Hawavumi ila wamo sana tu

Tuesday April 20 2021
hawavumi pic
By Olipa Assa

KUNA wachezaji Simba, Yanga na Azam FC wanafanya kazi kubwa, ila majina yao yanakuwa midomoni mwa mashabiki pindi ikitokea wamefanya kitu cha kuwapa furaha, nje ya hapo majina yao hayana bahati ya kutajwa mara kwa mara kama ilivyokuwa kwa mastaa wengine.

Mbaya zaidi wao ni wachezaji wanaokutana na maneno makali inapotokea wakafanya makosa ya kibinadamu uwanjani, ambayo yakifanywa na mastaa wao pendwa hawapigiwi kelele kama zao, jambo ambalo linaonekana thamani yao ni ndogo, licha ya huduma zao kuwa muhimu.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa hao wanaojituma na thamani yao inaonekana pale tu wanapofanya kitu, baada ya hapo husikii wakitajwa ama kupewa nafasi kama ilivyo kwa wengine.


MZAMIRU YASSIN - SIMBA

Licha ya kwamba jina lake haliimbwi sana na mashabiki wa Simba tofauti na ilivyo kwa mastaa wengine, Mzamiru ni mchezaji mpambanaji aliye na muendelezo wa kiwango chake tangu asajiliwe ndani ya kikosi hicho mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Advertisement

Ni mchezaji mwenye nguvu, zinazomwezesha kupambana na kuchhangia kuliweka salama eneo la kati la Simba. Pamoja na kutimiza majukumu yake ya kiungo, Mzamiru kufikia sasa ametupia mabao mawili na ametoa asisti moja ya bao.


ERASTO NYONI - SIMBA

Kulingana na umri wake hana cha kupoteza, ila Erasto bado ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Simba. Uwezo wake na namna anavyobadilisha mchezo timu ikiwa imezidiwa ni vitu vya kawaida kwake kwani ni mchezaji mzoefu mwenye kipaji kikubwa, anayetumia akili na nguvu katika kuifanya kazi yake.

nyoni zoezi pic

Nyoni ni kati ya wachezaji wachache duniani wanaocheza nafasi nyingi uwanjani kwa ubora ule ule. Anacheza nafasi zote za ulinzi nyuma ikiwamo kiungo cha ulinzi, na pia kiungo wa kati au wa ushambuliaji.

Miguu ya Erasto ni miguu ya dhahabu. Anajua kuficha mpira na pia ni mtu hatari sana akipiga frii-kiki.

Erasto pia anarusha mpira kama kona, ingawa haonekani akifanya jambo hili mara kwa mara.Mwalimu Alex Kashasha anasema huyu ni mtu ambaye kila wakati ana vitu vipya miguuni mwake.


DEUS KASEKE - YANGA

Ni kati ya wachezaji muhimu katika kikosi cha Yanga, akianzia benchi mara nyingi amekuwa akibadilisha mchezo kama vile kulazimisha mashambulizi, akitumia nguvu na kucheza kwa chenga za hapa na pale za kuwasumbua mabeki na viungo wakabaji wa upinzani.

KASEKE PICHA

Miongoni mwa michezo ambayo Kaseke alifanya kazi kubwa ya kuipa Yanga pointi moja ni mechi dhidi ya Mbeya City iliyopigwa Februali 13, 2021 kwenye Uwanja wa Sokoine, ambapo aliingia kipindi cha pili na kufunga bao dakika ya 84 na mchezo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mbali na hilo Kaseke hadi sasa ameifungia timu yake mabao sita na asisti tatu za mabao, lakini bado sio kati ya wachezaji vipenzi vya mashabiki.


SALUM ABUBAKAR - AZAM

Mastaa mbalimbali wamewahi kukiri umahiri wa kazi za Sure Boy, miongoni mwao ni aliyekuwa kiungo wa Yanga, Papy Kabamba ‘Tshishimbi’, Emmanuel Gabriel (mchezaji wa zamani wa Simba). Lakini Sure Boy si mchezaji anayetajwa sana hadi itokee amefanya kitu kikubwa dhidi ya Simba na Yanga, nje na hapo mechi ambazo hazipo midomoni mwa mashabiki wa klabu hizo kongwe ni ngumu kusikika.

Ni mchezaji anayetibua mipango ya wapinzani wao, akisaidiana na mabeki wa timu yake kuwakaba washambuliaji wa timu pinzani kabla ya kumfikia kipa, ukongwe wake anautumia vyema kuisaidia Azam katika mechi mbalimbali.


BENARD MORRISON - SIMBA

Namna jina lake linavyotajwa Simba limepoa, sio kama alivyokuwa anatajwa kila kona wakati yupo Yanga iliyomsajili kwa mara ya kwanza 2020 akitokea DC Motema Mapembe, lakini ni mchezaji mwenye madhara pindi anapopewa nafasi ya kucheza na amekuwa msumbufu kwa wapinzani na kuipa faida timu yake kupata frii-kiki ambazo wakati mwingine zinakuwa zinawapa mabao.

hawavumi morisoni pic

Japo nafasi yake sio kubwa ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza ama kuingia akitokea benchi, Morrison hadi sasa amefunga mabao matatu na asisti tatu za mabao ya Ligi Kuu Bara nje na mashindano mengine kama CAF na Kombe la Shirikisho Afrika.


METACHA MNATA-YANGA

Ni kama jina lake kwasasa linataka kusahaulika kutokana na kutocheza mechi kadhaa, ila ni kipa muhimu ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kumpa ushindani Faruk Shikhalo, huku mdogo wao Ramadhan Kabwili akiendelea kupata uzoefu kwao.

Wakati Metacha anaanza kikosi cha kwanza jina lake lilikuwa kubwa midomoni mwa mashabiki wa Yanga, kipindi hicho Shikhalo akipambana kupigania namba na sasa amefanikiwa. Ili Yanga iwe na ushindani katika nafasi ya kipa, bado itawahitaji makipa hao wawili washindane kama ilivyo kwa Simba kati ya Aishi Manula na Beno Kakolanya, licha ya kwamba sio namba moja ila anaongeza ushindani kikosini.

Advertisement