Haya ndio makosa makubwa mawili ya Simba msimu huu
Muktasari:
Na ndio maana huwezi kushangaa kuona Malaga ikishinda ugenini dhidi ya Barcelona bao 1-0, huwezi kushangaa kuona Swansea wakiifunga Manchester United mabao 2-1. Hilo ndilo soka la Ulaya na ndio maana tunalipenda.
TUMEKUWA tunashuhudia matokeo ya kushangaza katika Ligi Kuu za Ulaya. Ni matokeo ambayo hayana shaka hata kidogo na yanafanya ligi za huko kuvutia kila wiki.
Na ndio maana huwezi kushangaa kuona Malaga ikishinda ugenini dhidi ya Barcelona bao 1-0, huwezi kushangaa kuona Swansea wakiifunga Manchester United mabao 2-1. Hilo ndilo soka la Ulaya na ndio maana tunalipenda.
Huku kwetu Tanzania ni vigumu sana kujua matokeo halisi ya uwanjani, kwa sababu rushwa inatawala zaidi katika mechi tofauti na uhalisia wake.
Mechi inaweza kuchezwa siku mbili kabla ya mechi yenyewe. Mwamuzi wa mchezo anajua matokeo kabla ya mechi yenyewe. Makomandoo wanajua matokeo kabla mechi haijachezwa.
Hata hivyo, unaweza kuona hali hiyo ya mechi kuchezwa nje ya uwanja imeanza kupungua. Na ndio maana unaona timu kama Simba ikifungwa na timu ndogo kama Stand United, au Azam ikilazimishwa suluhu na Polisi na baadaye Prisons.
Hapa tulipofika ndio panapostahili. Mpira sasa unachezwa uwanjani na hicho ndicho tunachokitaka, kwa sababu ilikuwa inaudhi sana kuona kila mechi Yanga na Simba ndio zinashinda.
Hata hivyo, sipendi kulijadili hilo katika uchambuzi huu, ila nataka nijaribu kuangalia sababu ambazo zinaifanya Simba iendelee kusuasua katika Ligi Kuu Bara.
Kwanini Simba haifanyi vizuri? Kunaweza kuwa na sababu nyingi, kila mchambuzi atakuwa na sababu zake, lakini sababu kubwa kwangu itakuwa ni kikosi cha kwanza kubadilika ghafla ndani ya muda mfupi na timu hiyo kuwa na wachezaji wengi chipukizi.
Katika kikosi kilichocheza mwishoni mwa wiki dhidi ya Stand United, kulikuwa na wachezaji wawili tu wa Simba ambao walicheza msimu uliopita. Wachezaji wengine wote ni wapya. Walikuwa ama wamesajiliwa dirisha dogo au walikuwa wametokea timu ya vijana ya Simba.
Kikosi cha Simba dhidi ya Stand United kilikuwa hivi: Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Murshid Juuko/Said Ndemla, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Abdul Banda, Elius Maguli, Ibrahim Ajib/Danny Sserunkuma na Emmanuel Okwi/ Simon Sserunkuma.
Katika kikosi hicho ni wachezaji wawili tu: Jonas Mkude na Ramadhani Singano ambao walicheza msimu uliopita kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa msimu.
Kipa Ivo Mapunda, alisajiliwa wakati wa dirisha dogo na wachezaji waliobaki wengi walikuwa wakitokea timu ya Simba B na wengine ni wapya kabisa. Emmanuel Okwi alikuwa Yanga.
Kwa hiyo kwa kuangalia kikosi hiki utagundua kuwa katika kikosi cha kwanza cha Simba, wachezaji ambao walikuwapo msimu uliopita hawazidi watatu.
Huwezi kufanya vizuri ukiwa na wachezaji wanane uwanjani au tisa wapya katika timu. Haiwezekani kwa sababu wachezaji wanahitaji muda kuzoeana.
Ukiangalia kikosi cha Yanga ambacho kimeifunga Mbeya City mabao 3-1 mwishoni mwa wiki, kulikuwa na wachezaji wawili tu wapya; Andrey Coutinho na Amissi Tambwe. Wengine wote ni wa zamani.
Kwa vyovyote vile Yanga itaendelea kutamba na kuwa nzuri kwa sababu wachezaji wake wamezoeana kwa muda mrefu tofauti na Simba ambayo imekuwa ikibadili kikosi chake kila msimu.
Ukichukua picha ya Simba ya msimu uliopita, unaweza kuwaona wachezaji watatu tu waliobaki katika kikosi cha kwanza cha sasa tofauti na Yanga ambayo ukichukua picha yao unakuta kuna sura mbili tu mpya.
Lakini sababu nyingine muhimu ambayo Simba wanatakiwa kuiangalia ni umri wa wachezaji wao. Ukiondoa Mapunda, Okwi na Sserunkuma, wachezaji wengine wote wana umri wa miaka 19 mpaka 23. Katika umri huu kuna mambo mengi.
Huu ni umri ambao vijana wamefika katika hatua ya kujiachia, wakifika Shinyanga badala ya kufikiria mechi, usiku huo watakwenda disko, watazurura hovyo na siku ya pili watakwenda kwenye mechi wakiwa wamechoka.
Ni tofauti na Yanga ambako wachezaji wengi wamepita umri huo na wanatambua majukumu yao nje na ndani ya uwanja.
Kikosi cha Yanga dhidi ya Mbeya City kilikuwa hivi; Ali Mustafa, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amiss Tambwe, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho.
Katika kikosi hicho cha Yanga karibu wachezaji wote wamevusha ‘umri wa kujiachia’.
Hawa ni binadamu bado, lakini kutokana na umri wao wanatambua majukumu yao na wanafahamu jinsi ya kusawazisha.
Kwa hiyo makosa makubwa mawili ambayo Simba wameyafanya ni kubadilisha kabisa kikosi chao cha msimu uliopita, lakini pia wameshindwa kuweka uwiano sawa wa umri wa wachezaji wao.
Nimeifuatilia Simba mechi nyingi, sioni kama ni timu inaweza kuchukua ubingwa kwa kikosi hiki, hawawezi kushika nafasi ya pili pia. Wanahitaji kutumia nguvu kubwa kushika nafasi ya tatu.