Hawa ni wanaotisha RBA

HATUA ya mzunguko kwenye Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) imemalizika na sasa timu nane upande wa wanaume zitaanza kuonyeshana kazi kwenye hatua ya robo fainali itakayoanza leo kwenye Uwanja wa Don Bosco Oysterbay huku wanawake mechi za  hatua hiyo zikitarajiwa kuanza Septemba.
Wakati robo fainali ikianza leo Jumatano kuna wachezaji walitisha kwenye hatua ya mzunguko wa ligi hiyo na kwa mujibu wa mkurugenzi wa ufundi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam(BD), Haleluya Kavalambi mwisho wa msimu vinara watapewa zawadi kama itakavyokuwa kwa vinara wa mechi za mtoano (play off).
“Sasa tunakwenda na utaratibu tofauti yaani hatufanyi kama zamani ambapo  mfungaji bora alikuwa mmoja tu hadi mwisho wa msimu, lakini kwa sasa tutakuwa kila eneo na wachezaji bora, mfano kutakuwa na mfungaji bora wa hatua ya mzunguko na pia tutakuwa na mfungaji bora wa hatua ya mtoano (play off),” anasema Haleluya.

Ufungaji Bora
Kwa upande wa wanaume Tyrone Edward wa UDSM Outsiders aliibuka kinara kwa kufunga pointi nyingi kwenye hatua ya mzunguko wa ligi hiyo akiwa amefunga pointi 300  sawa na robo ya tatu ya pointi ambazo timu yake imefunga katika mechi 14 ilizocheza.
Outsiders imefunga jumla ya pointi 925 huku ikiruhusu kufungwa pointi 788.
Abas Omary wa Chui ameshika nafasi ya pili kwa kufunga pointi nyingi akiwa ametupia kwenye nyavu pointi 253 huku Jonas Mushi wa JKT  akifunga pointi 234
Wakali wa mitupo mitatu (Three Point)
Huko kwenye kikapu kuna burudani hadi basi kwani achana na kufunga pointi nyingi tu, lakini je unafungajefungaje?
Hakuna jambo ambalo linavutia na kuwafurahisha mashabiki wa mchezo huo kama mchezaji akifunga akiwa mbali yaani nje ya D - ni jambo linalosisimua na kuamsha shangwe.
Sasa hakuna mchezaji mtaalamu wa kufunga kwa mipira ya mbali (three points)  kwenye hatua ya mzunguko kama Erick Lugora wa Pazi ambaye amefunga kwa mitupo mitatu minne. Erick amefuatiwa na Jonas Mushi wa  JKT aliyefunga kwa mitupo mitatu mara 40 wakati Joas Maheta wa Savio  akiwa wa tatu kwa kufunga mara 31.

Asisti
Pasi za mabao hazipo kwenye soka tu kwani hata katika kikapu nako watu hawako nyuma katika kumuhadaa adui na kutoa pasi nzuri kwa wachezaji wenzao. Omary Ndula wa JKT ameibuka kinara wa kutoa pasi nzuri zilizosaidia timu yake kupata pointi katika michezo waliyocheza kwani ametoa asisti 79 akifuatiwa na Robert Nakuru wa Mchenga Stars aliyetoa pasi 62 wakati Alex Clement wa Pazi alitoa pasi 58

Rebound
Ili uweze kushinda kwenye kikapu lazima uwe vizuri katika kufunga, lakini pia uwe na watu wa maana wanaojua kulinda goli na kudaka mipira yaani rebound. Watu hao wa maana kwenye mpira wa kikapu wanaitwa ‘mabig’ na timu nyingi huwa zinawatumia wachezaji wenye miili mikubwa kwa lengo la kuhakikisha wanadaka mipira yote inayoelekea kuingia ndani ya goli lao. Basi bwana kuna wakali wa hizo kazi ambao hawana mchezo katika kulinda goli wakiongozwa na Jordan Manang wa Mchenga aliyeokoa mara 179, akifuatiwa na Sisco George wa Ukonga Kings aliyeokoa mara 158 sawa na Diuglas Kandulu wa Pazi.  

Steal (kuiba mipira)
Kwenye kikapu  mchezaji anatakiwa kuwa mjanja mjanja ili kuifanya timu yake iongoze kwa pointi nyingi ikiwemo kuhakikisha unaiba mipira kwa wapinzani (steals) na kwenda kufunga.
Alinani Msongole wa ABC ndiye kinara wa kuiba mipira akiwa amefanya hivyo mara 30 akifuatiwa na Robert Nakuru wa Mchenga Stars aliyeiba mara 26 wakati Stanley Mtunguja  wa Ukonga King akichukua mipira mara 18.

Kwa wanawake moto Burudani haikuwa kwa wanaume tu kwani hata wanawake kulikuwa moto na kuzalisha wakali kibao katika vipengele tofauti. Faraja Mhomisori wa Jeshi Stars ametupia nyavuni pointi 319, huku Noela Renatus wa Vijana Queens akiongoza kwa asisti 81.