Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Kwaheri Heritier Makambo, safari hii haikuwa riziki

HATIMAYE Yanga wameachana na mshambuliaji waliyempenda, Heritier Ma Olongi Makambo. Waliwahi kumpenda sana. Mzee wa kuwajaza. Alirudi kwa shangwe kubwa klabuni hapo takribani miezi 18 iliyopita. Safari hii haikuwa riziki yake.
Alikuja mara ya kwanza klabuni hapo kiajabuajabu tu. Nadhani aliletwa na aliyekuwa na kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye ni raia mwenzake wa DR Congo. Hatukujua uwezo wake. Lakini ghafla akaibuka bonge la staa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga.
Alisaidiwa zaidi na Ibrahim Ajibu Migomba pamoja na Fei Toto. Tatizo lao kubwa walicheza katika Yanga ambayo ilikuwa na njaa. Hata hivyo alifanikiwa kutengeneza jina kubwa na aliondoka nchini akiwa mtu tofauti na yule aliyekuja.
Alienda zake Horoya ya Guinea na habari zake zikasahaulika nchini. Baadaye Yanga ikapata tajiri mwenye fedha zake akaanza kuiunda Yanga mpya. walikuja washambuliaji kama David Molinga, Yikpe na Michael Sarpong lakini hakuna ambaye alimfikia Makambo kwa uwezo.
Ghafla Yanga wakataka kujiimarisha zaidi wakaamua kumrejesha nchini Makambo. Aliwasili uwanja wa ndege kwa shangwe kubwa. Lakini ujio wake uliambatana na mshambuliaji mwingine wa Congo, Fiston Mayele ingawa kila mtu alikuwa ametoka katika njia yake. Mayele aliwasili kutoka Congo wakati Makambo aliwasili kutoka Afrika Magharibi.
Mayele aliwasili kinyonge na kimya kimya. Mashabiki wengi wa Yanga waliweka matumaini yao kwa Makambo. Kwa Yanga iliyokuwa inaundwa na mastaa wapya akina Khalid Aucho, Yannick Bangala, Djuma Shaaban, Jesus Moloko, Farid Mussa na wengineo, ilikuwa inaonekana kama vile Makambo angeng’ara zaidi.
Ilionekana kama Makambo aling’ara zaidi akiwa na akina Ajibu vipi kwa Yanga hii? Na alipofunga bao zuri katika pambano la wiki ya Wananchi dhidi ya Vipers ilionekana kama vile Makambo angekuwa na mwendelezo bora kwa kipindi kingine cha pili cha maisha yake Yanga.
Hata hivyo ghafla Yanga walijikuta wakiangukia kwa Mayele. Kuanzia pale alipofunga bao pekee la ushindi dhidi ya watani wao Simba pambano la ngao ya Jamii, Mayele hakurudi nyuma. Ghafla staili ya kuwajaza ya Makambo ikazimwa na staili ya kutetema ya Mayele.
Na leo Makambo anaondoka Yanga huku wakiwa hawashtuki. Wana uhakika na Mayele. Ameshawafanyia mambo makubwa ndani ya kipindi kifupi alichokuwa na Yanga. Swali la msingi ni, Makambo amepatwa na nini?
Kuna mambo mengi. Nasikia kwamba tangu akiwa na Horoya katika msimu wake wa pili Makambo alikuwa hapati nafasi kabisa. Labda alikuja Yanga huku akitoka katika mahala ambapo benchi lilimuathiri. Yanga hawakutambua hili.
Lakini pia alipofika Mayele alianza kung’ara moja kwa moja na kocha Mohamed Nabi alimuamini Mayele moja kwa moja katika kikosi cha kwanza. Kuna jambo ambalo niliamini kwamba kocha Nabi alikuwa anakosea. Alikuwa anampa Makambo dakika chache zaidi. Hata hivyo naambiwa kwamba hata mazoezini Makambo alikuwa haonyeshi makali yake.
Kitu ambacho kilimpoteza zaidi Makambo ni uwepo wa Mayele. Kuna baadhi ya wachezaji huwa wanatimiza majukumu yao zaidi wakiwa katika presha. Pindi Mayele alipokuwa chaguo la kwanza Makambo hakucheza Yanga katika presha.
Kuna wachezaji ambao upinzani huwa unawaongezea makali na kuna wachezaji wa aina kama ya Makambo. Kama angekuwa peke yake angejua kwamba muda wote mashabiki wa Yanga wanasubiri mabao kutoka kwake. Angejikuta katika presha kubwa ya kufanya vizuri kila mechi.
Lakini hapo hapo kama yeye angekuwa mshambuliaji namba moja katika timu ni wazi kwamba Nabi angelazimika kumpanga mara kwa mara kitu ambacho kingerudisha uwezo wake wa kujiamini. Badala yake benchi alilotoka nalo Horoya likaendelea kumuathiri katika kikosi cha Yanga.
Naamini kama Makambo angekuwa chaguo la kwanza halafu Clement Mzize angekuwa chaguo la pili basi angeelewa mzigo mkubwa ambao unamuelea katika mikono yake. Alipojikuta akiwa katika chaguo la pili hakuwa na presha kubwa.
Na Ndio maana kwa sasa Mayele ana presha kubwa katika nafasi yake kwa sababu anajua wajibu wake wa kufunga. Kwanza anajua anaibeba timu yake lakini hapo hapo anatambua kwamba ana mbio zake binafsi na wafungaji wengine katika kuwania kiatu cha dhahabu.
Bado naamini kwamba kama Makambo akipata nafasi ya kucheza katika timu nyingine za kawaida za Ligi Kuu kama Coastal Union, Kagera Sugar au Mtibwa bado anaweza kuwasaidia kuliko washambuliaji wa timu hizo wanachofanya.
Kikubwa kingine kilichomuondoa Yanga ni ukweli kwamba achilia mbali walikuwa hawamtegemei lakini pia kwa sasa wana pesa. Sifa za timu kubwa ni kutokuwa na uvumilivu na viwango vya chini vya wachezaji. wana pesa, kwanini wakusubiri urudi katika fomu kama inachelewa? Wanaondoa mtu na wanaweka mtu mwingine.
Makambo alichelewa sana kurudisha fomu yake akiwa na Yanga. Najua kwamba Yanga walitamani kuachana naye hata mwishoni mwa msimu uliopita lakini walikuwa hawana jinsi. Ni hatari kucheza katika timu kubwa huku kiwango chako kikiwa chini kwa muda mrefu. Zaidi ya yote ni kwamba kuna mwenzako anafanya vema katika nafasi hiyo.
Na sasa tunamkaribisha rasmi Kenneth Musonda. Staa wa Zambia. Huyu tusubiri kumuona kwanza lakini hapana shaka kwamba amekuja klabuni kwa ajili ya kumsaidia Mayele kufunga mabao. Inavyoonekana Yanga hawamuamini sana kinda wao, Clement Mzize na wanaona hayupo tayari kwa ajili ya kucheza mechi ngumu za kimataifa kama Mayele akiumia. Nafasi hiyo imekwenda kwa Musonda.