Ile Mbeya City dume hii hapa!

Muktasari:
- Kama hujui, Mbeya City ilipanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 na kuvitetemesha vigogo vya soka zikiwamo Simba, Yanga na Azam FC.
MBEYA City imerudi tena Ligi Kuu Bara ikiwa ni misimu miwili tu tangu iliposhuka daraja 2022-2023 baada ya kuicheza ligi hiyo kwa takribani miaka 10.
Kama hujui, Mbeya City ilipanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 na kuvitetemesha vigogo vya soka zikiwamo Simba, Yanga na Azam FC.
Mbeya City ilipanda na kutembeza boli la maana kiasi cha kukaribia kurejea kile kilichowahi kufanywa na Tukuyu Stars pia ya Mbeya mwaka 1986 ilipopanda daraja na kubeba ubingwa wa ligi hiyo (enzi hizo ikiwa ni Ligi Daraja la Kwanza).
Wabeba hao walimaliza msimu huo wa kwanza ikiwa nafasi ya tatu, nyuma ya waliokuwa mabingwa Azam FC, Yanga na kuipiku hadi Simba iliyomaliza ya nne.
Wagonga Nyundo hao wa Mbeya maarufu kama Wanakoma Kumanya, ikiwa chini Kocha Juma Mwambusi ilionyesha haikupanda kwa bahati katika ligi hiyo, kwani ilimaliza raundi ya kwanza iliyokuwa na mechi 13 nafasi hiyo ya tatu ha haikutoka hapo hadi mwisho wa msimu.
Si hivyo tu, lakini City katika mechi 26 ilizocheza msimu huo, ilipoteza tatu tu, mbili zikiwa za ugenini dhidi ya Yanga iliyokuwa ya kwanza kuifunga baada ya kucheza mechi 15 mfululizo bila kupoteza, kisha ikafuata Coastal Union na mabingwa wa wakati huo, Azam ikawa timu pekee kuifunga nyumbani.
Hata hivyo, baada ya kuanza msimu kwa kishindo na kuzitetemesha vigogo, Mbeya City ilianza kupunguza kasi taratibu hadi iliposhuka daraja misimu miwili iliyopita kabla ya kurejea tena msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Ligi ya Championship nyuma ya vinara, Mtibwa Sugar.
Mwanaspoti linakukumbushia kikosi kazi kilichotingisha nchi pale iliposhiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, ikiwa timu isiyofungika nyumbani kirahisi hadi Azam ilipofanya hivyo wakati ikitangaza mapema ubingwa kwa kuichapa mabao 2-1.

DAVID BURHANI
Huyu ndiye aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo kipindi hicho na alipokaa langoni ilikuwa ngumu kumtungua kirahisi ndiyo maana siyo ajabu msimu huo ilimaliza ikifungwa mabao 20 ikishika nafasi ya tatu ya timu zilizofungwa mabao machache baada ya Azam (15) na Yanga (19).
Kwa sasa Burhan ni marehemu kwani alikumbwa na mauti Machi 2021, kipindi hicho akiitumikia Kagera Sugar, lakini bado anaendelea kukumbukwa kwa kuifanya Mbeya City kuwa chama dume.
JOHN KABANDA
Beki wa kulia kulikuwa na hii mashine ambayo ilikuwa haina mambo mengi lakini kazi yake ilikuwa kubwa, haikuwa rahisi kupita kwake.
Kabanda alikuwa akipokezana na Aziz Sibo na Hamada Kibopile katika eneo hilo la beki ya kulia na mambo yalikuwa moto kwelikweli.
Kwa sasa Kabanda inaelezwa yuko Morogoro anakoishi, japo haijajulikana kama anaendelea kucheza mpira au la.
HASSAN MWASAPILI
Hii ndiyo iliyokuwa mbavu ya kushoto tegemeo ya City. Mwasapili alikuwa mwamba kwelikweli, kijana fulani mwenye mwili mwembamba na mjuzi wa kutumia mguu wa kushoto kwa kupiga krosi na umahiri wa kukaba na kutengeneza mashambulizi kutokea nyuma.
Mwasapili alikuwa chaguo la kwanza la Kocha Mwambusi na kwa sasa anaendelea kukiwasha akiwa na timu ya Championship ya Mbuni ya Arusha.

YOHANA MORRIS
Beki wa kati kulikuwa na mtu mbishi na mwenye hesabu Yohana Morris ambaye ilikuwa ngumu kupita kwake kirahisi kutokana na nguvu na akili yake.
Alicheza karibu msimu mzima wa kwanza na kuipa heshima timu hiyo, kwa mujibu wa wachezaji wenzake wanaeleza jamaa kwa sasa hachezi tena soka akiwa amepumzika.
DEO JULIUS
Pacha wa Morris alikuwa huyu Deo Julius ambaye naye alikuwa na ubora mkubwa wa kupambana na mipira ya juu, pia kucheza kwa hesabu.
Ukuta huu uliipa nguvu kubwa Mbeya City na inaelezwa kama ilivyokuwa kwa Morris Julius naye amepumzika kucheza soka la ushindani.
Deo alikuwa akipokezana na Yusuf Abdallah ambaye naye alikuwa mtu sana katika eneo hilo la beki ya kati.
ANTHONY MATOGOLO
Katika eneo la kiungo cha ukabaji kulikuwa na mkata umeme mmoja matata, Antony Matogolo, kimo chake kirefu na ubishi aliokuwa nao wa kutibua hesabu za wapinzani ulimbeba na kuipa nguvu timu yake.
Matogolo alisumbua sana kwa kimo chake na utulivu wake, kwa sasa naye amepumzika akijitafuta taratibu nje ya uwanja.
DEUS KASEKE
Winga ya kulia kulikuwa na huyu fundi, Deus Kaseke ambaye ulikuwa unamuona anashambulia kutoka pembeni, pia timu ikipoteza mpira anaingia ndani kuja kukaba.
Kiwango cha Kaseke kiliwachanganya sana Simba na Yanga na kuingia vitani na kumsaka kabla ya Yanga kunasa saini yake kwa umafia uliokuwa unafanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Injinia Issac Chanji, Katibu Mkuu wa wakati huo Dk Jonas Tiboroha aliyekesha kuhakikisha anamsajili wakitumia fedha za aliyekuwa tajiri wao marehemu Yusuf Manji.
Kwa sasa jamaa bado anacheza akiwa pale Pamba Jiji, baada ya kupita Yanga, Singida Big Stars iliyokuwa ikifahamika pia kama Singida Fountain Gate.
STEVEN MAZANDA
Fundi huyu aliyekuwa anacheza dimba la juu akitawanya mpira kwa ufundi mkubwa. Mazanda alikuwa kama mtu asiyekuwa na haraka, lakini kazi yake ilikuwa ya uhakika.
Alisumbua sana na hakuwa mchezaji anayeongea sana, lakini kiwango chake kiliongea kwa niaba yake uwanjani.
Kwa sasa fundi huyo wa mpira amepumzika kidogo kucheza soka la ushindani.

PAUL NONGA
Safu ya ushambuliaji ilikuwa na watu wawili wa kwanza, ni huyu Paul Nonga, alikuwa hatari kwenye kufunga kwa kichwa na hata miguu.
Mabeki wengi walipata tabu kutokana na ubora wake, hakuwa mshambuliaji wa kukata tamaa, alipambana wakati wote, kwa sasa yupo pale Geita Gold kama kocha.
MWAGANE YEYA
Namba 10 bora ya Mbeya City alikuwa huyu mwamba ambaye kitaaluma ni mwalimu, Mbeya City ilikuwa kama timu ya urithi kwake kwa namna alivyokuwa anapambana kutafuta mabao kule mbele kwa vichwa na mashuti makali. Mwamba huyu aliyekuwa akiitumikia timu hiyo huku akiendelea na shughuli yake ya ualimu, ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa timu msimu huo kwa kufunga mabao saba.
Kwa sasa Mwagane alishaacha kucheza soka lakini kuonyesha City bado ni timu yake anaendelea kuitumikia hadi sasa ikirejea Ligi Kuu akiwa kama meneja wake.
SAAD KIPANGA
Winga ya kushoto alikuwa huyu mtu mrefu anayetumia mguu wa kushoto akiwa na nguvu kubwa ya kupiga krosi na mashuti makali na alikuwa akitoka anaingia winga mwingine mkali Alex Joseph Seth.
Kwa sasa Kipanga aliyemaliza msimu huo na mabao matano akimfuata Mwegane kwa mabao, hasikiki sana tofauti na alipotoka City na kwenda JKT Ruvu (sasa JKT Ruvu), Green Warriors na Pamba Jiji japo alirudia Mbeya 2019-2020 lakini hakuwa na makali kama aliyokuwa nayo alipotua hapo akitokea Rhino Rangers aliyoipandisha pia Ligi Kuu msimu kadhaa iliyopita.

KOCHA JUMA MWAMBUSI
Huyu ndiye aliyeifanya Mbeya City kuwa tishio kwa namna alivyoifanya icheze hata kwa dakika 120 na wala isionekane kuchoka, huku ikiwapeleka puta timu pinzani kwa jinsi alivyowajaza pumzi wachezaji na kuwapa mbinu na ari ya kupambana mwanzo mwisho.
Mwambusi msimu huu alikuwa akiinoa Coastal Union walioachana nao hivi karibuni, lakini akiwa amewahi kupita katika timu kadhaa akizipa mafanikio makubwa ikiwamo, Yanga, Azam FC na Ihefu, sasa Singida Black Stars.
MZIKI KAMILI 2013-2014
Alex Joseph Seth, Anthony Mayungu Matogolo, Deogratus Deo Mwashinga, Yohana Morris Ngonye, Hamad Hamza Kibopile, Richard Peter Ngalison, Richard Brown Mwakyoma, Mwagane Yeya Mwanazyembe, Yusuph Wilson Mbijima, John Daud Kabanda na Francis Casto Maganga.
Wengine ni; Geofrey Julius Mwalyego, Yusuph Abdallah Lulinda, Steven David Mazanda, Deus David Kaseke, Hassan Charles Mwasapili, Juma Ramadhan Abdi, Mussa Rajabu Lusewe, Baraka Felix Haule,
Mohamed Said Kijuso, Jeremiah John Mangasin na Kenny Ally Mwambungu.
Pia kulikuwa na mashine nyingine kama; Christian Sembuli Kimwaga, David Abdallah Burhan, Paul John Nyangwe, Paul Michael Nonga, Peter Pascal Mapunda na Azizi Issa Sibo.