JICHO LA MWEWE: Kizunguzungu cha tuzo kinavyoacha maswali mtaani

SHABIKI mmoja alinivamia na kuniuliza maswali muhimu kuhusu tuzo zilizofanyika mapema wiki iliyopita. Maswali yake yalikuwa na changamoto lakini nikaona bora niyajibu hapa kwa faida ya wengi. Mpira wa Bongo una siasa nyingi ndani yake.

Vipi kuhusu Aishi Manula kuwa kipa bora? Ndiyo mwaka wa nne huu Aishi anakuwa kipa bora katika ligi yetu. Kipa bora ni yupi? Tuanzie hapa. Wapo wanaodai kipa bora ni yule ambaye hajaruhusu mabao mengi. Ni utata mkubwa katika hili. Vipi kama anacheza katika timu ambayo haishambuliwi sana?

Wengine wanaamini kipa bora ni yule ambaye ameokoa michomo mingi. Bahati mbaya makipa wa namna hii wanapatikana katika timu dhaifu. Huko ndipo unakuta kipa analazimika kuokoa michomo mingi. Hata hivyo, kuanzia huko duniani kwingine hadi huku utaratibu wa kipa bora umeendelea kuwa ule ule ambao umetumika kumchagua Aishi. Bado dunia inaangalia zaidi kipa ambaye amefungwa mabao machache na ambaye pia hajaruhusu nyavu zake kuguswa katika mechi nyingi (clean sheet). Huwa haijalishi sana kama anacheza katika timu bora na haishambuliwi mara kwa mara kama ilivyo kwa Aishi na Simba yake. Mimi ni nani nipingane na dunia? Acha Aishi apewe tuzo yake kwa utaratibu ule ule tuliozoea.

Beki bora? Amepewa Mohamed Hussein Tshabalala wa Simba. Kwa waliokuwepo ambao alikuwa anagombea nao haya yalikuwa maamuzi sahihi. Tshabalala alikuwa na msimu mzuri kuliko Shomari Kapombe. Kuliko pia Dickson Job wa Yanga licha ya kwamba wanacheza nafasi tofauti uwanjani.

Swali la msingi hapa ni kukosekana kwa Josh Onyango anayeweza kuwa beki bora wa kati katika ligi yetu kwa sasa. Hatujui kwa nini Josh hakuingia katika kundi la wanaogombea au labda uzalendo ulitumika zaidi katika tuzo hizi? Inawezekana.

Katika eneo la kiungo hatukuwa na Luis Miquissone. Hatujui kwa nini. Labda tulijaribu kuweka uwiano sawa kati ya wachezaji wa Simba na Yanga katika kila eneo lakini Mmakonde kama kawaida yake alikuwa katika ubora wake msimu ulioisha. Sijui kwa nini hakuwekwa walau agombee halafu ashindwe.

Vinginevyo aliingizwa Fei Toto ambaye alimaliza Ligi vema baada ya kuwasili kwa kocha Mohamed Nabi ambaye alimsogeza mbele katika eneo la kiungo akajikuta akifunga zaidi na kutoa pasi za mwisho. Hata hivyo namba zake bado ni za chini kulinganisha na zile za Miquissone.

Fei huyu huyu alichaguliwa mwanasoka bora wa michuano ya Azam Federation. Bado katika michuano hiyo namba zake haziwezi kufanana na Miquissone. Nadhani uliletwa Usimba na Uyanga kwa ajili ya kubalansi mambo na kuwaridhisha Yanga katika tuzo. Vinginevyo katika nafasi zote mbili Mmakonde alistahili kupewa tuzo. Au kwa sababu hayupo nchini?

Vipi kuhusu John Bocco kuwa mchezaji bora? Sina neno. Angeweza pia kuwa Clatous Chama na nisingekuwa na neno. Wote wawili walikuwa na msimu mzuri. Bocco ameng’arishwa zaidi na mabao yake na ni kitu kinachompambanua zaidi kuliko washambuliaji wengine wa ndani.

Kuelekea kuwania hizi tuzo hatukuona majina ya Idd Nado na Prince Dube wakigombea kitu chochote. Ni kichekesho kiaina lakini mara zote Azam wamekuwa wakionewa katika mambo mengi kwa sababu sio timu ya wananchi. Huwa wanaonewa pia kwa sababu sio walalamishi. Kama Nado na Dube wangekuwa wanacheza timu zetu za kelele tungesikia kelele nyingi lakini si unaona jinsi kwa sasa hali ilivyo kimya?

Bao bora? Hapa kuna maoni tofauti kuhusu bao bora. Hata wazungu wamekuwa wakibishana kuhusu bao bora ni lipi. Kuna bao lililofungwa kwa umbali mrefu kama lile la Bernard Morrison dhidi ya Namungo. Wapo wanaoamini mabao kama haya ni bora. Lakini kuna wanaoamini bao bora ni lile linalotokana na juhudi binafsi za mchezaji kama vile kupiga chenga watu wengi kabla ya kufunga. Ni kama Ryan Giggs alivyofanya dhidi ya Arsenal au Diego Maradona alivyofanya dhidi ya England mwaka 1986.

Lakini wapo pia wanaoamini bao bora ni lile linalotokana na wachezaji kupigiana pasi nyingi kabla ya mmoja wao kumalizia. Wakati mwingine zinaweza kupigwa pasi 40 kabla ya mfungaji kumalizia. Yote haya yanawezekana. Bao la Morrison lilikuwa bora lakini hata la aliyechaguliwa lilikuwa bora pia baada ya juhudi binafsi.

Mhamasishaji bora? Tuwe wakweli hakuna kitu kama hiki kwa wenzetu. Tunaweza kusema tumeifanya kivyetu lakini mwishowe tuzo zinapaswa kuishia kwa wachezaji, benchi la ufundi na waamuzi. Hawa kina Bongozozo, Haji Manara na Masau Bwire wote wangeweza kupewa tuzo za kuwatambua kwa kazi wanazofanya. Hatukuhitaji kujua nani ni zaidi ya mwingine kiasi cha kupigiwa kura. Mwishowe waandaji wa tuzo kama hizi wasiwe na hofu na masuala ya Usimba na Uyanga. Mpira unachezwa hadharani. Kama ningekuwa na mamlaka ya kuchagua wachezaji bora nisingesita kuchagua wachezaji wote wa Simba. Kipa ningemweka Aishi, beki ningemchagua Onyango, kiungo ningemchagua Chama au Miquissone na mshambuliaji angekuwa Bocco. Hii ingeweka mazingira mazuri katika tuzo zinazofuata. Hofu ya Yanga wangechukia, huwa inaharibu tuzo.

Soka ni mchezo wa hadharani na sitashangaa kuona wachezaji wengi wa Yanga wanaingia katika kinyang’anyiro cha tuzo msimu ujao kwa sababu kwa sasa Yanga wana watu bora. Kina Khalid Aucho, Fiston Mayele, Yannick Bangala na wengineo wakiendelea hivi sidhani kama hawatakuwepo kihalali kabisa katika tuzo za msimu ujao.

Wakati mwingine masuala ya kubalansi huwa tunayapeleka hata katika uteuzi wa kikosi cha timu ya taifa kitu ambacho sio sahihi. Mpira unachezwa hadharani na wachezaji bora huwa hawajifichi. Kama kila kitu kinaweza kutoka Simba pekee acha iwe hivyo. Kama kila kitu kinatoka Yanga pekee acha iwe hivyo.

Kitu kingine ambacho huwa kinanishangaza ni namna ambavyo kuna wachezaji wa zamani wamekuwa wakitambuliwa katika kila tuzo. Mfano ni Mzee Abdalah Kibadeni au Sunday Manara. Imekuwa kama vile fasheni kwamba kila tuzo lazima watambuliwe. Haipaswi kurudiwa mara kwa mara. Zamani hakukuwa na wachezaji wengine?

Sio mbaya pia kupeleka tuzo za heshima kwa wachezaji ambao walishafariki. Vipi kuhusu akina Athuman Mambosasa? Si wana ndugu zao bado wanaishi? Vipi kuhusu akina Hussein Tindwa ambao walifia uwanjani? Hatuoni umuhimu wa kuwakumbuka?