FUENTES: Aziz KI sio wa mchezo mchezo

Muktasari:
- Aziz KI alifunga mabao wakati Yanga ikishinda 6-0 akiwa ametokea benchi, na kuchangia jingine lililofungwa na Dube Abuya na kumfanya aivushe Yanga kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao manne hadi sasa.
ACHANA na mabao mawili aliyofunga huku akiuchunua kushangilia kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar wakati Yanga ikiing'oa kwa aibu CBE SA ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 7-0, kuna beki mmoja mahiri wa Azam, Yeison Fuentes amemtaja Stephane Aziz KI kama balaa zito katika Ligi.
Aziz KI alifunga mabao wakati Yanga ikishinda 6-0 akiwa ametokea benchi, na kuchangia jingine lililofungwa na Duke Abuya na kumfanya aivushe Yanga kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao manne hadi sasa.
Nyota huyo wa Yanga msimu uliopita alimaliza kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu akifunga mabao 21, huku akihitimisha vita ya eneo la kiungo dhidi ya nyota wa timu nyingine za ligi hiyo, lakini Fuentes anakiri hata yeye hawezi kumsahau Aziz KI kwa namna alivyompa wakati mgumu tangu atue nchini.
Fuentes amefichua siri amekuwa na wakati mgumu katika dakika 270 alikutana na Yanga akiwa na Azam kwa namna Aziz KI alivyomkosesha amani na kusema jamaa sio mtu wa mchezo mchezo licha ya kuonekana anatabasamu muda wote wa mchezo.
Fuentes amejiunga na Azam FC dirisha dogo la usajili msimu uliopita amekutana na Yanga mara tatu lakini hatokaa akasahau dakika 90 za fainali ya FC huku akimtaja kiungo Aziz Ki

DAKIKA 90 ZA AZIZ KI
Beki wa Azam FC, Fuentes licha ya kutumika na timu hiyo kwenye mechi tatu dhidi ya Yanga ameutaja mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho kuwa alikuwa na kazi maalum.
"Mchezo wangu bora tangu nimetua Tanzania ni mechi dhidi ya Yanga ambao tulicheza Zanzibar siku hiyo nilipewa kazi maalum," anasema beki huyo raia wa Colombia na kuongeza;
"Sitaweza kuusahau huo mchezo haikuwa kazi rahisi niliyopewa niliambiwa nimkabe Aziz Ki muda wote nisimpe upenyo kwasababu ndio mchezo hatari kikosini kwao."
Fuentes anasema alikuwa anamkaba hadi kivuli ili kumthibitishia kocha wake kwamba kazi anaiweza hakuna kinachoshindikana huku akiweka wazi kuwa alikuwa na siku ngumu sana.
"Sio rahisi kumkaba Aziz Ki licha ya kufanikiwa kumkaba na kuto kumpa nafasi ya kupachika bao hata moja siku hiyo nilikuwa na wakati mgumu mno na naelewa hata yeye nilimtoa mchezoni hadi alishindwa kupiga penati kwa usahihi." Anasema.

MSIMU WA MATAJI
Kila mchezaji ndoto yake ni kutwaa mataji hakuna mchezaji ambaye anafurahia kiasi cha fedha anachokipokea bila ya mafanikio ya kuvaa medali na mataji kama ambavyo anathibitisha Fuentes.
"Ndoto yangu ni kucheza timu yenye mafanikio makubwa hilo naliona ndani ya Azam FC msimu ulioisha tulipambana tukamaliza nafasi ya pili, tulikuwa bora na tulitoa changamoto kwa wapinzani," anasema na kuongeza;
"Malengo ya msimu uliopita kwa namna moja yalitimia sasa tumeanza msimu mpya japo sio kwa ubora lakini bado tuna michezo mingine mingi ya kupambania ili tupate matokeo mazuri na kufikia malengo ya kutwaa mataji."
Anasema msimu ulioishja walikosa mataji yote mbele ya Yanga, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na FA hilo wamelisahau wanawekeza nguvu mpya msimu huu ili waweze kunyakua.

NAVARRO ANAHUSIKA
Ni wengi wanajiuliza kwanini mastaa kutoka Colombia wamekuwa wakiongezeka ndani ya kikosi cha Azam FC, Fuentes amefichua siri ya ongezeko lao Tanzania.
"Nilipata ofa kutoka kwa uongozi wa Azam FC ambao ulikuwa unanishawishi ili niweze kuungana na timu hii haikuwa rahisi kqwangu kujiunga moja kwa moja hadi hapo nilipowasiliana na mmoja wa wachezaji kutoka huku ambaye aliwahi kujiunga na timu hii," anasema na kuongeza;
"Mimi nimeshawishiwa na Franklin Navarro, baada ya kumwambia nimepokea ofa kutoka Azam FC alinishawishi kwa kuniambia mazingira ya timu yenyewe na kila kitu kilichopo sikuwa na namna nyingine yoyote ya kukataa," anasema Fuentes na kuongeza;
"Nipo sehemu sahihi sikufanya makosa kuja Azam FC mazingira yote niliyokuwa nasilimuliwa kwa njia ya simu nimekutana nayo kwani hapa kuna uwanja wa mazoezi, bwawa la kuongelea, vifaa vya mazoezi kila mchezaji anatamani kucheza timu yenye mazingira kama haya."
Anasema alikuwa amepata ofa nyingi lakini aliona mpango wa maendeleo ya klabu hiyo na yeye akiwa bado na umri mdogo anamini kwa maendeleo na mipango ya Azam FC ataweza kufikia malengo.

AZAM KUWA BORA
Kila mchezaji anakuwa na malengo binafsi lakini pia kwaajili ya timu anayoitumikia kama anavyothibitisha Fuentes kuwa amejiunga na Azam FC kwa lengo la kuongeza uzoefu binafsi sambamba na kuipambania timu hiyo kufikia malengo.
"Nimetoka Colombia kuja tanzania sio kushangaa nimekuja kupambana kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ubora ikiwa ni pamoja na kuona naipambania timu hii inakuwa bora sio Tanzania tu," anasema na kuongeza;
"Soka la Tanzania linakuwa na wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali wanatamani kuja kucheza nimepata nafasi natamani kupambana kwa kuhakikisha naifanya timu hii kuwa bora Barani Afrika kwa kushirikiana na wenzangu."
AITAJA YANGA
Miezi sita aliyocheza ndani ya kikosi cha Azam FC tayari amekutana na Yanga kwenye mechi mbili moja ya ligi na nyingine ilikuwa ngao ya Jamii, na fainali ya Kombe la Shirikisho ambayo ilifanyika Zanzibar ameitaja mechi hiyo kuwa ndio bora kwake.
"Yanga ndio timu nimekutana nayo mara nyingi zaidi kwenye mechi na ndio timu ambayo nimebahatika kukutana na wachezaji wengi wazuri ambao walinipa changamoto ya ushindani," anasema na kuongeza;
"Licha ya ugumu wote nilionyesha juhudi zangu kwa kupambana na kuhaikishia Azam FC kuwa hawakukosea kunipa mkataba wa kuitumikia kwani niliisaidia ikamaliza nafasi ya pili kwenye msimamo."
Fuentes anasema ubora wa wapinzani wao Yanga ulidhibitishwa kwa timu hiyo kutwaa mataji yote mawili ya ndani na ndio maana anakiri kuwa ndio timu ilikuwa bora msimu ulioisha.
Kwenye mechi tatu alizocheza Fuentes, Azam imeshinda mechi moja tu ya ligi kwa kuifunga Yanga mabao 2-1, walikubali kichapo cha 4-1 Ngao ya Jamii na walifungwa kwa penati kwenye mchezo wa fainali 6-5.

LUGHA SI ISHU
Wakati wadau wengi wa soka wakijiuliza ni lugha gani anatumia staa huyo kuwasiliana na wenzake hasa wanaocheza eneo la ulinzi mwenyewe amefunguka na kuweka wazi kuwa kuzungumza sio rahisi anafanya kwa vitendo.
"Soka sio mchezo wa kuzungumza sana sisi tunaelewana kwa vitendo naelewa lugha ninayozungumza sio rafiki kwa wenzangu japo kuna wengine tunaelewana lakini muda mwingi nimekuwa nikizungumza kwa vitendo," anasema Fuentes na kuongeza;
"Pia tunacheza wachezaji wa mataifa tofauti tofauti kama lugha ndio ingekuwa inatoa matokeo kwa kuzungumza basi timu nyingi zingekuwa zinapata wakati mgumu kwenye mawasiliano." Anasema.
FEI TOTO UTANI SANAA
Achana na ubora unaotajwa au kuonyeshwa na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' unaambiwa ndie mchezaji ambaye anazungumza na kila mtu kambini na mchekeshaji wao.
"Ni mtu mzuri sana amekuwa akiwasiliana na kila mmoja ukiondoa ubora wake uwanjani ni mtu wa utani ukikaa naye karibu basi utacheka muda wote," anasema na kuongeza;
"Kuhusiana na ubora wake hilo kila mmoja analiona kwani mpira ni mchezo wa wazi unapochezwa kila mmoja anaona nafurahi kucheza naye pamoja na anamchango mkubwa kikosini."