Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

GARRINCHA: Mbrazili fundi wa mpira, aliyeangushwa na pombe

KIJIWE Pict

Muktasari:

  • Pia wamekuwapo wajanja waliowazidi wapinzani wao maarifa, waliokuwa na visa, mikasa na vituko vilivyonifanya niwaone sio watu wa kawaida.

KATIKA kuandika habari za michezo kuanzia miaka ya 1960, nimekutana na kusikia habari za wachezaji makini, mahiri, jasiri na makatili.

Pia wamekuwapo wajanja waliowazidi wapinzani wao maarifa, waliokuwa na visa, mikasa na vituko vilivyonifanya niwaone sio watu wa kawaida.

Nimeona mengi katika mashindano ya Gossage (sasa Kombe la Chalenji la Afrika Mashariki na Kati), makombe ya klabu na nchi za Afrika, na fainali za Kombe la Dunia Uingereza (1966) na Mexico (1970).

Katika wachezaji walionivutia kwa mengi mbali ya mchezo wao, sitamsahau Garrincha wa Brazil.

Nilikutana na Garrincha (Manuel Francisco dos Santos) kwa mara ya kwanza nilipokwenda kumfanyia mahojiano Grand Hotel Bohemia, iliyopo Prague, Jamhuri ya Czech, mwaka 1965 nilipokuwa ninasomea uandishi wa habari.

Alikuwa mcheshi na mwenye mikasa na nilipomgusia niliposikia anapenda pombe, aliniambia kila mtu alikuwa na kitu alichokipenda.

KIJI 01

“Wengi hupenda harufu ya mafuta mazuri, lakini wapo wanaopenda harufu ya kinyesi,” aliniambia huku akitabasamu. Jawabu lake lilitosha kuniambia nilikutana na kiumbe wa ajabu.

Garrincha (ndege mdogo) alikuwa mchezaji mashuhuri wa Brazil wa miaka ya 1950 na 1960 na aliisaidia kubeba Kombe la Dunia 1958 na 1962.

Ulevi ulimharibia maisha na kupelekea kupata ajali za gari zaidi ya mara 10, lakini kifo chake mwaka 1983 kilitokana na maini kuoza kutokana na pombe nyingi. Alikuwa wa kwanza kuingia baa ilipofunguliwa na wa mwisho kutoka.

Alipenda mabibi na ilikuwa kawaida kuzungukwa na vimwana hata 10 na kila mmoja alisema ni mpenzi wake. Aliwahi kueleza kwamba alianza maisha ya mapenzi akiwa na miaka 12.

Garrincha aliudhibiti mpira kwa ustadi kwa kupiga chenga za maudhi na kumalizia kwa kusukuma kombora la urefu wa kimo cha kuku au mbuzi.

Kilichoshangaza ni kuwa miguu yake ilipinda tangu alipozaliwa na mmoja ulikuwa mfupi kidogo kuliko mwingine kwa nusu inchi.

Alifanya maajabu alipokuwa mchezaji wa pembeni katika miaka ya 1950 na 1960 kwa kumiliki mpira kama vile miguu yake ilikuwa na sumaku na kuvutia watazamaji kwa kutimua mbio na mpira kwenye chaki kuelekea kwenye kibendera cha kona.

KIJI 05

Alikuwa mfungaji bora katika fainali za Kombe la Dunia za 1958 na 1962 ambapo Brazil ilibeba Kombe la Dunia.

Mwishoni mwa fainali za 1962 zilizofanyika Chile, gazeti moja la nchi hiyo liliuliza: “Huyu Garrincha ni kiumbe aliyetokea dunia ipi?”

Katika michezo yake zaidi ya 30 akiwa na Pele, Brazil haikupoteza hata mchezo mmoja, na mashabiki wa soka walisema wachezaji hawa walipokuwa pamoja mchezo ulianza kwa Brazil kuongoza 2-0, moja la Garrincha na jingine la Pele.

Mwishoni mwa 1999 alitangazwa na Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (FIFA) kama mchezaji bora namba 7 wa karne ya 20.

Aliichezea klabu ya Botafogo kwa miaka 12 na kwa kuheshimu mchango wake, chumba kilichotumiwa na klabu hiyo kwenye uwanja maarufu wa Maracana kimepewa jina la Garrincha.

Katika hali ya kawaida usingetarajia kwa umbile lake na matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo kuwa mchezaji nyota wa kandanda. Uti wa mgongo wake ulipinda na mifupa ilikuwa laini kuliko kawaida. Mguu wa kulia ulipinda mbele kama mche uliokufa na wa kushoto ulikuwa mfupi kuliko wa kulia.

KIJI 02

Alipokuwa mdogo baba yake hakumshughulikia kutokana na kutawaliwa na ulevi, sifa aliyokuja kuirithi Garrincha.

Licha ya ulemavu wa miguu, uti wa mgongo wenye matatizo, umbo dhaifu na kama vile alikuwa na utapia mlo, Garrincha alifanya mambo ambayo wasiokuwa na matatizo kama yake hawakuyamudu.

Magoli yake mengi yalikuwa ya kuwapiga chenga walinzi na golikipa.

Alijiunga na timu ya Brazil mwaka 1958 baada ya kung’ara alipozichezea klabu za Atletico Junior na baadaye Flamengo aliyokuwa nayo mpaka 1969.

Garrincha aliniacha hoi nilipomuona kwa mara ya kwanza akiwa amelewa na kuichezea Brazil ilipotembelea Prague 1965.

Brazil ilipowasili Prague, gazeti la Rude Pravo lilikuwa na makala ya Garrincha na picha zake nyingi. Radio Prague na kituo cha televisheni vilizungumzia vituko vyake vya kuwala chenga walinzi na golikipa na kufunika uso kwa mkono alipousindikiza mpira wavuni.

KIJI 04

Brazil ilipokutana na Czechoslovakia, Garrincha hakuteremka uwanjani na hakuwepo kwenye ubao wa wachezaji wa akiba.

Mashabiki walivamia uwanja na kusema walifika kumuona Garrincha na kutaka mchezo uahirishwe hadi siku Garrincha atapoweza kuingia uwanjani.

Polisi walijaribu kutuliza hasira za mashabiki na hawakufanikiwa mpaka ilipoelezwa alikuwa njiani anakuja. Polisi walitumwa kumtafuta na walimkuta akiwa katika baa jirani na hoteli aliyofikia akichapa bia ya Pilzen (jina hili la mji maarufu wa Jamhuri ya Czech ndilo lililozaa bia inayojulikana kwetu kama Pilsner), aliyochanganya na vodka ya Urusi.

Askari walimbeba pamoja na pombe yake na kufika naye uwanjani akipepesuka na kupelekwa katika chumba cha kubadilisha nguo.

Baada ya dakika chache mchezaji mmoja wa Brazil alitoka na Garrincha aliingia. Niliwaambia waandishi wenzangu tutegemee kuona kivuli cha Garrincha kwa vile alikuwa amelewa, lakini alilisakata kabumbu na kuwapiga chenga walinzi kwa ustadi na kumchukua dakika 15 tu kufunga mabao mawili, na baada ya hapo alitoka akijidai ameumia.

Mchezo ulipoendelea alipenya kwenda baa kwa awamu ya pili ya kunywa pombe.

Garrincha alitakiwa na klabu za Juventus ya Italia (1954), Real Madrid ya Hispania (1959) na Internationale na AC Milan za Italia mwanzoni mwa miaka ya 1960, lakini alikataa.

Aliichezea Brazil michezo 50 na kustaafu baada ya fainali za Kombe la Dunia za 1966 zilizofanyika Uingereza.

KIJI 03

Alipoichezea Brazil walifungwa mara moja tu na Hungary na alisema hiyo ilitokana na kutokuwa na pacha wake Pele aliyekuwa ameumia.

Moja ya mabao yake yanayozungumzwa sana ni lile la kabla ya fainali za Kombe la Dunia za 1958.

Aliwapiga chenga walinzi wanne wa Italia na golikipa, na alipolikaribia goli alirudi nyuma na kuwala tena chenga na baadaye kuukwamisha mpira wavuni.

Kioja kingine ni Botafogo ilipocheza na Palmeiras. Alipoupata mpira alikwenda kwenye goli la timu yake, akampigia saluti golikipa na kurudi nyuma na mpira.

Aliwakata chenga wachezaji sita na golikipa na kuipatia bao Botafogo. Kisha aliukota mpira wavuni, akautia kwapani na kwenda mbio hadi golini kwao, akaudunda na kuutia kimiani.

Baadaye alieleza kwamba alimwambia muamuzi mpira uendelee kwa matokeo ya 1-1 na magoli yote yakiwa amefunga yeye.

Alipostaafu, aliandaliwa mchezo wa kumuaga mwaka 1973 na watazamaji 131,000 walifurika Uwanja wa Maracana kumuaga. Baada ya hapo ikawa yeye na pombe na pombe na yeye, na mara kadhaa alipata ajali alipokuwa akiendesha gari akiwa amelewa.

Mara nyingi alipigana na watoto wake wapatao 20, kati yao 14 wakiwa wa nje ya ndoa aliozaa na warembo wa Brazil.

Mnamo mwezi Januari 1983, Garrincha alipoteza fahamu kwa siku mbili kutokana na pombe na alipopata nafuu alikataa kuacha pombe iliyomtawala kama alivyoutawala mpira.

Mara nane alilazwa hospitalini kwa kuzidiwa na pombe na aliaga dunia akiwa na miaka 49.

Kati ya matukio yanayokumbukwa katika fainali za 1962 zilizofanyika Chile ni la mbwa kuingia uwanjani Brazil ilipocheza na England na mchezo kusimama.

Mbwa wa Jimmy Greaves wa England alikuwa pembe za chaki akiangalia Garrincha alivyokuwa akiwapiga chenga wachezaji. Mbwa huyo aliingia uwanjani na kumrukia Garrincha kama paka anavyomfanyia panya. Mbwa huyo alimkojolea na ilimbidi Garrincha abadili sare.

Garrincha alisema msako wa mbwa ulimfurahisha kuliko ushindi wa 3-1 dhidi ya England.

Garrincha aliyechaguliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa mchezaji bora, alimchukua mbwa huyo na kwenda naye Brazil baada ya kuifunga Czechoslovakia 3-1 katika fainali.

Alisema Brazil ilishinda kombe na yeye alishinda kumpata mbwa, zawadi kutoka kwa rafiki yake Jimmy. Alimpa yule mbwa jina la JG, yaani Jimmy Greaves.

Siku ya mazishi yake, Jimmy alibeba picha ya Garrincha akiwa na mbwa na kuiweka juu ya kaburi na kusema: “Kwaheri rafiki mpenzi.”

Kama pombe ilivyomharibu Garrincha, ndivyo ilivyomtibua Jimmy na kumlazimu kulazwa hospitali ya wagonjwa wa akili, lakini hatimaye aliamua kuacha pombe.

Miaka michache iliyopita, mabaki ya mwili wake yalifukuliwa na kukatwa mifupa ya miguu.

Wapo wanaoshuku washirikina wanaosaka mafanikio katika kandanda huenda ndio walioiiba mifupa hiyo, na wengine wanadhani yupo daktari aliyetaka kugundua Garrincha alikuwa na siri gani miguuni hata akapiga chenga zilizompatia umaarufu.