Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Mnyama alianza kama swala akamalizia kama Simba

Muktasari:

  • Al Ahli Tripoli walikuja katika ardhi ya Tanzania kama timu tishio kutoka Afrika Kaskazini. Ilionekana dhahiri kwamba siku moja kabla ya mechi hii pale Unguja watani wangembamiza mabao ya kutosha rafiki yetu kutoka Ethiopia, CBE.

NA walimaliza kazi huku kila mtu akibaki na mdomo wazi. Kama ilivyo kawaida yao. Simba. Uwanja wa Mkapa ni wao. Ni katika mechi za kimataifa. Zipo jioni chache ambazo waliwahi kukosea, lakini hii ilikuwa miongoni mwa siku ambayo hawakupaswa kukosea.

Al Ahli Tripoli walikuja katika ardhi ya Tanzania kama timu tishio kutoka Afrika Kaskazini. Ilionekana dhahiri kwamba siku moja kabla ya mechi hii pale Unguja watani wangembamiza mabao ya kutosha rafiki yetu kutoka Ethiopia, CBE.

Ni kweli walifanya hivyo na deni likabaki kwa mtani ambaye dalili zake hazikuwa nzuri. Kikosi chake bado hakijaungana vyema, lakini pia pambano la kwanza halikutoa dalili nzuri kwa Mnyama pale Tripoli. Alitumia muda mwingi kukaba na kuzima mbinu za wenyeji kuliko kufanya mambo yake binafsi.

Na katika pambano hili la Temeke dalili pia zilikuwa mbaya baada ya Paciencia Mabululu, mshambuliaji hatari kutoka Angola kufunga bao la kuongoza kufuatia kujichanganya kwa walinzi wa Simba katika eneo lao. Kipa wao, Moussa Camara hakuwa na la kufanya.

Kufikia hapo hakukuwa tena na mikwaju ya matuta. Kwa mpira wa Kiafrika ulivyoendelea na sheria zake zilezile, tayari Al Ahli Tripoli walikuwa wanasaka sare na Simba walikuwa wanasaka ushindi wa aina yoyote ile. Simba walikabiliwa na mtihani mzito zaidi.

Ghafla yakaja mabao mawili ya maajabu. La kwanza lilifungwa na Kibu Dennis. Mpira wake aliopiga kwa sarakasi haukuonekana kuwa na nguvu, lakini ulimkuta kipa wa Al Ahli Tripoli akiwa hajielewi. Jua lilimzingua au hesabu zake ziliamini kwamba mpira ungetoka nje. Lilikuwa bao la ajabu kidogo.

Halafu likaja bao jingine kutoka kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, Leonel Ateba. Kiungo mmoja wa Al Ahli Tripoli aliuchezea mpira kama masikhara na kujikuta akimpasia Ateba. Unaweza kusifu utulivu wake na namna alivyomtungua kipa wa Al Ahli Tripoli.

Kuna washambuliaji ambao wanapasiwa mpira na kushikwa na kigugumizi kwa sababu hawategemei hali hiyo. Ateba aliutendea haki mpira huo.

Kufikia hapo Simba walikuwa wamepita. Walihitaji kuweka saruji zaidi katika ushindi wao na ilipatikana nafasi nyingine tena ambapo Jean Charles Ahoua alionekana hajaotea kulekelea katika lango la Al Ahli Tripoli. Alimpasia Ateba akafunga, lakini kumbe kabla ya hapo mwamuzi alikuwa ameshapuliza filimbi.

Baadaye ikachezwa rafu mbaya kwa Deborah Fernandes Mavumba. Ingeweza kumvunja mguu. Kinachoshangaza ni kwamba mwamuzi hakutoa kadi yoyote ile, lakini aliweka faulo. Ina maana aliona. Waamuzi kutoka Afrika ni tatizo. Ndiyo maana kwa wenzetu katika hatua zote huwa wanatumia VAR.

Baadaye akaingia kijana anayeitwa Edwin Balua. Ana kipaji kikubwa, lakini bado hajajipata. Leo anaweza kucheza hivi na kesho anaweza kucheza vile. Katika siku yake atakupigia mipira mizuri ya faulo pamoja na kumkimbiza adui. Katika siku nyingine ataonyesha ukosefu wake wa uzoefu.

Mechi hii ilikuwa jioni nyingine nzuri kwake akitokea katika benchi. Alifunga bao ambalo Simba walilihitaji kuthibitisha kutinga makundi. Bao la tatu. Kumbuka kwamba sekunde chache zilizopita Simba walikuwa wamekoswa na Mabululu. Shukrani kwa Camara.

Al Ahli Tripoli walikuwa wamejaa katika lango la Simba wakisaka bao la kusawazisha ili wao wawe katika nafasi nzuri ya kupita. Simba walihitaji shambulizi moja tu la kushtukiza kwa ajili ya kuiua mechi. Balua aliifanya kazi hii kwa ufasaha.

Namna ambavyo alikokota mpira kwa umbali mrefu. Namna ambavyo aliamua kuwa mchoyo kwa wenzake wawili kando yake, lakini bado akachukua uamuzi sahihi wa kupiga shuti kali lililompita kipa. Balua alimalizia jioni njema kwa Simba.

Baada ya kila kitu unajaribu kutazama mambo kwa upana wake. Simba wanahitaji kuendelea kusuka kikosi chao. Kocha Fadlu Davis bado ana kazi kubwa ya kufanya. Tatizo kubwa lililopo ni kwamba lazima ataingia katika mlinganisho (comparison) na watani zake Yanga.

Wakati mwingine mlinganisho huu hauji kwa watani tu, bali unarudi nyuma wakati ule Simba ikiwa moto chini ya Clatous  Chama, Luis Miquissone, Larry Bwalya na wengineo. Bado Simba inahitaji umiliki mkubwa wa mpira. Inahitaji pasi za kuonana na uwezo mzuri wa wachezaji binafsi. Kuna kiwango bado hakijafikiwa, lakini mwelekeo ni mzuri.

Wachezaji kama Joshua Mutale, Ateba, Kibu hawatazamani kwa haraka. Ni tofauti na ilivyokuwa zamani. Hasa huyu Mutale anahitaji kutuliza kichwa chake. Anaonekana kuwa machachari zaidi, lakini siyo hatari.

Kasi yake haiwasadii Simba. Wakati mwingine anakimbia na mpira anauacha nyuma. Lazima ajitazame upya. Simba inahitaji ubora zaidi ya ule alionao. Lakini kwa vile bado Simba yenyewe inajitafuta, basi anaweza kuisaidia kwa sasa.

Kipa Camara lazima apewe maua yake. Unaanza kuwaza nafasi ya Aishi Manula mpaka sasa. Camara anastahili kukaa langoni mpaka atakapopoteza nuru aliyonayo kwa sasa. Ukweli ni kwamba kwa sasa anang’ara. Bila yeye Simba wangekuwa wametolewa hatua hii. Alifanya kazi nzuri Tripoli na akaja kumalizia kazi nzuri Temeke.

Tuendelee kuisikilizia Simba ya misimu miwili mbele ambayo msingi wake umeanza kujengwa tena leo. Wachezaji wamejikuta katika wakati mgumu kwa sababu asilimia 60 ya wachezaji ni igizo jipya klabuni. Mechi za makundi na michuano ya Ligi Kuu zitawaimarisha zaidi klabuni na kujenga msingi mmoja.