Giza la ubingwa msimu huu limeanza kuingia Yanga

Muktasari:

YANGA wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa wamekusanya pointi 51 mbele ya Azam na Simba. Azam ana pointi 49 wakati Simba ana pointi 46. Hata hivyo, Yanga ipo na Azam wapo mbele michezo dhidi ya Simba ambao wamecheza mechi 21 ikiwemo ya jana Jumatano na Mtibwa Sugar.

YANGA wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa wamekusanya pointi 51 mbele ya Azam na Simba. Azam ana pointi 49 wakati Simba ana pointi 46. Hata hivyo, Yanga ipo na Azam wapo mbele michezo dhidi ya Simba ambao wamecheza mechi 21 ikiwemo ya jana Jumatano na Mtibwa Sugar.

Simba wana mechi za viporo zilizotokana na kuwa na ratiba ya mechi za kimataifa ambapo wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa wametinga hatua ya robo fainali, hivyo kama mechi za viporo hazitamalizika hadi mwezi ujao bado wataendelea kuwa na mechi mkononi.

Viporo vya Simba haviwatishi wala kuwakatisha tamaa Yanga, maana inawezekana wakashinda ama kupoteza na wkaipoteza basi hapo ndipo penye matumaini makubwa ya ubingwa kwa Yanga.

Hata hivyo, ili Yanga watwae ubingwa huo ni lazima washinde mechi zao zote na sio kutoka sare ambazo zinawapunguzia pointi lakini pia wakifunga na kuomba watani zao wapoteze mechi zao iwe za kiporo ama zilizomo kwenye ratiba yao.

Sidhani, ingawa inawezekana Simba wakapoteza mechi zao ama kutoka sare nyingi tu. Lakini kwa namna ambavyo wamepania kutetea ubingwa wao na namna ambavyo wana ari ya ushindi kuanzia kimataifa, uwezekano wa kupoteza basi ni kwa asilimia ndogo sana.

Wanasema kwenye mpira lolote linawezekana lakini si kwa kiwango hiki tunachokiona kwa Yanga ambao kadri siku zinavyoenda mbele ndivyo wanavyozidi kupoteza umakini uwanjani.

Kwa hakika mashabiki wao wameanza kukata tamaa ingawa viongozi wao wanawaaminisha kuwa ni lazima watwae ubingwa wa ligi, sawa na inawezekana, lakini je kwa kiwango gani ambacho wachezaji wanakipambania uwanjani ili kupata matokeo mazuri?

Inawezekana viongozi wanapambana kwa kila njia kuhakikisha timu yao inafanya vizuri ila hawajui wana wachezaji wa aina gani wa kuwapa matokeo mazuri, hapo nguvu inaweza kupotea bure.

Wanaleta kocha mpya, sawa ila wanamleta ili aje apate matokeo gani na kwa timu ipi ya kubeba ubingwa? Naamini hapa ni lawama, labda kama wanamleta kocha mpya ambaye anakuja kuizoea ligi na kuwasoma wachezaji ili msimu ukimalizika awe na maamuzi yake.

Ila kama nia ni kutwaa ubingwa, basi huko kutakuwa ni kuwadanganya wanachama na mashabiki wao pia kumtwisha zigo la lawama kocha wao, kwa timu ambayo tayari usiku umeanza kuingia.

Nadhani, Yanga wanapaswa kupambana tu kuonyesha kile walichonacho kwasasa na sio kutumia nguvu kubwa kupigania kitu ambacho msimu huu hawajajipanga nacho, wacheze soka ila wakiamini kwamba wanatengeneza timu ya kutwaa ubingwa kwa miaka ijayo.

Hata watani zao walisota sana kufikia hapo walipo, walisahau hata njiapanda Kipawa ikoje kwani kupanda Ndege kwao ilikuwa ni ndoto, nakumbuka walikuwa na mchezo kama wanaoufanya Yanga hivi sasa.

Kwanza Simba kipindi hicho walikuwa na ukata mkubwa hata kusajili wachezaji wa viwango vya juu ilishindikana, wadau na wenye mapenzi na timu ndiyo walitoa fedha zao mfukoni kusajili lakini usajili wao ndiyo ule wa tiamaji tiamaji. Wakati Simba wanaungaunga huku Yanga chini ya tajiri wao Yusuf Manji walifanya kufuru kwa kuleta wachezaji wa hadhi ya juu, waliishi vizuri na kulipwa mishahara minono kama ilivyo watani zao sasa. Wao hivi sasa wana GSM lakini si kwamba anamaliza kila kitu kwa kipindi kifupi, anachokitoa kwenda Yanga ni kikubwa ila huenda hawakufanya uchunguzi wa kiwango cha juu kwenye usajili wao, walitaka mafanikio ya haraka sana pasipo kuangalia wameikuta Yanga ipo sehemu gani. Hivi sasa, viongozi wa Yanga wana vita mbili, malalamiko ya kuonewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kupambania ubingwa, sasa hapo ni lazima moja litawaponyoka kama hawatakuwa i dakika hizi za lala salama. Na pengine wanayafanya hayo yote kwa pamoja tayari wamejua kuwa nini kipo mbele yao kwa upande wa timu kupata matokeo mazuri uwanjani, ila inafikirisha sana.