Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Foreman: Kutoka bondia hadi kuchoma nyama

Muktasari:

  • Lakini wakati huo huo amejikuta akikabiliana na pambano aliokuwa hana uzoefu nalo na ambalo linaweza kumharibia jina na maisha yake.

WAKATI wa ujana wake, George Foreman alipambana kwa ujasiri katika ndondi na kuacha historia ya kuvutia na sasa akiwa na miaka 75 akiwa anatumia muda mrefu kuhimiza upendo anapohutubia kanisani anaelezewa zaidi kwa hoteli zake zinavyochoma na kukaanga nyama kwa kutumia jiko liliopewa jina lake.

Lakini wakati huo huo amejikuta akikabiliana na pambano aliokuwa hana uzoefu nalo na ambalo linaweza kumharibia jina na maisha yake.

Nalo ni la kufunguliwa kesi na wanawake wawili wanaodai aliwabaka na kuwadhalilisha katikati ya miaka ya 1970 wakati alipokuwa akiwika kwenye ulingo wa masumbwi.

Wanawake hawa wawili ambao majina yao yamefichwa na kutajwa kama S. Denise na H. Gwen kila mmoja amefungua kesi yake akidai walibakwa na Foreman wakati wakiwa wasichana wadogo wenye kuvutia.

Wakati kesi hizi zikiwa zinaendelea, Foreman ambaye alipokuwa kijana alipenda sana kuendesha magari makali, siku nyingine magari manne tofauti kwa siku moja.

Kila aliposhinda pambano kubwa alinunua gari na hatimaye alikuwa na magari 69 ya aina mbalimbali. Sasa ameyauza 64 na kati ya hayo matano aliyoyabakisha ni aina ya Volkswagen Beetle ambayo ndio gari yake ya kwanza.

Kati ya magari aliyouza katika mnada alioufanya hapo kwake ambako yalikuwapo magari hayo ni aina ya Ford GT, BMW Z8, 1959 Chevrolet Impala, Ferrari Spider, Testarossa na 2015 Porsche 911 Turbo. Katika mnada huo alikusanya jumla ya dola za Kimarekani 1.587 milioni (karibu Sh3 bilioni).

“Nimesema mapenzi ya magari sasa basi, kwani mke wangu Jane niliyenaye kwa zaidi ya miaka 40 amechoshwa na kazi ya kuyatunza magari haya yaliyokuwa katika jengo la futi 16,000 za mradi katika nyumba yangu,” alisema Foreman.

George Foreman wa Marekani, mwenye asili ya Kiafrika alikuwa bingwa wa dunia wa ngumi za uzito wa juu kabla ya kustaafu na alirudi katika ndondi miaka 10 baadaye na kuwashangaza watu kwa vile alipigana kama vile alirudi katika ujana wake.

Miongoni mwa waliomsihi akiwa mzee wa kanisa kubadili uamuzi ni waumini wa kanisa lake, familia, marafiki na aliowahi kupigana nao.

“Masumbwi ni mchezo wa vijana...kizee usitutafute balaa. Pumzika kanisani. George tunakupenda na kama unatupenda usikaribie ulingo wa masumbwi,” liliandika gazeti la kwao Atlanta, Marekani.

Foreman aliporudi kupigana alikuwa na miaka 38 na baada ya wiki chache za mazoezi alikwenda California kupambana na Steve Zouski na kumchakaza kwa KO ya raundi ya nne.

Wengi walitegemea Foreman aliyekuwa na uzito wa ratili 270 na matatizo ya kunyanyua miguu, angelikung’utwa, lakini alishinda kibabe na kuendelea kushinda mapambano manne huku uzito wake ukipungua na kuzidi kuwa mwepesi kama kijana.

Katika mwaka 1988, akiwa na miaka 39, alishinda mapambano tisa na wapo waliosema alizaliwa upya. Kilichovutia ni ijapokuwa alipoteza madoido yake ya ujana, makonde yake yalikuwa mazito na hachoki.

Aliendelea na mazoezi, biashara na kuhubiri kanisani na kumtembelea rafiki yake Muhammad Ali aliyemsihi asipigane kwa vile ni mzee.

Baadaye alikutana na Gerry Cooney 1990 na kudhibitiwa, lakini katika raundi ya pili Foreman aliyekuwa na miaka 41 alishambulia kama simba aliyejeruhiwa na kumtoa nje Cooney.

Foreman alipanda chati ya wapiganaji wa uzito wa juu, kama ilivyokuwa kabla hajastaafu miaka 13 nyuma.

Katika mwaka 1991 alipambana na bingwa wa dunia, Evander Holyfield. Foreman, akiwa na miaka 42 na hakutarajiwa kuhimili makonde ya Holyfield aliyekuwa mdogo wake kwa miaka 17.

Pambano lilipoanza Foreman alijihami na mashabiki walimwambia: “Leo utapata unachokitafuta”. Baadaye alisukuma makonde ya uhakika, lakini pambano ilipomalizika Holyfield alitangazwa mshindi kwa pointi. Foreman alisema: “Nusu ya ndoto yangu ya kuonyesha hata ukiwa na miaka 40 unaweza kupigana raundi 12 imetimia. Naahidi mtashangaa zaidi”.

Baadaye alipambana na Alex Stewart, ambaye katika pambano lake la mwisho alitolewa na Mike Tyson. Foreman alimuangusha Stewart mara mbili raundi ya pili, lakini Stewart hakusalimu amri. Pambano lilikwenda hadi raundi ya 10 na Foreman alichapwa vibaya na uso kuloa damu. Watu wengi walimtaka astaafu, lakini alikataa na kusema alikuwa na deni kwa mashabiki na kilichobakia ni kutimiza nusu ya ndoto yake. Katika mwaka 1993 alikutana na mpiganaji chipukizi Tommy Morrison na Morrison alishinda kwa pointi. Marafiki zake walipomwambia jua limetua aliwaambia mambo bado na katika mwaka 1994 alitaka awanie ubingwa wa dunia aliouachia alipostaafu miaka 15 nyuma.

Mashirika ya kimataifa ya ndondi, IBF na WBA, yalipomkatalia alikwenda mahakamani na kudai alibaguliwa kwa sababu ya umri mkubwa. Alishinda na kupewa nafasi ya mwisho ya kupigania ubingwa wa dunia uliokuwa wazi. Nayo ni kurudiana na Morison Las Vegas, Nevada.

Moorer aliongoza na alimdhibiti Foreman, lakini mambo yaligeuka raundi ya 10 Foreman alipomtwanga Moorer konde la kulia kwenye kidevu kilichodata na kumwaga damu. Moorer alishindwa kuinuka.

Wengi hawakuamini Foreman kuuchukua tena ubingwa wa dunia na kuweka rekodi ya kuwa bingwa akiwa na miaka 45, mpiganaji mkongwe kushika wadhifa huo.

Siku chache baadaye alizungumzia kupambana na Mike Tyson, lakini WBA walimtaka apambane na Tony Tucker. Foreman alikataa na akavuliwa ubingwa.

Baadaye alipambana na Axel Schulz wa Ujerumani kuteteaa ubingwa wa IBF na alishinda. IBF ilipanga warudiane Ujerumani, lakini Foreman alikataa na kuvuliwa ubingwa.

Katika mwaka 1966, akiwa na miaka 46 na siku 169, alikwenda Tokyo na kumshinda chipukizi Crawford Grimsley. Mwaka uliofuata alipigana na Lou Savarese na kushinda na WBA walipomuona kiboko walimkutanisha na Shannon Briggs ili mshindi apambane na bingwa wa WBC, Lennox Lewis.

Foreman alipoteza kwa pointi, uamuzi uliotiliwa shaka kwa kuonekana Foreman angekuwa bingwa kwa mara ya tatu ndondi ingepoteza`ladha. Hii ilimfanya Foreman kustaafu.

Siku hizi anawafundisha ndondi vijana, hutangaza mashindano katika televisheni na anahubiri kanisani.

Alipokuwa kijana alitumia muda mwingi vituo vya polisi kwa kufanya fujo na alipewa kazi ya askari, lakini aliachishwa kutokana na kuwapiga wenzake.

Alipata umaarufu akiwa na miaka 19 alipochukua medali ya dhahabu ya Olimpiki ya 1968. Alianza ngumi za kulipwa 1969 na alipigana mara 13 na kushinda mapambano yote, mara 11 kwa KO.

Cookie Wallace alimalizwa katika sekunde ya 23 tu tangu pambano kuanza na 1973 alikutana na aliyekuwa bingwa, Joe Frazier na kumtoa katika raundi ya pili kwa kumsukumia zaidi ya makonde 10 mfululizo.

Kwa kutetea ubingwa alikwenda Venezuela 1974 kukutana na Ken Norton aliyemshinda Muhammad Ali kwa pointi.

Alikutana na Muhammad Ali kule Zaire (sasa DR Congo) 1974, ambako mashabiki wa Ali walikuwa wakiimba “Ali bomaye” wakimaanisha “Ali muue (Foreman)”. Ali alikwepa makombora kwa kwenda kwenye kamba na kuitumia kurudi ulingoni kwa kasi kumchapa Foreman ambaye ilipofika raundi ya sita alichoka.

Katika raundi ya nane Ali alimsakama Foreman kwa makonde mazito na mwamuzi kumtangaza Ali mshindi. Foreman alipumzika mwaka mzima na aliporudi alikuwa imara kama chuma. Sasa anafanya biashara za nyama za kuchoma zinazomtengenezea dola 150 milioni kwa mwaka, mara tatu ya fedha alizopata alipopigana.

Vile vile ni mshirika wa kampuni ya mashine za kuchoma nyama ziitwazo George Foreman, anauza nguo na anazo hisa katika kampuni za magari. Ana watoto 10, wanawake watano na wanaume watano. Watoto wote wa kiume wanaitwa George na mmoja wa kike, Freeda ni mpiganaji mashuhuri.