Huyu ndiye mpishi wa Simba

Muktasari:

USIONE miili ya mastaa wa Simba ina afya, tabasamu na nguvu, nyuma yake kuna mtu mmoja makini sana, anayejali afya zao kwa kupika madikodiko ya maana, halafu itakushangaza ukimjua ni nani.

USIONE miili ya mastaa wa Simba ina afya, tabasamu na nguvu, nyuma yake kuna mtu mmoja makini sana, anayejali afya zao kwa kupika madikodiko ya maana, halafu itakushangaza ukimjua ni nani.

Simba imemwamini Samwel ‘Sam’ Mtundu katika kitengo hicho kwa muda mrefu sasa ndiye anayefanya wachezaji wa timu hiyo wachanue kutokana na aina ya upishi wake alioukalia darasani na kuumiza kichwa.

Mwanaspoti linafika hadi kambi ya Simba iliyopo Mbweni, kufanya mahojiano na Sam ikiwamo kushuhudia umahiri wake katika mapishi, jamaa ni mtaalamu, akifanya shughuli zake mate yatakudondoka.

“Nina zaidi ya miaka 10 sasa ndani ya Simba nikiwa kama mpishi mkuu,” anaanza kwa kusema Sam akiongeza: ”Kiujumla nilianzia kwenye hoteli mbalimbali kubwa nchini pia kwenye meli nimefanya kama miaka sita hivi,” anasema.


KWANINI UPISHI

Si wanaume wengi wanaopenda kupika ama kuchagua kazi ya upishi, lakini Sam kuna vitu vilivyomvutia huko.

Anasema: “Nilivyokuwa nawaangalia wale wapishi wa shule walivyokuwa wanachezea visu basi nilitamani kufanya kazi kama yao, nilitoka huko nikiwa na hiyo hamu kabisa.

“Nilienda kujiendeleza chuo cha Njuweni Kibaha, Pwani ambako fani yangu ilianzia hapo.”

Anasema wakati anajitosa kusomea kazi hiyo marafiki zake wengi walimcheka na kumuona kama hafai katika jamii.

“Walitaka kunivunja moyo nilipoenda kusomea masuala ya mapishi, lakini leo licha ya kazi zao na elimu zao, nawazidi mshahara wangu mara tano hadi sita.

“Mwisho wa siku niwaambie hoteli inalipa, nilichukua kazi sahihi kabisa katika maisha yangu,”anasema.


KWENYE MELI

Kwenye meli alikaa miaka sita, akiwa mpishi mkuu wa wazungu ambao walikuwa wakifanya utafiti wa masuala ya gesi baharini.

“Tulitembea nchi nyingi sana kupitia baharini, asikwambie mtu kwenye meli sio mchezo inafikia sehemu meli inayumba kama karatasi vile, lakini katika kutafuta maisha hakuna namna unapambana tu, mnakaa baharini mkiwa mmesimama hata miezi mitatu minne,” anasema akieleza changamoto kubwa kwenye meli inakuwa ni upweke.


CHAKULA CHA WACHEZAJI

Anabainisha kuwa, kazi ya kupika chakula cha wachezaji ni ngumu lakini kwa kuwa anajua nini anakifanya ndio maana anaweza kutimiza majukumu hayo bila tatizo kabisa.

Anasema wachezaji wana vyakula vyao ambavyo daktari ndiye anayepanga wale chakula cha aina gani kwa wakati upi.

“Tunawaandalia wachezaji chakula kulingana na aina ya mechi wanayoenda kukutana nayo na eneo husika, nafuata maelekezo zaidi.

“Mfano tunaenda kucheza mechi ngumu, wachezaji wanatakiwa kula vyakula vyenye wanga mwingi, vyakula vyao havina mafuta, vingi ni michemsho,” anasema.

Anasema vyakula vya wachezaji havina viungo vingi kama vya hotelini.

“Vyakula vya hotelini vina viungo vingi sana, tofauti na chakula cha mchezaji, nikiwa napika chakula cha hotelini utasikia harufu ukiwa mbali tofauti na hiki cha wachezaji.

“Chakula cha hotelini kinakaa sana kwenye jokofu tofauti na wachezaji ambao wanakula vitu freshi kabisa,” anasema na kuongeza kuwa;

“Jiko la kupikia wachezaji mwanzoni lilinisumbua na hiyo ni kutokana na mapishi ambayo nilikuwa nikiyafanya zaidi ya hotelini yanayojaa viungo vingi sana.”


KUFIKA

SIMBA

Anasema wakati anafanya kazi kwenye meli, walikuwa wanakuja Bandari ya Dar es Salaam mara kwa mara na ndipo alipokutana na aliyekuwa kiongozi wa timu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.

“Nilikutana na kina Kaburu na Mohamed Nassor, waliona nina mapenzi na Simba wakaona ni mtu ambaye ninawafaa sana, nilikuja hapa nilimkuta mpishi ambaye alikuwa anapika ilimradi tu anapika.

“Wakati huo walikuwa hawaelewi mchezaji anatakiwa kula nini na kwa wakati gani, sasa walitaka kuingia katika mapinduzi, kutoka kula kiholela mpaka kula kisasa,”

Anasema baada ya kuingia alikuja na vitu vipya kama tambi, makaroni, vitu vingi ambavyo wachezaji wanatakiwa kula kwa ajili ya kujenga mwili.

Anasema wakati ameingia kulikuwa na Simba fulani hivi ya akina Haruna Moshi ‘Boban’, Amri Kiemba ambayo mchezaji anaamua kula anachojisikia na sio kupangiwa kula nini.

“Tulikutana na ugumu huo wa kuanza kuelekeza mchezaji anatakiwa kula hivi na kutokula hiki kwa kushirikiana na daktari.

“Ulaji unakuwa ni tofauti, kuna mchezaji unakuta ana mwili mkubwa hawezi kula chakula sawa na mwenye mwili mdogo, kunakuwapo na utofauti mkubwa katika hilo,” anasema.


KWA NINI SIMBA?

Anasema mbali ya kuwa mpishi lakini ni shabiki wa timu hiyo na alianza kuipenda kutoka ndani ya familia yake yenye maskani Kimara ambayo huiambii kitu juu ya hilo.

“Pale Kimara enzi za kina Mwameja ilikuwa kupata jezi tu ni mtihani mkubwa sana, kupata tu bendera ilikuwa ni kazi kweli kweli.

“Upande wa Kimara tulikuwa watu watatu tu ikiwepo nyumba yetu tulikuwa na bendera sasa ili kuifanya isipotee wala kuibwa tulipanda juu ya mnazi na kuitundika juu, walikuwa wanajua bendera iko kwao Sam tu.”


CHANGAMOTO JIKONI

Pale Simba anapikia zaidi ya watu 40 ambao wanakula na kusaza. Kwa upande wake anasema uzoefu ndio silaha kubwa sambamba na kujiamini.

“Ukiwa mpishi unahitajika kuwa na kasi, umakini na usafi wa hali ya juu, maana chakula ni kitu cha kukifanya kwa uangalifu mkubwa sana,” anasisitiza.


VIFAA VYA JIKONI

Anasema, hajawahi kupata wakati mgumu katika kuandaa chakula kwani kila siku wananunua vyakula vipya na freshi kabisa.

“Kila siku kuna bajeti ya kula vitu freshi mfano nyama kila siku lazima ifuatwe buchani, tofauti ya baadhi ya timu zinazokula kwenye mahoteli vyakula vinakaa wiki mbili.

“Simba wanakula vitu freshi hata mboga za majani zinatoka shambani siku hiyo hiyo na kupikwa, vinanifanya hata mpikaji kuwa na kazi ndogo kupika,” anasema.


MAISHA YAKE SIMBA

“Kambini ndio asilimia kubwa ya maisha yangu yapo hapa, nakaa hapa sana, kwetu Morogoro naenda mara moja moja lakini maisha yangu ni hapa hapa.”

Anasema, wakisafiri inawalazimu kwenda na vyakula vyao kwani wakati mwingine wanakoenda hakuna au ni vigumu kupata kiurahisi vitu ambavyo wanahitaji.

“Tunaposafiri nje ya nchi, tunalazimika kwenda na vyakula vyetu mfano mchele, nje wanatumia mchele kama pisholi, mchele mwingine ni kama plastiki, lakini wao ndio mchele waliouzoea tofauti na sisi.

“Tunabeba mchele, maharage na hata unga, vya nje vinakuwa tofauti kwa ubora, unaweza kununua unga aisee ukashangaa umejaa chenga lakini ndio unga wao na wameuzoea na hapo wanauita namba moja,” anasema.


KURUBUNIWA

Mara nyingi soka la Afrika limejaa fitina za hapa na pale ambazo hulazimika wapinzani kuingilia mpaka chakula na hata sehemu za kulala wapinzani.

Sam anasema, katika maisha yake hajawahi kukumbana na kishawishi cha namna hiyo ili aihujumu timu na ikitokea ikawa hivyo atakabiliana nacho.

“Haijawahi kutokea, yaani kwanza naipenda sana timu yangu, halafu tukiwa nje ni ngumu, nakuwa jikoni muda wote, ila balozi katika nchi husika hutusaidia kutupa watu wawili ambao nasaidiana nao,” anasema.

“Jikoni napewa nafasi kidogo sana hivyo kama mpishi macho yangu muda wote yanakuwa jikoni sitoki, hata wapinzani wametuona kuwa tuko makini sana, Simba wamejipanga sana kusema kweli hawataki utani,” anasema.


MAISHA YAKE NA WACHEZAJI

“Wachezaji wamenizoea sana wananiita Bro Sam wananiheshimu sana, sibagui wala kumpendelea mchezaji kwa kuwa ni staa au vipi hapana, kila mchezaji kwangu ni sawa na mwenzake,” anasema na kuongeza utaratibu huo ndio unamfanya kuishi nao vizuri na karibu.

Anasema Simba ya sasa iko juu zaidi ya awali na hiyo inachagizwa na namna ambavyo viongozi wanajitolea pesa kuifanya timu hiyo kupiga hatua zaidi,

“Simba iko mbali sana sana, sijaona timu ya kuifananisha. Wanamsema bosi sijui nini, wakati mtu anajitolea pesa zake ambazo hajui hata kama zitarudi, kuendesha timu hii ni gharama asikwambie mtu, anapotokea mwanachama eti tupeni timu yetu huwa nashangaa sana, wakati hachangii kitu na hata kadi kulipia hana,” anasema


AMPA TANO

BARBARA

Sam anampongeza mwanadada Barbara Gonzalez ambaye ni Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo kwa namna ambavyo anapambana wawapo ndani na hata nje ya nchi ili kuhakikisha Simba inapata matokeo.

“Unajua Barbara mnasafiri usiku mko naye, mnaenda uwanja wa ndege unakuta kuripoti saa sita kuondoka saa nane, huyo dada tunakuwa naye bega kwa bega, lakini mtu ambaye hajui anachukulia poa aisee inaumiza sana.

“Huyu dada anapambana bwana, anaipenda Simba na ndio maana muda mwingi anapambana kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.”


MAFANIKIO

“Siwezi kusema yote lakini Sam ni mtu ana maisha yake hivi mazuri na tofauti na watu walivyomtegemea hapo awali, hata mwanangu akitaka kuwa kama mimi sawa tu.

“Upishi unalipa, wenzetu nje wanalipwa vizuri sana, tofauti na hapa ambapo hata hoteli hazilipi vizuri wapishi, unakuta anaingiza zaidi ya Sh 150 milioni halafu analipwa Sh 600,000 hadi 800,000,”

“Ndio maana sitaki kusikia habari za kurudi kwenye mahoteli wanatunyonya sana, hakuna haki, unakuta mtu anaingia asubuhi mpaka jioni, havilingani na kile anachokiingiza, hata wahudumu pia anasimama asubuhi mpaka jioni analipwa Sh.150,000 tofauti na Kenya,” anasema Sam.

KUIKACHA SANAA

Sam alisomea sanaa ya uigizaji na uandishi script za filamu, akaigiza pamoja na kina Nyamayao, na pia akarekodi albamu yake ya ‘Kifo cha Mama’ lakini kote hakufanikiwa kama kwenye upishi.