JICHO LA MWEWE: Ndio maana kina Okocha walitimka Nigeria!

HII ni mara ya kwanza kufika Nigeria. Nimekuja na Yanga. Nimekuja pia kuchunguza kwanini wachezaji wengi wa Nigeria wapo nje ya nchi. Sio tu wachezaji bali hata raia wao wa kawaida. Kuna Wanigeria zaidi ya milioni moja wanaishi Afrika Kusini.

Yanga walikuwa wanacheza pambano lao Port Harcourt. Unatajwa kuwa mji wa tano kwa ukubwa nchini hapa. Haukawaii kufahamu ni kwanini Wanigeria wengi wanacheza nje ya nchi yao. Tumeanza kuwasikia wengi na hatutaacha kuwasikia.

Katika zama za zamani tuliwasikia kina Uche Okwechukwu, Rashid Yekini, Finidi George, Austin Jay Jay Okocha, Nwankwo Kanu na wengineo wengi. Zama hizi tuna kina Wilfried Ndidi, Kelechi Iheanacho na wengineo wengi ambao wametapakaa kila kona ya ulimwengu.

Wanigeria wameshindwa kugawana vyema kile kitu kinachoitwa keki ya taifa. Inaonekana ni taifa la watu wajanja ambao kila mmoja anachukua chake mapema na kuwaacha raia wake wakiwa maskini ingawa inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi imara Afrika.

Hauwezi kuliona hilo kwa macho. Kwanza kabisa watu ni wengi. Kando ya barabara za Port Harcourt watu ni wengi na maisha ni vurugu. Hii inatokana na ukweli kwamba Nigeria ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya watu Afrika kama sio duniani kwa ujumla. Sensa inaonyesha kuna Wanigeria 112 milioni wanaoishi nchini kwao. Vitongoji vya Port Harcourt vinaakisi idadi kubwa ya watu Nigeria. Kila kitu kimechakaa. Watu wamechakaa. Magari yamechakaa. Majengo yamechakaa na barabara pia zimechakaa.

Jiji la Port Harcourt linatajwa kuwa lenye utajiri mkubwa zaidi miongoni mwa majiji ya Nigeria. Hapa kuna utajiri wa mafuta lakini pia kuna bandari. Kinachoshangaza ni kwamba utajiri huo unabakia katika makaratasi au serikalini. Raia wake wamechoka, mitaa yake imechoka, barabara zake zimechoka. Naelezwa kwamba Abuja ndio mji ambao walau una majengo ya kisasa na barabara za kuvutia. Vinginevyo Nigeria imechakaa na ni wazi kwamba hesabu za wachumi Nigeria ni nchi tajiri haziakisi macho pindi utakapotembea vitongoji.

Raia wengi ni maskini na watu wachache ni matajiri. Kutoka katika hoteli ambayo Yanga walikuwa wamefikia ya Swiss Sprit kando yake kwa nyuma tu kuna nyumba zilizochakaa ambazo mabati yamewekewa mawe juu ili yasizolewe na upepo. Watoto wanacheza mpira mbele ya macho ya wazazi wao ambao wanapika chakula nje ya nyumba. Naambiwa hapo ndipo yanapoanzia maisha ya mchezaji wa Kinigeria. Kuondoka Nigeria na kwenda kucheza nje ya nchi kuna maana kubwa kwa mchezaji.

Kwanza mchezaji anaondokana na vurugu za jiji lake au mtaani kwake. Mchezaji yeyote wa Nigeria ambaye ataondoka Nigeria na kwenda kwingineko ghafla atajikuta katika jiji zuri, lisilo na vurugu kama ilivyo mitaa ya kwao. Pua yake itapumua vyema na masikio yataondolewa katika kelele zisizo na msingi.

Mtu yeyote ambaye ataondoka Nigeria atajikuta katika nafasi ya kuongeza kipato. Nigeria hii ina watu lukuki lakini ambao hawana ajira. Wengi kati yao wana elimu kubwa ambayo inawapa uhakika wa ajira mahala kwingine au uhakika wa maarifa ya kuishi.

Kwa wale ambao wamezaliwa na vipaji, soka inabakia kuwa njia kubwa ya kutengeneza maisha. Inawezekana katika umri mdogo wakapelekeshwa na mambo mawili. Kwanza ni kuona maisha ya kifahari ya mastaa wengi wanaocheza nje. Lakini pia msukumo kutoka kwa wazazi. Ni tofauti na nchi yetu ambapo baadhi ya wazazi hawaamini kama vipaji vya michezo na sanaa vinaondoa umaskini. Lakini pia mazingira haya magumu ninayoyaona Nigeria haishangazi kuona linamfanya Mnigeria aweze kuishi Shinyanga akicheza Biashara Shinyanga bila ya shida. Kwanza mji wenyewe Shinyanga kwake unakuwa mzuri tu kuishi tofauti na kelele za Port Harcourt.

Lakini, hapohapo Mnigeria hataki kutazama nyuma. Kwa nilichokiona hapa ni ngumu kwa Mnigeria kutazama nyuma kimaisha. Sawa nyumbani ni nyumbani, lakini nyumbani kunakuwa kutamu zaidi kama unaweza kurudi ukaishi kwa utulivu. Kwa nilivyoitazama Nigeria, nyumbani kunaweza kuwa kutamu kwa watu kama kina Jay Jay Okocha. Hawa wana majumba ya kifahari hapa na wana magari ya kifahari. Wanaishi kifahari. Nigeria hapawezi kuwa kutamu kwa raia wa kawaida ambaye hajafanikiwa nje ya nchi. Na haishangazi kuona hawarudi nyuma. Maisha ya Nigeria yana ushindani mwingi. Hakuna kazi ya mwanaume wala mwanamke. Nadhani idadi yao kubwa inasababisha watafute mkate katika ardhi nyingine nje ya nyumbani. Ni kama ilivyo kwa Wachina, Wahindi au Wabrazil. Mkate wa ardhi yao pekee hautoshi.