Hawa wamechomesha VPL

Muktasari:

LIGI Kuu Bara imeingia raundi ya pili ikiwa ni katika mbio za mwisho mwa msimu ili imalizike na bingwa aatakayenyakua ndoo ajulikane

LIGI Kuu Bara imeingia raundi ya pili ikiwa ni katika mbio za mwisho mwa msimu ili imalizike na bingwa aatakayenyakua ndoo ajulikane.

Wakati ligi ikiwa ikiingia hatua hiyo kuna wachezaji ambao wamefanya makosa yaliyozigharimu timu zao kwa namna moja au nyingine katika mechi zilizopita.

Mwanaspoti linakuletea matukio yaliyotokea kwa baadhi ya wachezaji na kufanya timu pinzani zinufaike na makosa waliyoyafanya.

FARID vs NAMUNGO

Winga wa Yanga, Farid Mussa katika mchezo wao dhidi ya Namungo aliifanya Namungo ipate bao la kusawazisha na mpira kwisha kwa matoke ya kufungana bao 1-1.

Farid alishindwa kumiliki mpira akiwa nje kidogo ya boksi lao na baada ya hapo alishindwa kuumiliki mpira vizuri na kujikuta ukiondoka miguuni mwake ukichukuliwa na Sixtus Sabilo ambaye haraka alipiga pasi kwa Steven Seyi aliyegeuka na kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ na Namungo kusawazisha kupitia staa wao, Seyi.

MWAMNYETO vs RUVU SHOOTING

Mechi hii mabeki wa Yanga walikuwa na makosa mengi jambo lililowafanya wafanye makosa madogomadogo mara kwa mara.

Bakari Mwamnyeto alifanya kosa katika dakika 59 baada ya kushindwa kutulia na mpira akiwa ndani ya boksi na kujikuta akitoa pasi kwa mshambuliaji wa Ruvu Shooting, David Richard na kufanya timu hiyo isawazishe.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Michael Sarpong na baadaye Ruvu walisawazisha kupitia Richard, kisha Yanga wakapata bao la ushindi baada ya beki wa Shooting kujifunga na matokeo kuwa 2-1.

MBISA vs YANGA

Kipa Mussa Mbisa - huyu kwanza alikubali kichapo cha mabao matano katika mchezo wao dhidi ya Yanga baada ya kushindwa kulilinda lango na mabeki wake.

Katika mchezo huo kwenye bao la tatu, Mbisa alishindwa kupiga hesabu za haraka kama ataweza kuucheza mpira mrefu wa Lamine Moro ambao ulizaa bao kupitia kwa Yacouba Sogne.

Lamine alipiga mpira mrefu, lakini kipa huyo alitoka langoni na kwenda kuruka katikati ya mabeki wake wawili na kumfanya Yacouba asiwe na kazi kubwa badala yake alituliza mpira na kutupia wavuni.

JUMA SHEMVUNI vs BIASHARA UTD

Beki Juma Shemvuni wa Mbeya City aliifanya Biashara United ipate bao mapema dakika ya tisa baada ya kushindwa kutuliza mpira vizuri wakati akiwa anauwahi uliokuwa wenyewe.

Shemvuni alipopoteza tu hatua chache, winga wa Biashara United, Christian Zigah aliuwahi mpira na kumuangalia kipa wa Biashara na kuupiga pembeni ya bega na kwenda wavuni. Katika mchezo huo Mbeya City walipoteza kwa kufungwa mabao 3-0.

METACHA vs DODOMA

Ukitaja makipa ambao wanafanya vizuri kwa sasa katika mchezo wa soka hapa nchini kwa ujumla hauwezi kuliacha jina la Metacha Mnata wa Yanga kutokana na kiwango chake ambacho amekuwa akikionyesha katika michuano mbalimbali ambayo timu hiyo inashiriki

Hali hiyo ndio maana hata kuachwa kwake katika kikosi cha wachezaji wa Taifa Stars wanaojiandaa kwa ajili ya michuano ya Chan imeibua mijadala mingi kwani wengi wana imani naye.

Lakini katika mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji, Metacha dakika ya pili mchezo alichomesha bao baada ya kushindwa kudaka vizuri krosi iliyopigwa na Dickson Ambundo, kwani aliudaka mpira na kuuachia huku akiwa hajaangalia pembeni yake kuna nani na Seif Karie alitupia wavuni licha ya Yanga kushinda 3-1.

KASEJA vs IHEFU

Kipa mkongwe Juma Kaseja wa KMC alishindwa kuzungumza vizuri na beki wake wa kati Lusajo Mwaikenda katika mchezo wao dhidi ya Ihefu na kufanya Ihefu ipate bao dakika ya nane likiwa ndilo la ushindi.

Mwaikenda alituliza mpira wa juu kwa kifua mbele ya Kaseja huku akiwa hajaangalia nyuma nani anakuja, wakati huohuo Kaseja naye alishindwa kuudaka mpira huo na kuishia kuugusa tu mwili wa Joseph Kinyozi ambaye hakufanya makosa bali alitupia bao wavuni.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 90.