Prime
JICHO LA MWEWE: Fundi Yusuf Kagoma ni wale masela wanaoishi ghetto

Muktasari:
- Kilikuwa kile kikosi cha awali kabla ya kikosi hiki cha Singida Big Stars. Kile ambacho kilisambaratika lakini baadaye kikarudi tena. Kagoma alikuwa anatawala dimba la kikosi kile na kumuacha Bruno akifanya uamuzi mwingine sahihi zaidi uwanjani. Kagoma alikuwa anagomea watu kweli kweli pale katikati ya dimba.
YUSUF Kagoma anawashangaza wengi? Ndio, lakini sio mimi. Nilimuona kule Singida United wakati ule rafiki yangu Mwigulu Nchemba alipoamua kukusanya kikosi chenye mastaa wengi wa kigeni, hadi Wabrazil kina Bruno Gomes. Kagoma alicheza timu ile katika kikosi cha kwanza. Na aling’ara.
Kilikuwa kile kikosi cha awali kabla ya kikosi hiki cha Singida Big Stars. Kile ambacho kilisambaratika lakini baadaye kikarudi tena. Kagoma alikuwa anatawala dimba la kikosi kile na kumuacha Bruno akifanya uamuzi mwingine sahihi zaidi uwanjani. Kagoma alikuwa anagomea watu kweli kweli pale katikati ya dimba.
Unapokusanya kikosi kama kile chenye mastaa wa kigeni, halafu mastaa walioachana na Simba na Yanga kina Deus Kaseke, ni ngumu kufikiria kama mtoto wa mtaani asiye na jina kama Kagoma akawa mchezaji panga pangua katika kikosi cha kwanza. Kagoma alikuwa panga na pangua na Bruno pale katikati.
Na sasa ametua Simba watu wanashangaa. Wanashangaa kipaji chake. Kiungo aliyesajiliwa kwa mbwembwe kama Augustine Okajepha aliyekuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Nigeria msimu uliopita anakaa katika benchi, lakini mtoto wa mtaani Tanzania, Kagoma anazima katikati ya uwanja akiwa katika jezi nyekundu na nyeupe za Simba.
Imenikumbusha mambo mengi. Mambo kama manne hivi. Kwanza ni namna ambavyo hatuwajui sana wachezaji wetu. Mara nyingi mashabiki wana ushabiki zaidi na wachezaji wa timu zao Simba na Yanga. Hawatazami wachezaji wa timu pinzani pindi wanapocheza na timu nyingine. Kama ingekuwa wanajua hilo wangemjua Kagoma siku nyingi tu.

Imenikumbusha unafiki wetu wa namna ambavyo tuliwaona Aishi Manula, Erasto Nyoni, John Bocco kama wachezaji hodari zaidi wakati walipojiunga na Simba wakitokea Azam wakati siku zote tangu wakiwa Azam walikuwa wachezaji hatari kama walivyo. Ndivyo tulivyo. Mchezaji anakuwa mzuri zaidi akifika Simba au Yanga.
Naamini mashabiki wengi wa Simba na Yanga awali walikuwa wanashangaa kwanini timu zao zilikuwa zimeingia katika vita ya Kagoma. Wangeingia katika vita ya Okejepha nadhani mitandaoni kungekuwa hakukaliki, lakini kwa sababu walikuwa katika vita ya Kagoma, mtoto wa Kitanzania wasiyemfahamu, basi walikuwa wanamchukulia poa tu.
Achilia mbali kumtazama akiwa na Singida United niliwahi pia kumtazama Kagoma kwa karibu wakati niliposafiri naye kwenda Indonesia mwaka jana katika pambano la kirafiki kati ya Taifa Stars na timu ya taifa ya Indonesia. Kagoma alinionyesha mpira mkubwa ambao niliamini yeyote ambaye angempata Kagoma kati ya Simba na Yanga angelamba dume.

Jambo la pili ambalo limenifikirisha mbali kwa Kagoma ni hili hapa. Zamani kuna makocha wengi wa timu za kigeni walikuwa wakifika nchini kucheza na Simba, Yanga au timu ya taifa wanakwambia mchezaji fulani, mwenye namba fulani anaweza kucheza soka la kulipwa Ulaya. Labda wangemzungumzia Athuman China au Method Mogella, au Hussein Marsha au mchezaji mwingine yeyote yule.
Hatukuweza kuamini kama wanasema kweli kwa namna ambavyo walikuwa wanatoka katika mataifa makubwa kisoka. Siku hizi kupitia kwa wachezaji kama kina Kagoma ndio tumeanza kuamini. Sio yeye tu Kagoma, bali kuna wachezaji wengi ambao wanatufanya tuamini. Mfano wa Kagoma anavyozima katika dimba na kuwa tegemeo huku MVP wa Nigeria mheshimiwa Okejepha anavyokalia benchi mara nyingi.
Pale katikati safu ya ulinzi ya Simba kuna Hamza Abdulrazak anaanza na ni kijana wa mtaani. Miongoni mwa mabeki bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita, Karaboue Chamou anakaa nje. Hawa wanaokaa nje sio wachezaji wabaya ila wachezaji wetu wamewazidi uwezo. Hapa ndipo ninapokumbuka zile kauli za makocha wa zamani kutoka nje kwamba wachezaji wetu walikuwa wanastahili kucheza Ulaya lakini tukadhani wanafanya mzaha.

Na hapa ndipo mdogo wangu, Kagoma amenikumbusha namna ambavyo tuna wachezaji wetu wengi wanaoishia ghetto. Mambo ni mengi. Kwanza kabisa mchezaji mwenyewe hajitambui sana. Halafu maisha yaliyomzunguka tangu utotoni hadi sasa yamemfanya asijitambue sana. Kuanzia kiburi cha kuona unaweza hadi kiburi cha kuwa na ‘connection’ nyingi ambazo wenzetu Wanigeria na wengineo wanazo.
Baadaye mchezaji kama yeye anayachukulia maisha kiurahisi tu. Haoni kama anaweza kufanikiwa zaidi ya alivyofanikiwa. Hakuna watu wa kumsukuma wala yeye mwenyewe hawezi kujisukuma. Mwishowe kabisa anaishia ghetto. Tumepoteza wachezaji wengi kwa staili hii. Na sio tu katika hilo, bali hata katika nidhamu binafsi ya mchezaji mwenyewe. Nasikia akiwa na Singida, Kagoma angeweza tu kuamua kurudi home na kupumzika bila ya sababu wakati Ligi inaendelea. Hawa ni aina ya wachezaji ambao wanajilea zaidi wenyewe kuliko kulelewa katika maadili ya soka kama ambavyo wenzetu kule Afrika Magharibi wanalelewa.
Mfano mwingine mdogo ni kama huu wa kusaini timu mbili. Simba na Yanga. Hadi leo tuna wachezaji wa ghetto ambao wanaweza kusaini mikataba ya timu mbili tofauti ndani ya dirisha moja. Hawaoni athari za kufanya hivyo. Inakuwa ngumu kwa mchezaji wa kisasa anayejitambua kuweza kufanya hivyo.
Lakini tukiachana na hilo. Mfano Kagoma akiendelea na moto huu huu halafu mwisho wa mkataba wake na Simba akahitajika kuendeleza huduma zake klabuni, unadhani anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi klabuni? Hapana. Anayemsimamia au yeye mwenyewe anaweza kujenga hoja za msingi kwamba Kagoma alipwe zaidi kuliko Fernandes Mavambo?

Mwisho wa kila kitu Kagoma amenikumbusha namna ambavyo daima Taifa Stars itaendelea kuwa katika mikono salama kwa miaka mingi ijayo. Taifa lenye vipaji litaendelea kuzalisha vipaji vya miaka mingi kadri Mungu alivyouliumba. Mipango yakinifu tu ndio ambayo inaweza kulitoa taifa yakinifu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Itazame Stars ya kina Mbwana Samatta na Himid Mao ambavyo inaenda kupokewa na hawa kina Kagoma na Clement Mzize. Ni jukumu lao kujitambua kwenda kucheza katika kiwango cha juu zaidi ya hapa, au ni jukumu la TFF kuendelea kuihudumia timu ya Taifa na timu nyingine za taifa kama inavyofanya sasa.
Bado kuna vipaji vingi ambavyo vinacheza kwingineko nje ya Simba na Yanga na vinaiacha Stars ikiwa katika mikono salama. Tatizo bado hawajafika katika timu zetu au ndio kwanza wamefika. Kama una Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca ambao wanacheza usisahau kukumbuka kwamba Hamza Abdulrazak hachezi bado na ni kijana mdogo.