JICHO LA MWEWE: Dejan alikuja kama upepo, ameondoka kama upepo

Siku 52 za Dejan Simba, utata wa kuondoka

IILIKUWA miongoni mwa safari fupi ambazo mchezaji anaweza kufanya na klabu. Ni kama safari hii ambayo mshambuliaji anayeitwa Dejan Georgijevic amefanya katika klabu ya Simba. Alikuja kama upepo na ameondoka kama upepo.

Naambiwa ameondoka nchini juzi alfajiri kurudi kwao Serbia. Tutamkumbuka kiasi. Mzungu wa kwanza kucheza Simba. aliwasili nchini wakati timu yake ikiwa imerejea kutoka Misri ambako waliweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Alikuwa mchezaji wa mwisho kusajiliwa na Simba, lakini hapo hapo akawa mchezaji wa mwisho kutambulishwa na Simba katika siku yao maalumu ya Simba Day. Tukamsikia MC akitamba “Hatujamalizaaa mlete Mzungu”.

Ghafla kila kitu kimefika mwisho. Kwanini? Dejan mwenyewe alituandikia katika ukurasa wake wa Instagram kwamba mkataba wake umevunjika kwa sababu klabu yake imevunja baadhi ya vipengele katika mkataba.

Simba wakamjibu usiku wake katika maelezo ambayo hayakufafanua sana zaidi ya kumlaumu Dejan kwa kulichukua suala lake na kulipeleka mitandaoni. Baadaye nikataka kujua zaidi kutoka kwa watu wa Simba kuhusu mgogoro wao na Dejan.

Kuna utata hapa. Naambiwa Dejan alikuwa ana madai yake kuhusu mishahara, Bonasi pamoja na pesa ya usajili wake ambayo alikuwa hajamaliziwa. Huu ni uzungu ambao Dejan alikuja kutuonyesha katika maisha ya soka.

Kitu kingine ambacho naambiwa Dejan alikuwa hajatimiziwa ni nyumba. Kuna mahali alipelekwa akaishi lakini akagoma wakati nyumba hizo hizo wameishi wachezaji wengi wa kigeni wa Simba. akaishia kukaa hotelini.

Hapa unaweza kuwaelewa viongozi wa Simba. Haya ndio matatizo ya wazungu. Wanataka kuishi katika viwango vya kwao wakati wapo bara la Afrika. Na hata kule Ulaya huwa wana shida hizi. Niliwahi kwenda Genk na kumkuta Mbwana Samatta anaishi katika nyumba ambayo nilidhani ni ya kifahari, lakini akaishia kuniambia kuna mshambuliaji wao wa Kigiriki alikataa kuishi katika nyumba hiyo kwa madai kwamba haikufikia kiwango.

Wakati mwingine ukimchukua mchezaji kutoka Ulaya akaja Afrika moja kwa moja haya ndio matatizo yake. Hiki ndicho ambacho unaweza kuvuna. Afadhali umchukue mchezaji Mwafrika aliyekulia Afrika kisha akaenda kucheza Ulaya halafu ukamrudisha, kuliko kumchukua Mzungu aliyezaliwa kule na kukulia kule.

Inawezekana Clatous Chama anaidai Simba, inawezekana Aishi Manula anaidai Simba, Inawezekana hata Augustine Okrah anaidai Simba. Uzuri wao wamecheza mpira wa Afrika na wanaweza kukuelewa katika baadhi ya mambo.

Huku kwetu unaweza kuambiwa “Subiri tajiri arudi ameenda Dubai katika kazi zake, akirudi tutakulipa.” Kwa huku ni rahisi Jonas Mkude akakuelewa lakini sio kwa mchezaji kama Dejan. Hawa wamekulia katika mifumo ya kizungu zaidi. wakati mwingine ni vigumu kuishi nao.

Ni kama makocha wazungu wanaokuja Afrika. Kuna wale ambao wanakuja moja kwa moja na kujikuta wanaondoka ghafla kwa sababu wanakutana na mazingira magumu ya kazi. Lakini kuna wale ambao tayari wameshazoea mazingira ya soka letu. Hawa ndio kina Micho.

Hata hivyo, kuondoka kwa Dejan nadhani kumeleta neema kwa watu wa Simba. sijui kama ataibukia Fifa au vinginevyo lakini ni wazi kwamba kama angekuwa katika kiwango bora uwanjani sidhani kama Simba wasingemtimizia mahitaji yake.

Katika kiwango ambacho Okrah anaonyesha Simba nadhani viongozi wataogopa kutomtimizia anachotaka kwa sababu kama akiamua kufungasha virago na kurudi kwao Afrika Magharibi viongozi hawatakuwa na kuwaambia mashabiki kisha wakaeleweka.

Sidhani kama viongozi wa Simba walifanya juhudi kubwa kuhakikisha Dejan anabaki. Hakufikia matarajio ya mashabiki wala viongozi na ndio maana hauoni kama mashabiki wanawapigia kelele viongozi wao kuhusu habari ya kuondoka kwake. Kama angekuwa Chama au Moses Phiri basi hadithi ingekuwa tofauti na Msimbazi kungewaka moto.

Ndani ya uwanja Dejan alionekana kama ana kitu fulani hivi. Hata hivyo, kadri ambapo watu walikuwa wanakisubiri kitu chenyewe hawakuweza kukiona. Kumbukumbu yake kubwa aliyotuachia ni bao alilofunga dhidi ya Kagera. Kiasi tulianza kuamini kwamba alikuwa ana kitu. lilikuwa bao la kishambuliaji hasa.

Baada ya hapo kiwango chake kikawa cha kawaida. Tatizo kubwa ambalo Dejan amekumbana nalo nchini ni kwamba ameikuta Simba ikiwa haipo sawa. Presha imekuwa kubwa kwa wachezaji wageni kufanya mambo makubwa.

Tatizo hili pia limeendelezwa na ukweli kwamba watani wao Yanga wapo vizuri na wamekuwa wakimtumia Dejan kama vile alama ya Simba kushindwa kusajili vema katika dirisha lililopita. Yanga badala ya kumuongelea Phiri wanageuza shingo zao na kupeleka kejeli kwa watu wa Simba kupitia kwa Dejan.

Dejan angefurahia maisha ya Simba na kuvumiliwa kama angeikuta Simba ya moto ambayo imepita miezi 24 iliyopita. Ingekuwa rahisi kwake kuingia uwanjani baada ya Jose Luis Miquissone, Meddie Kagere na Clatous Chama kumaliza kazi. Lakini kwa sasa kuna presha kubwa pale Simba. ushindi umekuwa mgumu na kuna kundi kubwa la wachezaji hawachezi katika baadhi ya nyakati.

Wakati mwingine sio wageni tu kama yeye, bali hata wachezaji makinda wanapata utulivu mkubwa wa kukua kisoka kama wanaingia katika timu ambayo inafanya vizuri na ina wachezaji wengi wakomavu. Ni kama Simon Msuva alivyofanikiwa kuingia Yanga iliyokuwa na wachezaji mahiri nyakati zile.

Hata hawa kina Israel Mwenda wanapata wakati mgumu kufanya vema zaidi kwa sababu wameikuta timu imeyumba kiasi. Uwezo wa kujiamini wa hata wachezaji wazoefu umeshuka kwa namna moja au nyingine.

Wosia wangu kwa Simba ni kwamba wasirudie kuteseka kutafuta wachezaji wa Ulaya waliozaliwa Ulaya. Bado Afrika ina wachezaji wengi wenye viwango vikubwa zaidi ya Dejan. Yanga hawakwenda Ulaya kumpata Fiston Mayele na wala Simba hawakwenda Ulaya kumpata Moses Phiri.