Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa Coastal iliyozitesa Simba, Yanga ikabeba ndoo!

MANGUSHI Pict

Muktasari:

  • Msimu wa 2015-2016 wa  Ligi Kuu Bara utabaki wa huzuni kubwa kwa mashabiki wa Tanga baada ya kushuhudia timu tatu za mkoa huo zikishuka daraja kwa mpigo, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya soka nchini  kwa mkoa mmoja kushusha timu tatu kwa mpigo.

KWA mashabiki wa soka wa Tanga, kuna misimu miwili tu ya Ligi ya soka nchini ambayo ni migumu kufutika vichwani mwao, mmoja ni ule wa mafanikio makubwa kisoka na mwingine wa huzuni ulioshuhudia mkoa huo ukishusha klabu tatu kwa mpigo kutoka Ligi Kuu Bara.

Achana na ile misimu iliyowahi kushuhudia timu za mkoa huo zikishuka daraja kwa vipindi tofauti, kwa soka kwa mkoa huo.

Msimu wa 2015-2016 wa  Ligi Kuu Bara utabaki wa huzuni kubwa kwa mashabiki wa Tanga baada ya kushuhudia timu tatu za mkoa huo zikishuka daraja kwa mpigo, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya soka nchini  kwa mkoa mmoja kushusha timu tatu kwa mpigo.

Wagosi wa Kaya, Coastal Union ilimaliza kama kibonde kwa kukusanya pointi 22 tu kupitia mechi 30, ikizibeba timu zote, juu yake ikiwa ni watani wao wa jadi African Sports iliyomaliza na pointi 26 kisha Mgambo JKT ikifuatia na pointi zao 28, zote zikishuka daraja kwa pamoja msimu huo.

Huu ndio msimu uliowakata stimu mashabiki wa soka wa Tanga, kwani hawakutarajia kutemeshwa tonge mdomoni, lakini msimamo wa Ligi wa msimu huo uliwakatili wakati Yanga ikitetea taji kwa kubeba ubingwa kwa mara ya pili mfululizo mbele ya Azam FC.

Lakini kwa upande wa furaha, msimu wa mwaka 1988 utaendelea kukumbukwa na mashabiki wa Tanga, kwani ndio ulioshuhudiwa timu mbili za mkoa huo zilibeba mataji makubwa ya Tanzania.

Ndio, katika Ligi ya Bara, Coastal Union ilibeba taji mbele ya Yanga kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwani kila moja ilimaliza na pointi 26.

Wagosi wao walifunga jumla ya mabao 26, lakini ikifungwa 18 kupitia mechi 22, ikishinda 11 na kutoka sare nne na kupoteza saba, ilihali Yanga iliyokuwa watetezi wa taji katika mechi 22 ilishinda nane, kutoka sare 10 na kupoteza nne ikifunga mabao 24 na kufungwa 16.

Ikiwa na maana kila moja ilikuwa na tofauti na mabao (GD) manane. African Sports yenyewe ilimaliza nafasi ya tatu ikikusanya pia pointi 26 kupitia mechi 22 ikishinda nane, ikitoka sare 10 na kupoteza nne kama Yanga ilia ilifunga mabao 23 na kufungwa 17.

Bingwa kwa msimu huo alisubiriwa kupitia mechi za mwisho, ambapo ilishuhudiwa Simba ikinusurika kushuka daraja kwa kuichapa Yanga kwa mabao 2-1 ikiziacha Tukuyu Stars ya Mbeya na Reli Morogoro zikienda Ligi Daraja la Pili (sasa Ligi ya Championship)

Utamu ni kwamba timu hizo tatu za juu zilikata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Muungano na Wanakimanumanu, African Sports ikabeba ubingwa na kuifanya Tanga kwa mwaka 1988 kung'ara ikibeba mataji yote makubwa ya msimu huo ikiwa ni rekodi kwao na haijawahi tena kutokea hadi Ligi ya Muungano ilipokuja kufutika 2003 na kuibuliwa tena kama Kombe la Muungano 2024.

Coastal na Sports kila moja msimu huo ilitwaa mataji hayo yaliyokuwa yakishikiliwa na Yanga iliyokuwa imeyatwaa msimu wa 1987, yaani kifupi Wagosi waliisafisha Yanga kibabe msimu huo.

MANGU 01

WANAMANGUSHI

Bila ya shaka kwa watoto wa 2000 ni ngumu kuelewa, Coastal a.k.a Wana Mangushi kwa msimu huo walikuwa moto kwelikweli kutokana na kuwa na kikosi cha kibabe kilichoweza kuzizima Yanga na Simba iliyokaribia kushuka daraja kwani ilimaliza ikiwa nafasi ya 10 kati ya timu 12 zilizoshiriki.

Mwanaspoti linakuletea jeshi zima la Wagosi wa Kaya waliobeba ubingwa huo wa Bara, likiwa ndilo taji pekee katika Ligi hiyo tangu ilipoasisiwa rasmi mwaka 1965 na walipo baadhi ya wachezaji hao walioiwakilisha nchi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) 1989.

Michuano hiyo ilifanyikia Nairobi, Kenya na Coastal kuonyesha ilikuwa sio timu nyepesi nyepesi, iliweza kufika hatua ya fainali na kupoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0 mbele ya watetezi wa taji hilo, Kenya Breweries (sasa Tusker FC) huku ikichezwa mechi hiyo saa chache tangu itoke kuing'oa AFC Leopards pia ya Kenya katika nusu fainali iliyopigwa usiku wa kuamkia mechi hiyo ya fainali.

MANGU 04

MAKIPA

Katika kikosi kilichobeba ubingwa huo wa Bara 1988, Coastal ilikuwa na makipa mawili, Hamisi Makene na Mohammed Mwameja. Makene ndiye alikuwa kipa namba moja, huku Mwameja wakati huo ndio akiibuka akiwa msaidizi wake na kila mmoja aliifanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa.

Makipa hao ndio walikuwa na kazi ya kuibeba Coastal katika mechi za msimu wa 1988 ambapo katika mechi 22 ilizocheza timu hiyo, iliruhusu mabao 18 na yenyewe kufunga mabao 26 na kutwaa taji mbele ya watetezi, Yanga.

Kwa sasa Mwameja anaendesha biashara zake jijini Dar es Salaam zikiwamo gareji za magari baada yakustaafu soka akiwa na Simba aliyoifikisha fainali za Kombe la CAF 1993.

MANGU 03

MABEKI

Skwadi la Coastal msimu iliyotwaa taji la Bara ilikuwa na mabeki wa pembeni watatu, akiwamo Said Salim 'Kolongo', Douglas Muhani na Joseph Lazaro walikuwa wakipokezana katika mechi 22 za msimu huo chini ya kocha Zakaria Kinanda 'Arrigo Sacchi' akisaidiwa na Joel Bendera na Jumbe Menye.

Lazaro kwa sasa ni kocha akiwahi kuifundisha kwa vipindi tofauti Coastal Union, African Sports na hata Mgambo JKT, wakati Muhani ni mchambuzi wa soka akijishughulisha na biashara, ilihali Korongo akitangulia mbele ya haki mnamo Novemba 21, 2018.

Kwa upande wa mabeki wa kati, Wagosi walikuwa na watu wa kazi akiwamo Yassin Abuu Napili,  Idrisa Ngulungu, Elisha John, Ally Mwaliva na Abdallah Tamim, waliotengeneza ukuta mgumu uliowapa kazi washambuliaji wa timu pinzani kuupita kwani hawakuwa wanacheka na yeyote uwanjani.

Napili kwa sasa anafanya biashara jijini Dar es Salaam, wakati Ngulungu aliyekuwa mchezaji kiraka akimudu nafasi karibu zote uwanjani ukiondoa kipa alitangulia mbele ya haki kutokana na ajali ya gari Agosti 2, 2013, wakati taarifa za Abdallah Tamim na Elisha John haijulikani walipo.

MANGU 05

VIUNGO

Eneo hili Coastal lilikuwa na mafundi kwelikweli ikijumuisha mawinga waliokuwa wakiteleza kama kambale kwa kasi na vipaji walivyokuwa navyo akiwamo Mohammed Kampira 'Kaball' aliyeitumikia timu hiyo tangu mwaka 1975 hadi 1992 kabla ya kugeukia ukocha hadi alipofariki dunia Mei 13, 2020.

Pia kulikuwa na Ally Maumba 'White Horse', mmoja ya viungo wabakaji wa aina yake waliowahi kutokea nchini akiwa na kipaji cha kumiliki mpira, akipiga chenga na kucheza kwa ajili, inaelezwa kwa sasa jamaa anaishi Ugiriki japo wengine wanasema yupo Hong Kong.

Viungo wengine waliokinukisha Coastal msimu huo ni Kassa Mussa, Aboubakar Hassan, Aggrey Chambo, Seifdin Kabange na Razak Yusuf 'Careca'. Kassa Mussa na Razak Yussuf 'Careca'  aliyeichezea timu hiyo tangu 1985 hadi 1991 kabla ya kujiunga na Simba aliyofika nao fainali ya Kombe la CAF 1993 inaelezwa wanafanya shughuli binafsi wakiishi barani Ulaya na kuna wakati huwa wanakuja nchini.

MANGU 06

WASHAMBULIAJI

Skwadi la Wagosi wa Kaya, lilikuwa na watu waliojua kuwatesa mabeki na makipa wa timu pinzani kwa kupiga chenga na kufunga mabao matamu yakiwamo ya mashuti makali ya mbali.

Safu ya ushambuliaji ya Coastal ya ubingwa iliongozwa na Juma Mgunda ambaye kwa sasa ni kocha wa Namungo akiwahi pia kuingoa Coastal na Simba na timu ya taifa, Taifa Stars kwa vipindi tofauti.

Mgunda alicheza sambamba na washambuliaji wengine mahiri waliotisha enzi hizo katik soka la Tanzania na anga za kimataifa kupitia timu y taifa, Tifa Stars, akiwamo Hussein Mwakuluzo na Kassim Mwajeki.

Skwadi hilo chini ya Zakaria Kinanda halijawahi tena kufanya maajabu kama iliyoafanya msimu huo wa 1988 kwani Coastal haijawahi sio kubeba ubingwa wowote, lakini hata kule kumaliza nafasi mbili au tatu za juu kwao imekuwa ndoto, japo msimu miwili iliyopita ilimaliza ya nne na kucheza mechi za kimataifa ambayo hata hivyo ilitolewa raundi ya kwanza na Bravo Maquiz ya Angola.