FIFA U17 ilivyoleta vyuma vilivyotikisa
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Khel Now hawa hapa ni mastaa watano walijitangaza kwa mara ya kwanza duniani kupitia mashindano ya soka ya vijana ya dunia, lakini baadaye wakaendelea kufanya vizuri kwa klabu na timu zao za taifa. Elewa kwamba, nyota hawa wameacha majina makubwa katika ulimwengu wa soka.
BERLIN, UJERUMANI: UNAPOANGALIA baadhi ya wachezaji waliowahi kuonyesha vipaji kwenye Kombe la Dunia, huwezi kuviweka kando vipaji vilivyoibukia katika nchi kadhaa kwenye mabara tofauti duniani.
Lakini, Kombe la Dunia la vijana chini umri wa miaka 17 limekuwa likiibuka na vyuma matata vinavyoutikisa ulimwengu wa soka. Kawaida, mashindano hayo ni kama jukwaa la kuibua nyota wa baadaye wa soka duniani, na vikosi vya timu 24 hujaa vipaji.
Kwa mujibu wa Khel Now hawa hapa ni mastaa watano walijitangaza kwa mara ya kwanza duniani kupitia mashindano ya soka ya vijana ya dunia, lakini baadaye wakaendelea kufanya vizuri kwa klabu na timu zao za taifa. Elewa kwamba, nyota hawa wameacha majina makubwa katika ulimwengu wa soka.
I. Alessandro Del Piero
Muitaliano huyu aliibukia katika fainali za Kombe la Dunia U-17 zilizofanyika 1991, lakini ni mshindi wa Kombe la Dunia 2006 akiichezea Italia ya wakubwa. Del Piero alizima vilivyo katika safu ya kiungo na ushambuliaji kwenye fainali za kombe hilo zilizofanyika kuanzia Juni 9 hadi Julai 9, 2006 huko Ujerumani.
Italia iliondoka na ubingwa wake wa nne wa michuano hiyo katika fainali iliyoikutanisha na Ufaransa, huku Ujerumani na Ureno zikimaliza nafasi ya tatu na nne mtawalia.
Katika muda mwingi wa maisha yake ya soka Del Piero aliichezea Juventus, na ilikuwa uti wa mgongo wa timu ya taifa ya Italia kwa miongo kadhaa. Klabu hiyo yenye mashabiki na wafuasi wengi maarufu kama Kibibi Kizee cha Turin, imeibua nyota wengi pia.
Wengi waliomfuatilia Del Piero wangesema alikuwa roho ya Juventus. Mshambuliaji huyo aliyeiacha klabu hiyo 2012, alionekana kwa mara ya kwanza katika fainali za U-17 akiwa na Italia, wakati mashindano yalipohamishwa kutoka Ecuador hadi Italia. Akiwa na umri wa miaka 16 na akichezea Padova, alifunga bao moja kati ya mabao mawili ya Italia walipoondoka kwenye hatua ya makundi.
Hali hiyo haikuwepo tena kwenye Kombe la Dunia 2006, kwani mshambuliaji huyo wa Juventus alikuwa sehemu ya kikosi chenye nguvu kilichoshinda taji mjini Berlin.
Kocha wa kikosi hicho, Marcello Lippi alitambua thamani ya Del Piero kikosini akamjumuisha, na licha ya kuwa hakuwahi kuwamo kwenye kikosi cha kwanza mara zote, lakini bao lake la pili alilofunga kwa utulivu katika nusu fainali dhidi ya Ujerumani huko Dortmund litabaki kwenye kumbukumbu za mashabiki wa Azzurri. Baadaye, alicheza Sydney FC (Australia) na Delhi Dynamos 2014 (India) kabla ya kustaafu.
2. Iker Casillas
Hakuna asiyekijua kizazi cha makipa bora wa miaka ya 1990 hadi 2010 walioitingisha Ulaya, kwani klabu kubwa zote zilitambia umahiri wao. Hizi ni pamoja na Manchester United, Arsenal, Chelsea (kwa England), Barcelona na Real Madrid (Hispania), Bayern Munich (Ujerumani), PSG, Marseille na Monaco (Ufaransa), Juventus, AC Milan na Inter Milan (Italia).
Katika milingoti mitatu ya goli la Real Madrid alikuwa kuwapo Iker Casillas, aliyeibukia katika fainali za Kombe la Dunia U17 mwaka 1997. Unapotaja jina la Casillas unazungumzia mshindi wa Euro 2008 na 2012 na Kombe la Dunia 2010 akiwa na timu ya taifa ya Hispania.
Casillas alikuwa roho ya Real Madrid, akiwa sehemu ya kikosi imara cha Hispania cha U-17 mwaka 1997 walipofika nusu fainali na kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ghana. La Roja walimaliza nafasi ya tatu, lakini waliibua hazina ya Casillas. Huyu alikuwa kipa wa namba moja kwa klabu na taifa kwa karibu muongo mmoja na nusu, akivutia mashabiki na wachezaji kwa ustadi wake, uongozi, na uelewa wa mchezo.
Hispania hatimaye ilitawala Euro 2008 chini ya kocha Luis Aragones na baadaye ikashinda Kombe la Dunia 2010 na Euro 2012. Licha ya kuondoka Real Madrid kinyonge, Casillas bado ndiye kipa pekee wa Madrista aliyeng’ara zaidi kuliko wote waliotangulia kwake na waliomfuatia baadaye.
3. Xavi Hernandez
Hili ni zao lingine la Hispania lililoibukia katika fainali za vijana chini ya miaka 17 mwaka 1997. Xavi Hernandez, mtaalamu wa chenga za maudhi na mhimili wa timu ya taifa ya Hispania pale katikati kwa miaka mingi.
Mchezaji huyo kama ilivyo kwa Casillas ni mshindi wa Euro 2008 na 2012 na Kombe la Dunia 2010 akiwa na Hispania. Xavi alikuwa moyo wa mafanikio ya Hispania katika kipindi cha miaka 14, licha ya kwamba alianzia katika vikosi vya chini alikodumu kwa miaka mitatu kuanzia kile cha chini ya miaka 17 hadi 23.
Kama alivyokuwa Casillas, mchezaji huyo alikuwa mbele ya mapinduzi ya soka la Hispania, Xavi akitajwa kuwa ubongo wa timu. Kiwango chake cha juu cha uhusiano na Andres Iniesta uwanjani kilichangia Hispania kushinda mataji matatu katika miaka minane. Alikuwa sehemu ya kikosi cha U-17 iliyomaliza nafasi ya tatu 1997, na baadaye akawa nyota wa Barcelona na Hispania, akishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu na La Liga mara nane. Xavi aliendelea kuwa muhimu hadi alipohama Barcelona 2015.
4. Toni Kroos
Kwa Wajerumani yapo majina mengi yanayokumbukwa wakati huu wakiikaribia fainali nyingine ya Kombe la Dunia inayofanyika Marekani, Canada na Mexico, miezi miwili na ushei ijayo. Lakini, kuna jina moja tu katika miaka ya 2000 lililotawala sana hasa ndani ya uwanja, nalo ni lile la kiungo Toni Kroos.
Achana na makipa wao kina Manuel Neur, Jens Lehmann na Oliver Kahn. Vilevile weka kando mastaa kama Thomas Muller, Bastian Schweinsteiger, Miroslav Klose na Mario Gomes, lakini Kroos ndilo jina linalokumbukwa zaidi kwa sasa.
Kroos aliibukia katika fainali za Kombe la Dunia U17 lililopigwa 2007, na ni mshindi wa Kombe la Dunia 2014.
Mchezaji huyo alithibitisha kuwa ndiye mchezaji bora wa kiungo duniani huko Brazil 2014.
Akiwa ‘barubaru’ aliiongoza timu ya Ujerumani U-17 katika fainali za vijana 2007 zilizopigwa Korea Kusini alikoshinda Tuzo ya mfungaji bora (Golden Ball) kwa mabao matano katika michezo saba wakimaliza nafasi ya tatu. Akiwa ni zao la akademi ya Bayern Munich baadaye alitua Leverkusen kwa mkopo wa muda mfupi kabla ya kuhamia Real Madrid na kuwa mmoja wa nguzo kuu za ushawishi katika soka la Hispania na Ulaya.
Katika Kombe la Dunia 2014, Ujerumani waliibuka mabingwa wakiishinda Argentina bao 1-0 mchezo uliopigwa katika Dimba la Maracana, Kroos akiwa mmoja wa wachezaji muhimu. Mwamba huyo pia amebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya matatu.
5. Ronaldinho
Unapozungumzia vipaji ilivyojaliwa dunia katika mchezo soka, huwezi kumuacha Ronaldo de Assis Moreira maarufu kama Ronaldhino Gaucho, mwamba wa Brazil aliyeibukia katika mashindano ya Kombe la Dunia U17. Mpaka alipohitimisha kazi yake uwanjani 2015, nyota huyo aliyezichezea timu za Barcelona, PSG na AC Milan huko Ulaya
aliondoka akiwa na bingwa wa fainali hizo za vijana na pia Kombe la Dunia 2002.
Kizazi chake ndicho kilichohitimisha ile Brazil ya samba ambayo ilizitesa timu mbalimbali duniani. Brazil ya Ronaldhinho ilidhibiti soka la dunia mwishoni mwa miaka ya 1990, na nyota huyo akiwa miongoni mwa mastaa vijana waliopandishwa timu ya wakubwa wakiwa tishio. Anakumbukwa kwa kufunga mabao mawili katika kampeni yao ya fainali za vijana U-17 nchini Misri.
Katika Kombe la Dunia 2002 lililopigwa Korea na Japan, Brazil waliibuka washindi wakiwa na safu kali ya ushambuliaji iliyoongozwa na Ronaldo, Rivaldo na Ronaldinho. Mwamba Ronaldinho alifunga bao la ajabu dhidi ya England kutokana na mpira wa free kick umbali wa futi 40. Baadaye alishinda Ballon d’Or na Ligi ya Mabingwa Ulaya 2005/2006 akiwa Barcelona, La Liga (2004–05 na 2005–06), Supercopa de Espana (2005, 2006).
Ronaldhinho aliondoka uwanjani akiwa na tuzo tofauti zaidi ya 30 kutoka katika timu, mashirikisho ya soka (katika timu za nchi alikocheza) pamoja na taasisi kubwa za kisoka na kijamii duniani.