Gamondi kaupiga mwingi kikosi Stars
Muktasari:
- Kuita kundi kubwa la wachezaji kama hivyo kuna faida kubwa kwa Gamondi mwenyewe na benchi lake la ufundi na pia kwa timu kiujumla kuliko angeita idadi kamili ya wachezaji 28 ambayo ndio inatakiwa ishiriki AFCON kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
INAWEZEKANA baadhi ya watu wasimuelewe kocha Miguel Gamondi kwa kuita wachezaji 53 katika kikosi chake cha awali kwa ajili ya AFCON 2025 lakini kijiwe kimemuelewa sana.
Kuita kundi kubwa la wachezaji kama hivyo kuna faida kubwa kwa Gamondi mwenyewe na benchi lake la ufundi na pia kwa timu kiujumla kuliko angeita idadi kamili ya wachezaji 28 ambayo ndio inatakiwa ishiriki AFCON kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kwanza, Gamondi anapata wigo mpana wa uteuzi wa wachezaji tofauti na angeita idadi hitajiwa kwa vile angelazimika kwenda na haohao hata kama baadhi watakuwa hawako katika ubora hivi sasa.
Lakini kuita idadi hiyo kubwa, inampa mwanya wa kubaki na walio bora na kuondoa wengine ambao atawaona kama hawajatosheleza mahitaji yake katika fainali hizo ambazo tumepangwa kundi C na timu za Uganda, Nigeria na Tunisia.
Hapo wachezaji watalazimika kuonyesha kiwango bora kwa vile kila mmoja atakuwa anahofia ushindani uliopo tofauti na wangekuwa wachache ambapo wangebweteka na kushindwa kumpa mwalimu na benchi lake la ufundi kile ambacho wanahitaji.
Kwa upande mwingine kuita wachezaji wengi kunatoa fursa kwa baadhi ya vijana wadogo kufanya mazoezi ya pamoja na kaka zao na kupata uzoefu ambao utawasaidia wao na timu za taifa siku za usoni hata kama wasipopata fursa ya kwenda Morocco hapo baadaye.
Wachezaji kama Abdulkarim Kiswanya, Vedastus Masinde, Abel Josiah, Cyprian Kachwele, Athumani Makambo na Sabri Kondo wanahitaji nyakati kama hizi ili kupata uzoefu wa nyota waliowatangulia ambao wametumikia Taifa Stars kwa muda mrefu.
Kijiwe kimependa pia kuona Gamondi amerudisha baadhi ya wachezaji ambao kabla ya ujio wake, baadhi walionekana kufungiwa vioo na kutopewa fursa ya kuitwa katika kikosi cha timu hiyo.
Ni kuonyesha kwamba yaliyopita si ndwele na sasa anataka kuwafanya wawe na mwanzo mpya katika kikosi cha timu yetu ya taifa.