HISIA ZANGU: Simu ya Shearer kwa Rashford ni ujinga tu

MTU mmoja anabeba gunia mbili za viazi katika mgongo wake. Anatembea kilomita moja kwenda kuvihifadhi. Analipwa shilingi elfu tano tu. Mwingine pale Australia anazama katika machimbo ya madini na kukaa chini kwa wiki kadhaa. Akisaka noti chache tu za kumfanya aishi.

Na wakati huohuo Alan Shearer anampigia simu Marcus Rashford kwa ajili ya kumpa msaada wa kiakili ili arudi katika fomu yake uwanjani. Rashford analipwa Pauni 200,000 kwa wiki. Anabembelezwa na kuelekezwa namna ya kurudi fomu. Waingereza wanashangaa kwanini hayupo fomu. Nimesoma hii habari majuzi nikacheka kidogo. Nikasoma mahala pengine kwamba hata staa wa zamani wa Manchester United, Paul Ince amempigia simu Rashford na kumfariji huku akisisitiza kwamba Rashford lazima asaidiwe. Lakini pia akasisitiza kwamba Rashford lazima aendelee kupangwa.

Hawa ndio Waingereza. Wapo katika ubora wao. Kuna mambo kama matatu hivi. Jambo la kwanza, kama ingekuwa inatokea kwa mchezaji mwingine ambaye sio Muingereza na yupo katika timu kubwa jina ambalo lingetumika hapo ni ‘flop’.

Kama angekuwa ni mchezaji kutoka Afrika au Amerika Kusini hawa akina Shearer ambao ni wachambuzi, pamoja na waandishi wa habari wa Uingereza haraka haraka wangemuita mchezaji flop. Lakini kwa sababu ni Rashford basi anabembelezwa.

Hawaongei umuhimu wa United kuanza kusaka washambuliaji wengine. Wanataka United imsubiri Rashford mpaka awe fomu. Kama ingekuwa ni kwa Carlos Tevez wangeanzisha uvumi wa kuondoka kwake Old Trafford. Wangemuita Flop. Lakini pia wangeandika umuhimu wa Manchester United kusaka mshambuliaji mwingine.

Hii ndio dunia ya Waingereza. Wao kwa wao wanabembelezana. Rashford analipwa mamilioni ya pesa kwa wiki ambayo wanadamu wengine tunahisi kwamba tunaweza kufa kabla hatujazigusa, achilia mbali kuzimiliki. Wao wanambembeleza acheze.

Wanatafuta sababu ya kutocheza kwake vizuri badala ya kusonga mbele na kuishauri United isake mshambuliaji mpya. klabu kubwa kama hii inamsubiri Rashford arudi katika fomu. Katika mechi 11 zilizopita hajafunga bao. Na katika mechi hizo, mechi nane benchi limemuita.

Zamani Sir Alex Ferguson pamoja na Uingereza wake lakini alikuwa hana uvumilivu na mambo haya. Kwake Nyekundu ilikuwa Nyekundu na kijani ilikuwa kijani. Alikuwa mkali kweli kweli na kuna kitu alikuwa anawafanyia wachezaji kinaitwa Hairdryer treatment.

United wanahitaji watu wa maana kwa sasa Liverpool na Manchester City wapo mbali yao. Chelsea inawapita na Arsenal inaonekana kusogea mbali zaidi katika mchakato wao wa kuwa timu bora. Kila siku wanaimarika. United wao wamebaki katika kubembelezana.

Ni haya haya ambayo Cristiano Ronaldo alikuwa ameyasema siku tatu zilizopita. Ronaldo amefungua moyo na kudai kwamba wachezaji wengi vijana wa Manchester United hawashauriki. Hawafanyi sana mazoezi lakini pia wanajiona wanajua na hawataki kumsikiliza mtu.

Nadhani Ronaldo alikuwa anawalenga hawa hawa akina Rashford. Hata kama tunaweza kudai kwamba Ronaldo ni tatizo lakini kumbe tayari ameshaliona tatizo. Watoto wa siku wamekuwa laini. Ndio hawa ambao wanapigiwa simu na akina Shearer kwa ajili ya kubembelezwa na kuliwazwa.

Haya yanatokea wakati Pep Guardiola na Manchester City yake hawana muda huo. Siku akikosekana Kelvin de Bruyne basi Ilkay Gundogan au Phil Foden atakuwa nyota wa mchezo. Wameitengeneza timu yao katika namna hii. Ince anataka Rashford aendelee tu kupangwa. Ndiyo, anaweza kuendelea kupangwa kwa sababu labda yupo United. Angekuwa yupo City asingeendelea kupangwa.

Raheem Sterling alianza msimu ovyo huku akiwa na manung’uniko kibao. Wenzake wakaendelea kupiga kazi huku yeye akisugua benchi. Baadaye fahamu zikamrudia akajituma na sasa amerudisha nafasi yake.

Hii ndio faida ya kuwa na makocha kama kina Pep. Lakini pia ndio faida ya kucheza timu kama Manchester City ambayo Waingereza hawaioni kuwa fahari yao kuzidi Manchester United.

Lakini kama nilivyosema hapo awali. Hawa watoto wa Kiingereza wana mioyo milaini ingawa wana matumizi makubwa ya nguvu uwanjani. Inatokana pia na asili zao. inatokana na makuzi yao pia. Jinsi ambavyo wamelelewa ni tofauti na watoto wa Afrika au Amerika Kusini. Hawa watoto wa Afrika au Amerika Kusini maisha yao ya utotoni yamewafundisha upiganaji. Sijui kama wanafahamu sana mambo ya saikolojia na kubembelezwa kama huku kwa kupigiana simu kurudishwa moyo wako wa kupambana.

Hawa kina Samuel Eto’o wametoka katika umaskini. Soka ndio ilikuwa njia pekee ya kutoka katika umaskini uliotopea. Carlos Tevez anadai kwamba bila ya soka angeweza kuwa jambazi. Haishangazi kuona wana mapambano. Lakini pia nafasi zao ni rahisi kutafutwa mtu mwingine kama akizubaa.

Hawa akina Rashford wametoka katika familia ambazo zina mkate wenye siagi. Haishangazi kuona mioyo yao inakuwa laini. Ni tofauti na Ronaldo de Lima ambaye mama yake alikuwa mhudumu wa Baa na alilazimika kucheza soka ili mama asiendelee na kazi hiyo. Kila unapokumbuka mateso ya utotoni unapiga moyo konde na hautaki familia irudi ilikotoka.

United wanabembelezana na Rashford. Analipwa Pauni 200,000 na haionekani kama nafasi yake ipo hatarini mwishoni mwa msimu. Haya ndio maisha ambayo pia yatairudisha Manchester United nyuma. Maisha ya kukariri.

Sioni kama Ronaldo ataendelea kuchezea United msimu ujao. Nadhani tutasikia kitu.

Sawa, hata yeye mwenyewe ni tatizo kwa sababu umri unamtupa mkono na soka la kisasa linahitaji mambo mengi ikiwemo ukabaji wa pamoja. Lakini hapana shaka amegundua kitu muhimu kwa vijana walio chini yake kwa sasa hapo Old Trafford.

Roy Keane pia amekuwa akizungumza mara nyingi kuhusu vijana wa kisasa kuwa laini.

Mchezaji anaweza kupoteza simu yake akajikuta ana mawazo mengi kiasi cha kushindwa kucheza soka wakati mchezaji mwenyewe analipwa pauni 200,000.

Zama zimepita zamani ambapo tumewapoteza watu kama Keane mwenyewe, Patrick Vieira, Antonio Conte, Jens Jeremies na wengineo. Wamebakia watoto laini kama hawa akina Rashford ambao wanataka kupigiwa simu wabembelezwe.

Kwangu mimi simu ya Shearer kwa Rashford inabakia kuwa ujinga mwingine tu ambao hauna maana yeyote. Kuna mamilioni ya vijana kando ya dunia wanahitaji simu hizi. Wanajiua kwa ukosefu wa kazi au ugumu wa kazi zilizopo.