Ishu ya ratiba, TFF yavunja ukimya

BAADA ya tetesi za kuwa huenda Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ikasogezwa mbele hadi mwezi ujao kupisha majukumu ya timu za taifa kwenye mechi za kirafiki, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limefafanua juu ya taarifa hiyo.

Awali, duru la pili la ligi hiyo lilipangwa kuanza Machi 12 kulingana na ratiba iliyokuwepo, lakini ilikwama kwa sababu ya kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa, hivyo kwa sasa ligi hiyo inatarajiwa kuanza Machi 29 kwa michezo mitano kupigwa kwenye viwanja tofauti, bingwa mtetezi JKT Queens atacheza na Bunda, Ceasiaa dhidi ya Simba Queens, Amani Queens itaivaa Fountain Gate Princess, Geita Queens itaikabili Alliance Girls na Yanga Princess itakipiga na Baobab Queens.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema hakuna kilichobadilika kwenye ratiba hiyo na mechi zitachezwa kama zilivyopangwa.

"Hatujatoa taarifa yoyote kuhusu mechi kusitishwa hivyo hizo habari sio rasmi na ratiba iko pale pale," alisema Ndimbo.

Simba inaongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 25, JKT iko nafasi ya pili na pointi 19, Yanga Princess pointi 18 huku Ceasiaa ina pointi 16.