JICHO LA MWEWE: Haaland anafikirisha kuhusu soka letu la Afrika
ERLING Haaland, staa wa Manchester City na Timu ya Taifa ya Norway huwa ananifikirisha kuhusu soka letu. Julai 21 mwaka huu ndio kwanza ametimiza miaka 22. Inanifikirisha kidogo. Kwa sasa tayari ni mshambuliaji mwenye kiwango cha juu duniani. Wazungu wanasema World Class striker.
Amefikije katika kiwango hiki akiwa na umri wa miaka 22 tu. Hawa ni kundi la watoto waliozaliwa mwaka 2000. Ni hivi karibuni tu. Amezaliwa baada ya Zinedine Zidane na wenzake kutwaa Kombe la Dunia pale Ufaransa. Amezaliwa miaka mitatu baada ya Mwalimu Nyerere kufariki. Kifupi ni mtoto wa juzi tu. Amenifikirisha kuhusu soka letu. Hata wachezaji wetu wanapoamua kudanganya umri bado umri wa miaka 22 hauwakuti Simba na Yanga achilia mbali Ulaya. Haaland ni alama ya namna ambavyo wenzetu huwa wanajua kuwatengeneza wachezaji na kufikia uwezo wao (potential) katika umri mdogo.
Kitu cha kwanza ambacho kipo wazi kabisa ni suala la lishe. Umbo kama lile la Haaland linakushawishi kocha kumuingiza katika kikosi cha kwanza hata akiwa na miaka 15 tu. Tayari anakuwa ana nguvu na stamina ya kucheza soka katika kiwango cha juu.
Wachezaji wetu wanazaliwa katika familia maskini ambazo hazitoi lishe sahihi kwa watoto. Tatizo hilo sio la Tanzania tu. Lipo katika nchi nyingi za Waafrika, hasa Waafrika weusi. Matokeo yake tunalazimika kudanganya miaka kwa ajili ya kujaribu kuwahi kuwafikia Wazungu. Nchi za Kiarabu walau wachezaji wake wanapata lishe nzuri.Watoto wa Kitanzania ambao wangeweza kutoa ushindani wa utimamu wa mwili ni watoto wa uzunguni. Watoto wa Masaki, Oysterbay, Mikocheni na maeneo mengine ambayo wanaishi matajiri. Hawa ndio watoto wanaozaliwa na kukulia katika afya njema.
Bahati mbaya ni kwamba soka na michezo mingi duniani huwa haichezwi na watoto wa matajiri. Wanaomiliki hii michezo hii ni matajiri, lakini wanaocheza ni watoto wa maskini ambao wanatafuta maisha. Ni watoto hawa hawa wa maskini ndio ambao lishe zao tunazijua.
Kuna mambo mawili. Kuna kumfanya mchezaji wa miaka 22 acheze mpira, pia acheze katika kiwango cha juu kama Haaland. Hapa sisi tunakabiliwa na mambo yote mawili. Makinda wetu hawana lishe, lakini hawapewi misingi imara ya kuucheza mchezo wenyewe.
Mitaani wanajitolea walimu wasio na uwezo wala misingi ya kiufundishaji achilia mbali ubovu wa viwanja. Wakati hayo yanatokea Wazungu wanakuza wachezaji wao katika misingi sahihi na lishe sahihi. Kama una kipaji kikubwa moja kwa moja unakwenda kuwa mchezaji mkubwa bila ya kujali suala la umri wako.
Wayne Rooney akiwa na umri wa miaka 17 alishakuwa mchezaji tegemeo Timu ya Taifa ya England na klabu yake ya Everton. Lakini tusisahau kwamba Pele alitwaa Kombe la Dunia na Brazil pale Stockholm akiwa na umri wa miaka 17. Ni kama ambavyo leo Haaland ameiteka dunia akiwa na miaka 22 tu. Lakini alianza kuiteka dunia tangu akiwa na umri wa miaka 17 pale Salzubrg.
Mara chache naweza kuandika kitu bila ya kutoa suluhisho. Hii ni miongoni mwa makala ambazo naweza kukosa suluhisho. Suala la lishe linatokana na umaskini wa nchi zetu pamoja na klabu zetu kwa ujumla. Sijui tunaweza kufanya nini ili kubadilisha jambo hili. Kumbuka kuna timu za hadhi ya Ligi Kuu huwa zinakula kwa kubahatisha. Vipi kwa timu zao za vijana?
Lakini hapohapo kumbuka lishe ya mwanamichezo inatengenezwa katika muda gani? Wenzetu wanawatengeneza wakiwa watoto. Mazoezi yao yanaendana na lishe. Kama timu kubwa nchini hazina programu hizi vipi kwa timu ndogo na za kawaida?
Matokeo ya kuwakosa kina Haaland katika nchi zetu za Kiafrika huwa hauwezi kuyaona kwa haraka. Kwa mfano, mpaka sasa Afrika haijawahi kufika katika hatua ya nusu fainali Kombe la Dunia, achilia mbali kufika fainali au kutwaa kombe lenyewe.
Katika michuano hii tunajikuta tumechanganya wachezaji wengi wenye umri mkubwa ambao walidanganya umri, lakini mbinu zao za soka ni tofauti na Wazungu. Ubora wetu huwa unakuja pale ambapo tunachanganyika na Wazungu katika timu zao. Tukiwa wenyewe kuna mahala unaona wazi tunakwama kwa urahisi.
Wakati mwingine mbaya zaidi huwa tunajidanganya katika michuano ya vijana. Waafrika huwa tunatamba katika michuano ya Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 17 au chini ya umri wa miaka 20. Ni rahisi kwa Ghana, Nigeria au Cameroon kuchukua Kombe la Dunia la vijana. Kumbe wakati Wazungu wakiwa na programu zao za ukweli za vijana, sisi huwa tunachezesha vijeba dhidi ya watoto wao.
Tunajidanganya tumeshinda kumbe baada ya miaka kadhaa ijayo wakati makinda wao wakianza kutumikia umri wa kweli, sisi vijeba vyetu vinaanza kuchoka huku pasipoti zao zikionyesha umri wa miaka 28. Ni tatizo la kukosa maisha ya kina Haaland ndani ya soka letu.
Haaland anatufikirisha. Yeye ni mfano tu wa Wazungu wengi ambao wanaandaliwa katika umri mdogo kufanya mambo makubwa. Achana naye, majuzi nilikuwa katika Jiji la Madrid na nilipata bahati ya kutazama mechi za mchezo wa Tennis. Nilitazama pambano kati ya Carlos Alcaraz na Novak Djokovic.
Huyu Alcaraz anakuja juu na tayari ameshaanza kushinda mataji makubwa ya tenisi ulimwenguni. Ana umri wa miaka 19 tu. Wakati nikiangalia pambano lile na jinsi mchezo wenyewe unavyotumia nguvu nilikuwa najiuliza imewachukua Wazungu mambo gani kumuandaa kijana wa miaka 19 kucheza tenisi ya ushindani kiasi kile. Ni suala lilelile tu ka Haaland.
Ukweli dunia wanayoishi kina Haaland na dunia yetu ni vitu viwili tofauti. Najaribu tu kuwaza ni namna gani tunaweza kuziba pengo lenyewe lakini nagundua kwamba ni suala la kihistoria zaidi.
Ni suala la muundo wa kidunia na uchumi wake. Sidhani kama itakuwa rahisi wa kijana halisi wa Kitanzania au Kiafrika kutamba Ulaya kama Haaland katika umri wa miaka 22 tu.