Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Ateba na Mnyama walijikuta wapo 'nyumbani' wakiwa ugenini

HISIA Pict

Muktasari:

  • Sisi wote ni Simba na Yanga. Nchi imegawanyika katika pande mbili. Matokeo yake ni kwamba hata kama hizi timu hazina vikosi vizuri, lakini zinachukua ubingwa au kushika nafasi ya pili.

LEONEL Ateba alifunga mabao mawili wakati Simba ilipokuwa katika uwanja wa 'nyumbani' pale Tabora kukabiliana na Tabora United. Simba na Yanga ni klabu za ajabu kuwahi kutokea duniani. Hauwezi kupata timu kama hizi katika kona yoyote ya dunia.

Kuelekea katika pambano hili hii mechi ilipigiwa chapuo na kelele nyingi. Zaidi ni kwa sababu pambano lenyewe lilikuwa linachezwa Tabora. Unatazamia pambano litakuwa gumu kwa Simba ndani na nje ya uwanja. Kumbe hapana. Ndani ya uwanja kuna ugumu, lakini nje ya uwanja kulikuwa na wepesi mwingi. Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulikuwa umejaza mashabiki wa Simba tu.

Sisi ambao tulikuwa nyumbani tukifuatilia kwa karibu pambano hili tulichoona ni mashabiki wengi wa Simba walioujaza uwanja wakiishangilia Simba. Naam, nchi imegawanyika katika pande mbili. Simba na Yanga, basi. Maisha yanakuwa mepesi kwa Simba na Yanga wakienda kucheza mikoani kama tulivyoona jana.

Simba haikuondoka na mashabiki Dar es salaam iliwakuta hukohuko Tabora. Wapo waliotoka mikoa jirani, wapo waliotoka wilaya za Tabora kwa ajili ya kwenda kuiona Simba na mastaa wake. Wapo mashabiki ambao kwa miaka mingi walikuwa wanaililia Tabora iwe na timu ya Ligi Kuu, lakini Simba ilipofika walihamia Simba. Yanga itakapofika watahamia Yanga.

HS 01

Duniani kote mashabiki hushabikia timu ya eneo lao. Watoto wanazaliwa wanaikuta timu ya eneo lao inashabikiwa na baba na mama. Unaweza kumkuta Mzungu -Mwingereza pale Posta Mpya ukimuuliza anashabiki timu gani anakwambia Tranmere Rovers. Ni shabiki wa damu hasa. Unamkuta Mjerumani anakuambia anashabikia St Paul.

Kama unatazamia shabiki wa Ujerumani akuambie anapenda Bayern Munich au Borussia Dortmund kwa sababu ni timu kubwa, basi unakosea. Kama unadhani shabiki wa Kiingereza atakuambia anashabikia Manchester United, Chelsea, Liverpool au Arsenal. Hapana. Kuna mashabiki kibao wa Luton. Kuna mashabiki kibao wa timu za daraja la tatu.

Hapa ndipo maisha yanakuwa magumu kwa timu kubwa zikienda kucheza na timu za kawaida katika viwanja vya ugenini. Wanalazimika kushinda mechi kutokana na ubora mwingi na sio kutegemea sapoti kutoka kwa mashabiki wa ugenini. Manchester United itasafiri mpaka London kucheza na West Ham United na mashabiki wachache wa United wanamezwa na mashabiki West Ham ambao wameanza kuishabikia timu tangu wakiwa watoto.

Juventus wakisafiri kwenda kucheza na Lecce wanalazimika kutoa machozi, jasho na damu kwa sababu wanajikuta wanachezwa katika mazingira magumu. Mashabiki wa Lecce wanajaa uwanjani. Juventus inajikuta ina mashabiki 1,000 tu waliosafiri na kumezwa na mashabiki wa Lecce. Tanzania hauwezi kukuta kitu kama hiki.

HS 05

Wakati Simba wakiwa wamejaza uwanja Tabora na Yanga wanaujaza uwanja Kaitaba, wikiendi hii Real Madrid walisafiri kwenda Barcelona kucheza na Espanyol na wakajikuta katika mazingira magumu hasa kiasi cha kunyolewa bao 1-0. Kwa wenzetu hakuna sapoti unayoipata. Kila mtu ni mfalme wa mji wake.

Sisi wote ni Simba na Yanga. Nchi imegawanyika katika pande mbili. Matokeo yake ni kwamba hata kama hizi timu hazina vikosi vizuri, lakini zinachukua ubingwa au kushika nafasi ya pili. Mfano ni pale Yanga walipoonekana kuwa wabovu chini ya kina Yikpe na David Molinga. Bado walishika nafasi ya pili mbele ya Azam ambayo haikuwa na matatizo yoyote ndani na nje ya uwanja.

Hizi timu zinapata sapoti na hazichezi katika mazingira magumu. Ni kama ulivyoiona Simba jana. Yanga nayo ikienda popote pale inajaza uwanja. Inachekesha pale nilipowaambia watu wa Azam wacheze mechi zao dhidi ya Simba na Yanga katika uwanja wa Mkapa na sio Chamazi. Pale Chamazi Azam ikicheza na Simba au Yanga inajikuta ipo ugenini na sio Chamazi.

HS 02

Kibaya zaidi ni kwamba katika uwanja kama wa Azam au KMC wachezaji wa Simba wanakuwa karibu zaidi na mashabiki wao na wanahamasishwa zaidi. Mchezaji anaweza hata kuvutwa jezi na shabiki wakati anapiga kona. Maisha yanakuwa magumu kwa wachezaji wa timu pinzani.

Nini kifanyike? Hatuna tunachoweza kufanya kwa sasa wala baadae. Maisha haya ni kama utamaduni. Tunapaswa tu kujilaumu kwamba tumeangukia katika utamaduni mbovu ambao unazikosesha timu za mikoani mapato pindi zinapocheza na timu nyingine ambazo sio Yanga wala Simba. Shabiki wa Mbeya yupo tayari akae katika televisheni kuangalia pambano la Simba na JKT Tanzania kuliko kwenda uwanjani kuitazama Mbeya City ikicheza na Azam.

Mapato ya milangoni katika mechi kama hizi za Prisons na Kagera Sugar huwa ni aibu. Simba na Yanga zilipaswa kupendwa na watu wa Dar es salaam tu, hasa maeneo ya Kariakoo. Hata hivyo zimejikuta zikipendwa nchi nzima. Zimependwa na kila mtu. Ni ngumu kwa timu za mikoani kuwa na nguvu.

HS 04

Zaidi ya hayo timu inakosa hamasa ya kimchezo na wachezaji hawajioni kama wana deni la kulipa kwa mashabiki kwa sababu muda mwingi wanakuwa wanacheza katika uwanja mtupu wa nyumbani. Mara mbili tu huwa wanajaza. Wanapocheza na Simba au Yanga. Hata hivyo wanakuja kuzomewa na sio kushangiliwa.

Mtoto mdogo wa Kagera anakijua kikosi chote cha Yanga au Simba, lakini ukimwambia ataje 'first eleven' ya Kagera Sugar anaweza akamfahamu mchezaji mmoja au wawili kwa sababu hao wachezaji waliwahi kucheza Simba na Yanga hapo zamani kabla hawajaangukia Kagera. Mtoto wa Norwich City anaifahamu timu yake tu. Hajui kuhusu Arsenal.

Kwa wenzetu kila timu ina nguvu yake. Kila timu ina mashabiki wake, kwa hiyo wana uhakika na mapato ya kiingilio hata kama wanapishana kidogo na wakubwa. Kila timu ina uhakika wa kuuza jezi zake. Kila timu ina duka lake. Hata wadhamini inakuwa rahisi kupatikana kwa sababu mdhamini anajua anadhamini timu ambayo ina mashabiki.

HS 03

Sisi nguvu kubwa imekwenda kwa Simba na Yanga kwa sababu wana mashabiki kila mahala wanapokwenda. Pesa za wadhamini nyingi zinakwenda kwao kwa sababu wana sababu ya kuthibitisha kwa wadhamini kuhusu wao kupewa pesa nyingi kuliko wengine. Huu ni ukweli mchungu.

Hata Azam wenyewe licha ya pesa zao wameshindwa kupambana na nguvu ya Simba na Yanga. Hata Prince Dube aliwahi kutuambia kuwa ndani ya Azam kuna viongozi wapo bize na Simba na Yanga. Azam hawahawa wakisafiri mikoani mechi zao zinakuwa ngumu kwa sababu hawapati mashabiki wa kuwashangilia kama ambavyo Simba wamepata Tabora jana.

Hata hivyo, pamoja na yote haya shukrani pia kwa Simba na Yanga kuziwezesha kimapato timu hizi pindi wanapokwenda mikoani. Walau Simba na Yanga wakipita katika hii mikoa huwa wanaziachia kipato hizi timu kwa staili hiihii ya mwenyeji kuchukua mapato yote. Hapa ndipo huwa tunakumbuka ule usemi wa Kiswahili. Mgeni njoo mwenyeji apone.