwa nje.

Na hata kama ina wabadala lakini hawasogelei kwa karibu uwezo wa Chama. Hata Aziz akija kuwa tishio katika ligi yetu bado kutakuwa na pengo dogo kati yake na Fei Toto lakini kwa Simba pengo siku zote limekuwa kubwa kati ya Chama na mchezaji yeyote ambaye atakuwa mbadala wake.

Mfano ni namna ambavyo Fei amekuwa aking’ara katika mechi tatu ambazo Aziz amekuwa nje. Tazama dhidi ya Singida United, halafu tazama jinsi ambavyo Simba ilikwenda kwa Larry Bwalya wakati Chama alipoenda Morocco. Pengo lilikuwa kubwa na halikupaswa kuwa hivyo.

Na kwa ujumla pengo linaendelea kuwepo hata wakati huu amerudi halafu anakosekana uwanjani. Utulivu unakuwa safarini. Ubunifu unakosekana katika eneo la mwisho. Yeye ndiye roho ya mashambulizi ya Simba katika eneo la mwisho. Anaweza kupiga pasi muhimu kwenda kwa mtu mwingine ambaye atapiga pasi ya bao, au yeye atapiga pasi ya bao, au atafunga.

Anapokosekana uwanjani basi Simba inakosa mambo haya matatu kwa wakati mmoja. Haishangazi kuona ushindi wao finyu katika mechi dhidi ya Ihefu na Namungo unahusisha kukosekana kwake. Ni tofauti na Yanga ambayo hakuna mahali imelikumbuka jina la Aziz Ki katika mechi tatu zilizopita.

Na sasa kuna mambo mawili lazima yafanyike kwa Simba halafu Aziz Ki. Simba lazima iimarishe kikosi chake na kuongeza ubora ambao kwa kiasi kikubwa utapunguza umuhimu wa Chama uwanjani. Lazima waletwe watu ambao wataibeba timu wakati Chama akiwepo uwanjani au asipokuwepo. Wakati mwingine inaweza kuwa katika nafasi tofauti au ileile. Kwa mfano, kuna wakati kulikuwa na mjadala nani roho ya Simba kati ya Jose Louis Miquissone na Chama. Ni kwa sababu Miquissone alikuwa anaibeba timu katika uzito uleule ambao Chama anaibeba. Tangu aondoke Miquissone alikuja Ousmane Sakho ambaye ameonekana kuwa mchoyo na asiye na malengo na timu. Amekuja Augustine Okrah ambaye alianza vizuri lakini kila siku kasi yake inapungua na yeye ameanza kuwa mbinafsi kama wenzake

Amekuja Nelson Okwa ambaye hajulikani anachokifanya uwanjani na kama hana maisha marefu Simba. Amekuja Kibu Dennis mpaka sasa yupo katika matatizo na mashabiki ambao hawamuelewi. Chama anabakia kuwa alama ya Simba kama ilivyokuwa kabla ya hawa hawajafika.

Lakini kwa upande wa Aziz Ki nadhani pia ni wakati wa yeye kutafakari kwanini Yanga hawakukasirika sana yeye na Chama walipofungiwa mechi tatu. Nadhani tukio hili alifanye kama motisha. Mchezaji yeyote mzuri na mwenye kipaji kama yeye lazima atataka kusimama juu ya timu na kuwa alama ya timu hata kama kuna wachezaji wengine muhimu.

Baada ya hili tukio agundue tu bado hajaishika timu kisawasawa kama ambavyo Chama ameishika Simba. Nafasi hiyo anayo kwa sababu akimaliza mazonge yote yaliyomzunguka kwa sasa halafu akarudi kuwa Aziz Ki yule wa ASEC Mimosas ambaye alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast hapana shaka hakuna mchezaji wa kugusa ubora wake.

Bahati nzuri Yanga inamsubiri na inaamini haijapigwa kwa sababu amekuwa akiwapa matukio mazuri uwanjani lakini pia wanajua yeye ni mchezaji wa aina gani pindi anapokuwa katika ubora wake. Vinginevyo kungekuwa na mjadala mkubwa kuhusu kiwango chake.