Prime
HISIA ZANGU: Vikapu vya noti kwa wachezaji toka kwa mashabiki vinafikirisha

Muktasari:
- Nimeona kwa Khalid Aucho, nimeona kwa Aziz Ki, majuzi nimeiona tena kwa Ladack Chasambi. Imeanza kuwa kitu cha kawaida kabisa. Mchezaji anayeonekana kucheza vyema zaidi ya wenzake anazawadiwa pesa na mashabiki.
NINAPOTAZAMA kikapu kikitembezwa kwenye Uwanja wa KMC kwa ajili ya kuwazawadia pesa wachezaji wetu mastaa huwa natabasamu. Nakumbuka namna ambavyo mpira wetu umepita katika milima na mabonde.
Nimeona kwa Khalid Aucho, nimeona kwa Aziz Ki, majuzi nimeiona tena kwa Ladack Chasambi. Imeanza kuwa kitu cha kawaida kabisa. Mchezaji anayeonekana kucheza vyema zaidi ya wenzake anazawadiwa pesa na mashabiki.
Sikia hii. Zamani mpira wetu ulikuwa unachezwa na maskini halafu unatazamwa na matajiri. Ilikuwa inanishangaza. Ilikuwa inaonekana kama vile mashabiki walikuwa wana vipato vikubwa kuliko wachezaji wanaocheza ndani ya uwanja.
Ndio, kazi ya wachezaji wa zamani ilikuwa kufikiria namna ya kuomba pesa kwa mashabiki pindi mpira unapoisha. Mchezaji anacheza, huku akiwaza kwamba jukwaa kubwa kuna mashabiki wawili watatu ambao anaweza kuwaomba hela ya kodi.

Wachezaji walikuwa maskini. Shabiki anayefanya kazi Mamlaka ya Bandari ni wazi alikuwa na pesa kuliko Edibily Lunyamila. Wachezaji walikuwa wanategemea zaidi mapato ya mlangoni kwa ajili ya vipato vyao.
Bahati mbaya zaidi ni kwamba mapato ya mlangoni pia yalitegemea na matokeo ya uwanjani. Mkifungwa mnaondoka na asilimia 20, mkitoka sare mnaondoka na asilimia 50 wakati mkishinda mnaondoka na asilimia 80. Maisha yalikuwa magumu kwa wachezaji.
Wachezaji baada ya mechi wangeweza kuoga na kisha kuanza kutangatanga kwa mashabiki wenye uchumi mzuri kwa ajili ya kuwapelekea matatizo. Kuna wakati hata wachezaji walipoumia uwanjani walikuwa wanachangiwa na mashabiki kwa ajili ya matibabu.
Nakumbuka tukio la beki nyota wa zamani wa Yanga, Fred Felix ‘Minziro’ ambaye alipigwa kiwiko na kiungo wa Simba, Hussein Marsha na kung’oka jino lake. Alichangiwa Sh6,000 na mkutano mkuu wa Yanga akapelekewa nyumbani. Wakati huo zilikuwa pesa nyingi. Miaka imekwenda na maisha leo yamebadilika. Nadhani leo wachezaji wengi ni matajiri kuliko mashabiki. Wachezaji wa leo wana mikataba mizuri. Wachezaji wa leo wa Simba na Yanga wengi mishahara yao inaanzia Sh7 milioni na kuendelea. Wachezaji wa leo wanatembelea magari mazuri na wamejenga nyumba nzuri.

Wachezaji wa leo wanapata pesa nyingi za ‘signing fee’. Achana na wachezaji wa kigeni, kuna mchezaji wa kizawa wanapewa Sh200 milioni kwa ajili ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili. Ni kiasi kikubwa cha pesa. Viongozi wa kileo pia wametanua wigo wa kupata pesa katika klabu kupitia mikataba minono ya udhamini kutoka katika vyanzo mbalimbali. Lakini wanapata pesa nyingi kutoka CAF ambako wamekuwa wakishiriki vyema mara kwa mara katika michuano yao mikubwa.
Leo wachezaji ni matajiri na mashabiki walio wengi ndio ambao wamekuwa maskini. Kibao kimegeuka. Lakini hapo hapo mchezaji anapotimiza vyema matakwa ya kazi yake bado mashabiki maskini wanajichanga kumpa pesa mchezaji.
Mchezaji anayelipwa kiasi cha Sh17 milioni kwa mwezi anapewa pesa na shabiki ambaye kipato cha genge lake kwa mwezi ni Sh 200,000. Haya ni mapenzi yaliyopitiliza na hii nadhani huwa inatokea Tanzania tu.

Sina cha kuzuia au kupinga katika hili lakini inanifikirisha sana. Huu utamaduni ukichunguza sana unatafakarisha. Inanikumbusha siku moja nilimwalika staa wa zamani, Tottenham Hotspurs, Victor Wanyama kuja nchini na akashangaa namna ambavyo mashabiki wengi wa Tanzania walikuwa bize kumuomba kupiga naye picha kuliko kumuomba hela.
Nairobi, Wanyama akionekana tafsiri yake ni kwamba mtu mwenye pesa ameonekana. Wale jamaa ni mabepari na wanajua thamani ya mtu mwenye pesa. Kwao mtu mwenye pesa huwa anaombwa pesa na sio kupewa pesa. Sisi huku ni tofauti.
Nadhani anaweza kuja Cristiano Ronaldo katika pambano la hisani pale Uwanja wa Mkapa na bado tukamchangia pesa kuliko kumuomba pesa. Mashabiki wa Tanzania wanapaswa kuingia katika kitabu cha rekodi ya maajabu ‘Guiness book of records.’.
Nadhani wachezaji pia wajitafakari kwa mapenzi makubwa wanayopewa na mashabiki. Kwa sasa wao ni matajiri na nadhani wanapaswa kuanza kufanya jambo kwa mashabiki pia. Klabu zao, hasa Yanga zimekuwa zikifanya jambo la hisani kwa makundi maalumu wanapokaribia kucheza mechi kubwa. Wachezaji nao sasa hivi waanzishe mifuko yao ya kimyakimya kwa ajili ya kusapoti mashabiki. Kwa mfano ni wale mashabiki ambao wamekuwa wakisafiri kila pembe ya nchi hii kwa ajili ya kwenda kutazama mechi zao.

Kuna matawi ambayo yamekuwa yakijichanganya kila kukicha na kusafiri umbali mrefu katika safari za hatari kwa ajili ya kwenda kutazama mechi za Simba na Yanga. Wachezaji wenye busara pia wanapaswa kuchangia kitu katika safari hizi.
Kule Ulaya nimewahi kushuhudia mara kadhaa wachezaji wakiwarudishia pesa mashabiki waliosafiri katika mechi ya ugenini na kisha timu kuambulia matokeo mabaya. Wanawarudishia pesa za tiketi zao.
Aprili 2023 wachezaji wa Tottenham Hotspur waliwarudishia pesa za tiketi na safari mashabiki waliosafiri kwenda Newcastle baada ya timu yao kuambulia kichapo cha mabao 6-1 kutoka kwa Newcastle United.
Huu ndio ustaarabu wa wachezaji matajiri wa klabu za wenzetu. Wakati huu tukiwachangia wachezaji wetu nao wanapaswa kutukumbuka. Wana vipato vikubwa. Wanapaswa pia kurudisha hisani. Wasisubiri sana viongozi wao wafanye hisani, hapana, na wao wanapaswa kufanya jambo la maana.