JICHO LA MWEWE: Fei Toto na Yanga wapendane ili iweje!

Muktasari:

  • Nilimsikia shabiki mmoja wa Yanga, Ray Kigosi akilalamika namna ambavyo Fei aliweka kidole mdomoni kama ishara ya kuwanyamazisha mashabiki wa Yanga baada ya kufunga penalti yake wiki iliyopita katika pambano la fainali ya FA.

NDIO mpira wenyewe ulivyo. Namaanisha namna ambavyo Yanga wanachukiana na Fei Toto, au tuseme ambavyo Fei Toto anavyochukiana na Yanga. Ndio mpira wenyewe. Wapendane ili iweje? Kwani waliachanaje?

Nilimsikia shabiki mmoja wa Yanga, Ray Kigosi akilalamika namna ambavyo Fei aliweka kidole mdomoni kama ishara ya kuwanyamazisha mashabiki wa Yanga baada ya kufunga penalti yake wiki iliyopita katika pambano la fainali ya FA.

Baadaye zikasambaa video nyingi zikimkejeli Fei kwa ubingwa ule wa Yanga. Kuna ile ambayo anaonekana akiwa anakimbilia vyumbani baada na kukacha kuchukua medali yake. Kuna picha pia ambayo inamuonesha Fei akiwa katika usawa mmoja na kombe.

Nadhani Fei aliwafunga mdomo Yanga na kidole kwa sababu mbili. Kwanza kabisa katika pambano la Ligi aliwafunga Yanga na akajaribu kuomba radhi, lakini haikusaidia. Kila alipoenda katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram aliendelea kuambulia matusi tu.

Lakini hata katika pambano lenyewe la Yanga na Azam pale katika ardhi ya kwao alijikuta akiambulia matusi na kuzomewa tu. Mwisho akaona ngoja na yeye arudi katika chuki yake. Kumbe kuomba suluhu kusingesaidia kitu. Na yeye ameamua kuweka wazi hisia zake hadharani.

Kwani siku ile wakati alipowafunga Yanga na kuwaomba radhi alitegemea nini? Kwamba wamsamehe? Isingewezekana. Mazingira ya kuondoka yalikuwa ya chuki. Namna alivyosema kwamba wamemlisha ugali na sukari isingewezekana tena kujenga daraja la uhusiano na watu wenye hasira. Watu ambao wanaamini hakuwa na sababu ya kuwaacha.

Kama West Ham walimzomea Declan Rice na Everton walikuwa wanamzoea Wayne Rooney kila aliporudi Goodson Park itakuwa Fei na Yanga? Hawa wawili waliondoka katika timu ndogo wakaenda katika timu kubwa, tena ambazo hazina upinzani wa jadi na timu zao.

Rice alikulia West Ham kama kinda. Rooney akakulia Everton kama kinda. Rice akapata nafasi ya kwenda timu kubwa zaidi, Arsenal. Klabu yake ikapata pesa. Hata mashabiki wa West Ham wanajua kwamba Arsenal ni wakubwa kuliko wao na Rice amekwenda katika timu anayostahili zaidi. Hata hivyo, walimzoea Rice aliporudi kucheza dhidi yao. Na katika pambano la mwisho ambalo West Ham walipaswa kuizuia Man City ili Arsenal awe bingwa, wao wakafurahi kuona wamefungwa na Rice amekosa ubingwa na Arsenal. Itakuwa Fei?

Rooney alienda timu kubwa zaidi Manchester United lakini Everton hawakuwahi kuafiki. Kila siku alipokuwa anatembelea Goodson Park walikuwa wanamzomea. Itakuwa Fei? Mashabiki huwa hawaamini sababu zozote za kimsingi za mchezaji wao bora kuhamia kwingine. Hata sababu ya kibiashara inabakia kuwa ya viongozi tu.

Mchezaji ambaye anaondoka bila ya chuki na mashabiki wanamkubali ni yule ambaye ameisha. Ni yule ambaye ameenda kucheza mbali na upeo wa macho yao. Ni yule ambaye amezeeka. Ukiwa wa moto kama Fei halafu umeenda kwa wapinzani hakuna anayeweza kukuelewa.

Kama Fei angeuzwa kwenda zake Mamelodi halafu akarudi kucheza na Yanga wasingemzomea. Mwisho wa mechi wangemshangilia. Lakini kwa mazingira aliyoondoka basi ni jambo la kawaida tu katika soka kuwa katika kisiwa cha chuki. Mchezaji mwingine ambaye hazomewi ni yule ambaye kiwango chake ni cha kawaida tu wakati anaondoka klabuni.

Nini kinatokea? Kwa mchezaji jeuri inamtia nguvu zaidi. Anajaribu kumuonyesha mpenzi wake wa zamani namna ambavyo anaweza kuishi bila yeye. Labda ndio maana Fei amekuwa na msimu bora kuliko msimu wowote ule tangu aanze kucheza soka.

Anaamka kitandani akiwa na hasira ya kuthibitisha ubora wake. Chuki za mashabiki wa Yanga kwake zimekuwa chachu katika mafanikio ya msimu huu. Na kama alikuwa anategemea Yanga wamsamehe na wampende, yaani ili iweje? Wafurahie mabao yake?

Kwa upande wa Yanga nao pia ni chachu. Unaona namna ambavyo wanatamba kuwa wameendelea kufanikiwa bila yeye. Wanacheza huku wakijaribu kuthibitisha kwamba kuondoka kwa Fei hakujawaathiri. Haishangazi kuona katikati ya chuki hii Fei ameendelea kuwa bora na Yanga imeendelea kuwa bora.

Kwa asili ya soka duniani kote, Yanga wataendelea kumchukia Fei hata atakapovaa jezi ya timu ya taifa. Na yeye hawezi hata siku moja kuitakia Yanga mema hata kama wataingia fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Hivi ndivyo inavyokuwa kwa mchezaji aliyehama kwa namna yake.

Njia pekee ya kurudi kwa uhusiano wao ni pale atakapoamua kurudi Yanga. Mashabiki wa soka ni wanafiki. Dakika moja tu ambayo Fei ataamua kurudi Yanga utawasikia wakiambiana “Mtoto ameamua kurudi nyumbani”. Utashangaa kama ni mashabiki hawa hawa ambao kwa sasa vifua vyao vimejaa chuki.

Kwani Yanga walimsamehe Haruna Niyonzima alipoenda Simba? Hapana. Walikuja kumsamehe aliporudi kwao tena kwa mara nyingine. Ndivyo ilivyo duniani kote. Usitegemee usuluhishi mwingine kwa namna yoyote ile.

Yaani Fei na Yanga sasa hivi wapendane ili iweje? Acha wasukumane katika katika mafanikio. Ili mradi hawarushiani mawe basi acha tu wachambane kwa kadri wanavyoweza. Achilia mbali haya mapenzi ya kawaida ya mwanamke na mwanaume basi, mapenzi mengine mabaya zaidi ni ya mpira. Hauwezi kufanya chochote Yanga na Fei wapendane kwa sasa.

Kwa sasa tuendelee tu kukaa na bisi zetu huku tukitazama filamu hii ya kusisimua kwa sasa katika soka. Sitazamii kama itaisha msimu ujao. Itaendelea kuwepo hata kama Fei ataamua kuhamia timu nyingine ambayo sio Yanga. Huu ni ukweli ambao hauwezi kuuzuia. Wapendane ili iweje?