JESCA; Mtoto wa mwamuzi anayezichapa ‘kiume’
Muktasari:
- Jesca mwenye umri wa miaka 26, anayepigana uzani wa super flyweight (kilo 52), amesema moja ya vitu vinavyomuumiza ni watu kuamini kuwa mwanamke anayepigana ngumi lazima awe jike dume au aishi maisha tofauti na wanawake wengine.
UKIMUONA akiwa ulingoni anarusha ngumi unaweza kudhani ni mwanamke mwenye maisha ya ukakamavu muda wote au mbabe fulani hivi. Lakini nje ya ulingo, bondia wa kike Jesca Mfinanga ni mwanamke anayependa urembo, biashara ndogondogo na maisha ya kawaida kama wasichana wengine.
Jesca mwenye umri wa miaka 26, anayepigana uzani wa super flyweight (kilo 52), amesema moja ya vitu vinavyomuumiza ni watu kuamini kuwa mwanamke anayepigana ngumi lazima awe jike dume au aishi maisha tofauti na wanawake wengine.
Akizungumza na Mwanaspoti, Jesca anasema ameamua kutenganisha maisha ya kazi yake ya ubondia na binafsi ili kuwafanya mabinti wengine wasiuogope mchezo huo.
“Watu wengi wakimuona bondia wa kike wanaamini lazima awe mkorofi au anaishi maisha ya kiume, lakini mimi napenda sana urembo na kujitunza. Mimi ni mwanamke wa kawaida kabisa,” anasema Jesca.
Anasema licha ya kutumia muda mwingi mazoezini, bado anapenda kupendeza, kuvaa vizuri na kufuatilia maisha ya mabondia wa kike wa kimataifa ili kujifunza namna wanavyoishi nje ya ulingo.
Miongoni mwa mabondia anaowafuatilia kwa karibu ni Seniesa Estrada maarufu kama “Super Bad” pamoja na Claressa Shields.
“Napenda kuona wanawake wanaonyesha kuwa ngumi ni kazi kama kazi nyingine. Unaweza kuwa bondia lakini ukabaki mwanamke mwenye mvuto, mwenye ndoto za kuolewa na kuwa na familia,” anasema.
ALIVYOINGIA KWENYE NGUMI
Jesca amesema kabla ya kuingia kwenye ngumi alikuwa akivutiwa zaidi na sanaa ya uigizaji, hasa filamu za mapigano.
Anasema mlezi wake, Japhet Kaseba ndiye aliyemshawishi aanze kujifunza ngumi ili aweze kuigiza vizuri filamu za mapambano.
“Nilianza mazoezi kwa ajili ya kuigiza lakini baadaye nikajikuta nimeupenda mchezo wenyewe. Kadri nilivyoendelea kufanya mazoezi ndipo nikaanza kuona huu ndio unaweza kuwa maisha yangu,” anasema.
Jesca aliingia rasmi kwenye ngumi za kulipwa mwaka 2019 na pambano lake la kwanza alipigana Februari 8, 2020 dhidi ya Veronica Thomas ambapo alishinda kwa pointi.
UANDISHI WA HABARI NA BIASHARA
Mbali na ngumi, Jesca anasema amesomea uandishi wa habari, lakini hakufanikiwa kumaliza kutokana na changamoto za ada. Hata hivyo, anasema hilo halikumkatisha tamaa kwani aliamua kutumia kipaji chake kujitafutia maisha kupitia ngumi pamoja na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.
“Napenda kujitegemea. Sitaki kutegemea ngumi pekee. Nafanya biashara ndogondogo na pia nafundisha watu mazoezi ya kupunguza uzito na vitambi,” anasema na kuongeza kuwa, wanawake wengi humtafuta kwa ajili ya mazoezi ya kupunguza uzito, kuondoa nyama uzembe na kujenga maumbo yao.
“Warembo ambao hawataki matumbo makubwa au uzito uliopitiliza huwa nawasaidia kufanya mazoezi maalumu. Hii nayo inanisaidia kupata kipato,” anasema binti huyo wa mwamuzi wa ngumi, Pendo Njau.
NIDHAMU
Jesca anasema mchezo huo unahitaji nidhamu ya juu tofauti na watu wanavyowachukulia mabondia kama watu ambao hawana nidhamu kubwa.
Kwa kawaida hufanya mazoezi mara mbili kwa siku, lakini kipindi cha maandalizi ya pambano anafanya hadi mara tatu kwa siku.
Anasema hata anapokuwa kwenye siku zake za hedhi hulazimika kujikaza ili kutopoteza ratiba ya mazoezi.
“Kama maumivu yanakuwa makali sana napumzika kwa muda, lakini lazima nimwambie kocha ukweli ili ajue namna ya kunipangia mazoezi,” anasema.
Aidha anasema mchezo huo unahitaji bondia kujitunza kwa kufuata maelekezo ya kocha kuhusu lishe, mapumziko na mwenendo wa maisha.
Jesca pia amempongeza mpenzi wake kwa kuelewa kazi yake na kumpa ushirikiano kipindi anapokuwa kwenye maandalizi ya mapambano.
“Nikiwa kwenye maandalizi ananielewa kabisa. Lakini nikiwa huru nafanya kila kitu kama mwanamke mwingine, napika, nafua na kufanya kazi zote za nyumbani,” anaeleza.
KILICHOMKUTA SAUZI HATASAHAU
Mwaka 2024, Mfinanga alipata safari ya kwenda Afrika Kusini kupigania ubingwa wa Afrika dhidi ya Simangele Hadebe, lakini safari hiyo iligeuka kuwa mateso makubwa kwake. Jesca anasema changamoto zilianza tangu walipowasili Johannesburg baada ya kudai kuwepo mazingira yasiyo ya kawaida kwenye maandalizi ya pambano, ikiwamo kile alichodai kuwa ni hujuma wakati wa upimaji wa uzito.
“Nilivuliwa nguo zote wakati wa kupima uzito wakitaka kuhakikisha sina ujanja wowote, jambo ambalo liliniumiza sana,” amesema Jesca.
Bondia huyo anasema siku ya pambano walikaa muda mrefu bila chakula huku akidai pambano lake lilisitishwa katika mazingira ambayo hakuyaridhia.
“Nilihisi kudhulumiwa, maana nilikuwa naendelea kushambulia lakini mwamuzi akaamua kusimamisha pambano ikabidi nigome kuondoka ndio changamoto ilipoanzia hapo,” anasema.
Baada ya pambano hilo, Jesca na mwenzake walijikuta wakikwama Afrika Kusini baada ya promota aliyewapeleka kushindwa kuwapatia fedha na tiketi za kurudi Tanzania.
“Pambano lile nilikuwa Napata Milioni 12 nikaona hii sio sawa kwa nini nidhulumiwe ulingoni hadi kwenye pesa tukaanza kufuatiliwa nilinusurika kufa ikabidi tutolewe hotelini na kupelekwa Soweto kwenye nyumba ya mganga wa kienyeji, tulikuwa tunaishi kwa hofu kubwa,” anasema.
Hali hiyo iliwalazimu kuomba msaada kupitia video walizorekodi hadi zilipowafikia viongozi wa mchezo huo Tanzania pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
“Balozi James Bwana ndiye aliyetuokoa, tukahamishwa kule na kuishi ubalozini hadi taratibu za kurudi nyumbani zilipokamilika lakini walifuatilia hadi nikapewa pesa zangu ingawa hazikuwa zote,” anasema Jesca.
Anaeleza kuwa tukio hilo ameliweka kwenye kitabu cha kumbukumbu na kumfundisha kuwa maisha ya ngumi yanahitaji moyo mgumu hasa unapopigana nje ya nchi.
KWA NINI WANAWAKE HAWAONEKANI
Jesca anasema changamoto kubwa inayowakabili mabondia wa kike Tanzania ni ukosefu wa maslahi mazuri na kutopata sapoti sawa na wanaume.
Anawataja mabondia wa kiume kama Ibrahim Class au Hassan Mwakinyo hupata nafasi kubwa zaidi kutokana na ukubwa wa majina yao.
“Wanawake wengi wana vipaji lakini wanakata tamaa kwa sababu mapato ni madogo sana. Kuna bondia analipwa Sh200,000 kwa pambano, hiyo pesa haitoshi hata kwa maandalizi,” anasema.
Anaeleza wengi hulazimika kupigana mara nyingi ili kutafuta fedha za kujikimu badala ya kupanga vizuri maendeleo ya taaluma zao.
WANAUME WANAMUOGOPA
Jesca anasema mwanzoni wakati anaanza kupigana wanaume walikuwa wanamuogopa hata kumtongoza wakiamini maisha ya ulingoni sawa na maisha halisi.
“Walikuwa wanaamini labda nina vurugu au nina tabia za ugomvi. Lakini baada ya kunifahamu wakaona mimi ni mtu wa kawaida tu,” anasema huku akicheka.
Ila kwa sasa watu wengi wanamheshimu na kuelewa kuwa ubondia ni kazi kama kazi nyingine.
REKODI ZAKE
Kwa mujibu wa BoxRec na tovuti zinazofuatilia rekodi za mabondia duniani, Jesca Mfinanga ana rekodi ya mapambano 12 ya kulipwa, akishinda saba, kupoteza manne na kutoka sare moja.
“Ngumi imenipa maisha, imenipa kiwanja, imenipa nafasi ya kujulikana na kukutana na watu mbalimbali. Bado nina ndoto kubwa sana,” anasema.