Haya sasa! Kazi ianze

TIMU nne za wanawake zitaumana Jumamosi hii katika michezo ya Ngao ya Jamii wakati JKT Queens itakapocheza dhidi ya Fountain Gate Princess huku macho na masikio ya wapenda soka yakiwa katika mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba.

Hii ni mara ya kwanza kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzisha michuano hiyo ambayo inazikutanisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu katika Ligi Kuu ya Wanawake Bara msimu uliopita.

JKT Queens ndio walikuwa mabingwa wa ligi hiyo msimu uliopita baada ya kukusanya pointi 46 wakifuatiwa na Simba Queens waliovuna pointi 45, Fountain Gate walikuwa wa tatu wakiwa na pointi 41 wakati Yanga Princess ilikamata nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 34.

Mechi zote mbili zitafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, ambako JKT Queens itacheza na Fountain Gate Princess kuanzia saa 9:00 jioni wakati Simba Queens na Yanga Princess zitacheza kuanzia saa 12:00 jioni.


Dabi ndio mpango mzima

Achana na mechi hiyo ya kwanza kati ya JKT Queens na Fountain Gate Princess, macho na masikio ya wadau wa soka hapa nchini yapo katika dabi ya Kariakoo.

Mechi ya Simba dhidi ya Yanga ndiyo inaonyesha kuwavutia zaidi mashabiki wa soka kwenda kuingalia na kuifuatilia kutokana na upinzani mkubwa uliopo baina ya timu hizo.

Usajili ambao timu zote mbili zimefanya msimu huu ndio sababu kubwa ya watu kuisuburi kwa hamu mechi hiyo kuona je wachezaji hao watazisaidia timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara ya wanawake msimu ujao inaotarajia kuanza Desemba 20?

Baada ya msimu uliopita kumalizika kupitisha panga kwa wachezaji 13, msimu huu Yanga imewaongeza kikosini wachezaji Madina Traore (kutoka Burkina Faso), Rechenelle Kiteko (Congo), Rehema Yahaya, Lucy Mwenda (Tiger Queens), Lidya Maximillian (TSC Queens)), Neema Paul (Fountain Gate Princess) Faiza Seidu (Ghana), Adejobe Ejalonibu (Raja Casablanca) na Kaeda Wilson  ‘Mzungu’.

Kwa upande wa Simba wenyewe wamewaongeza kikosini wachezaji Elizabeth Wambui (Kenya), Joanitah Ainembabazi (Uganda) na Diakiese Isabelle kutoka Congo.

Jambo la kufurahisha ni kwamba ukipitia mtandao wa kijamii wa instagram wa Simba Queens, mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakiwahamasisha wachezaji wao na kuwataka kushinda mchezo huo ili kuwalipia kisasi cha mabao 5-1 ambacho kaka zao walikipita kutoka kwa Yanga Novemba 5 mwaka huu.


Yanga inakwama wapi kwa Simba?

Tangu msimu mwaka 2018, Yanga Princess imekutana na Simba Queens mara 10 lakini imeambulia ushindi mara moja tu huku mechi sita ikipoteza na kutoka sare mara tatu.

Katika mechi hizo 10, Yanga iliruhusu mabao 29 huku yenyewe ikifunga mabao manane tu.

Yanga Princess iliwahi kuifunga Simba Queens mara moja tu kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Aprili 24 mwaka 2022, bao lililofungwa na Clara Luvanga ambaye kwa sasa  anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Al Nassr  ya Saudi Arabia.

Kocha wa Yanga Princess, Mzambia Haaalubono Charles anasema haitakuwa mechi rahisi kutokana na rekodi ya Simba waliyonayo dhidi yao lakini anaamini watapambana zaidi kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.

“Maandalizi kwa upande wetu yanaendelea vizuri na nina furaha kwa ninachokiona mazoezini kutoka kwa wachezaji wangu kwani kila siku wanaimarika.

“Ukiangalia rekodi baina ya wapinzani wetu unaona kwamba Simba ni timu nzuri  hivyo tunahitaji kuingia ndani ya uwanjani na kujaribu kupambana zaidi dhidi yao. 

“Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu najua wenzetu bado wanaamini katika rekodi hiyo hivyo tunatakiwa kujiandaa vizuri na kuwa tayari kwa ajili yao,” anasema Charles.

Naye kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ’Mgosi’ anasema wao malengo yao ni kushinda mchezo dhidi ya Yanga ili kutinga fainali na kuwa timu ya kwanza kubeba ubingwa wa michuano hiyo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika kwa upande wa wanawake nchini.

“Tunawashukuru TFF, kamati ya ligi na wadau waliokuwa wakihamasisha haya mashindano yawepo  kwa ajili ya kukuza soka la wanawake, kama Simba tumeyafurahia kwani yatatupa mazoezi mazuri tunapoelekea kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu.

“Maandalizi yetu ni mazuri licha ya kwamba wachezaji kama 12 wameenda kuzitumia timu zao za Taifa lakini hilo halitupi shida kwani hata huko wanapata mazoezi mazuri na wakirejea wataungana na wenzao tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi,” anasema Mgosi na kuongeza;.

“Msimu uliopita  tulikosa ubingwa wa ligi hivyo msimu huu tunajipanga kwanza kuchukua Ngao ya Jamii kwani kuna msemo unasema ‘Nyota njema huonekana asubuhi’ hivyo tunaamini tukibeba ngao basi itatusafishia njia ya kuchukua ubingwa wa ligi msimu ujao.


MSIKIE KOCHA FOUNTAIN GATE

Kocha wa Fountain Gate Princess, Juma Masoud anasema wanaendelea na maandalizi katika kambi yao iliyopo Misungwi Mwanza kujiandaa na mechi dhidi ya JKT Queens huku akifurahia kuanzishwa kwa mashindano hayo.

“Tumefurahi kuanzishwa kwa mashindano haya kwani ukiangalia soka la wanawake Tanzania hakuna mashindano mengi ni ligi tu inachezwa tena inashirikisha timu chache.”

 labda sisi Fountain ndio kidogo tunanufaika na kucheza mechi nyingi kwa sababu tuna mashindano yetu mengine binafsi.

“Tunaendelea kujindaa kwa ajili ya Ngao ya Jamii na ligi kwa ujumla, tumeweka kambi Misungwi kwa wiki mbili sasa na tumecheza mechi tatu za kirafiki ambazo zimetupa mazoezi mazuri na tunajua tunakutana na mabingwa watetezi wa ligi hivyo mechi haitakuwa rahisi lakini tumejipanga, “anasema Masoud.

Fountain Gate Princess imecheza michezo mitatu ya kirafiki dhidi ya Alliance Girls na kutoka nayo suluhu kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Bunda Queens na ikachapa Geita Gold Queens bao 1-0.

Naye kocha msaidizi wa JKT Queens, Azish Kondo anasema wameyafurahia mashindano hayo kwani ni moja ya mazoezi wanapoelekea kuanza msimu mpya wa ligi.

“Tunafanya mazoezi kujiandaa na mechi hiyo ya ngao ya jamii pamoja na ligi kwa ujumla. Mechi dhidi ya Fountain itakuwa ngumu kwani ni timu nzuri lakini dakika ya 90 zitaamua wa kwenda fainali, “anasema Kondo.