Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fatuma: Yote haya sababu ya Kaseja

Muktasari:

  • Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza machache na kocha huyo aliyefanya vizuri na timu mbalimbali kuanzia zile za taifa na klabu, ambapo ameelezea mambo mengi huku akifunguka ujasiri wa kufanya kazi hiyo aliupata kupitia kwa kipa, Juma Kaseja.

NI nadra kuona makocha wa makipa wa kike katika timu za wanaume ila kwa Tanzania tumebarikiwa kumuona, Fatuma Omary wa JKT Tanzania anayetimiza vyema majukumu yake uwanjani, huku akijivunia kufanya kazi hiyo bila ya kuhofia jambo lolote.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza machache na kocha huyo aliyefanya vizuri na timu mbalimbali kuanzia zile za taifa na klabu, ambapo ameelezea mambo mengi huku akifunguka ujasiri wa kufanya kazi hiyo aliupata kupitia kwa kipa, Juma Kaseja.


KASEJA AMPA UJASIRI

Fatuma anamtaja aliyekuwa kipa wa Simba na Yanga, Juma Kaseja ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa Kagera Sugar, kuwa ndiye aliyemjengea ujasiri wa kufanya kazi na timu za wanaume, jambo ambalo anasema anamshukuru sana na kamwe hatamsahau. “Ujasiri wangu ambao wengi wanauona nimeupata kwa Kaseja kwa sababu ni mtu aliyeniondolea woga kwa mwanaume. Kiukweli najivunia yeye, ni msikivu na nawasiliana naye muda wowote huku stori zetu zikiwa ni za kazi tu,” anasema.


NIDHAMU MPANGO MZIMA

Anasema moja ya vitu vinavyomsaidia kufanya vizuri ni kujituma, kujitunza na kujiheshimu m, kwani kuwa navyo utafanikiwa popote. “Mimi napenda ninachokifanya ndio maana nipo hapa leo, mtu yeyote anaweza kufikia malengo aliyojiwekea endapo tu atakuwa na nidhamu na kujiheshimu kwa sababu hiyo ndio siri ya kufanikiwa, najivunia kazi ninayofanya na wala sijawahi kujutia.”

MAKOCHA KUTOTOKA NJE

Fatuma anasema, haamini sababu ya makocha wazawa kutotoka nje ya nchi ni kutokana na kutokuwa na uwezo isipokuwa nafasi. “Nchi imebarikiwa kuwa na makocha wengi na wakubwa lakini mijadala imekuwa mingi kuhusu kutotoka nje ya nchi kufundisha, watu wanapaswa kutambua sio suala la kutoka tu bali ni nafasi haijapatikana pia kwetu,” anasema.


AJIVUNIA RICHARD

Fatuma anajivunia uwepo wa kipa wa sasa wa JKT Tanzania, Denis Richard ambaye awali waliwahi kufanya kazi wote pamoja na KMC.

“Ni kipa mzuri na ninamfahamu kwa sababu nimefanya naye kazi kabla ya kukutana naye hapa JKT, sijampendekeza asajiliwe kama wengi wanavyosema ila nilimkuta hapa, anajua kutimiza majukumu yake vizuri uwanjani hivyo kiukweli binafsi najivunia.”


AWAASA WAZAZI

Anasema mpira kwa sasa ni ajira na ikiwa mzazi anaona mtoto wake ana uwezo wa kucheza na ana ndoto hizo amuache afanye. “Wengi wamenufaika na huu mchezo wa mpira kama ilivyokuwa mimi, nawaomba wazazi wawape sapoti watoto wao wenye ndoto za kucheza, hii itawasaidia sana kimaisha kwa sababu ni mojawapo ya ajira na inalipa ikiwa utaizingatia kwa kina,” anasema.


CHABRUMA AMKIMBIZA

Anasema wakati anaanza kucheza soka alikuwa ni mshambuliaji ila baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza ilibidi ahame nafasi na kucheza kipa huku mshindani alikuwa ni kocha mkuu wa JKT Queens, Ester Chabruma ‘Lunyamila’.

“Wakati nipo Sayari Queens nilikuwa nacheza mshambuliaji ila baada ya kusugua benchi kutokana na uwepo wa Ester Chabruma nilimuomba kocha wangu, Juma Bomba nihame nicheze kipa na kweli alinikubalia na kuanzia hapo nikawa na mwenendo mzuri.”


HAKUNA CHANGAMOTO

Fatuma anasema kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 hadi sasa alichofanya kazi hiyo, hajawahi kukutana na changamoto isiyo ya kawaida katika kazi yake ya soka. “Changamoto ni za kawaida tu ila siwezi kusema zimeniadhiri kwa chochote, wengi wamekuwa wananiuliza hivyo kwa sababu tu ya kufanya kazi na wanaume, niseme wazi kwangu najivunia na hakuna jambo lolote lililonikatisha tamaa kuanzia huko.”

NAJIAT AMKOSHA

Anasema, wapo makipa wengi na bora waliopita katika mikono yake na anajivunia wao ingawa kwa sasa ni kipa wa JKT Queens, Najiat Abbas. “Ni shujaa, shupavu na mbishi katika kazi, haogopi mwanaume zaidi ya kujali kile anachokifanya, naona kabisa anafuata nyayo zangu.”


SOKA LIMEMLIPA

Anasema kwa kiasi kikubwa mpira wa miguu umemlipa huku akieleza hataki kuelezea maisha yake binafsi japo anajivunia hapo alipo. “Nisingependa kuweka wazi kila kitu katika maisha yangu ila mashabiki wangu watambue kwamba nimesafiri sehemu nyingi za ndani na nje ya nchi na zimenifanya kufahamiana na watu wengi na wengine wananifahamu vizuri japo mimi siwafahamu.”


MAKIPA WAJITAMBUE

Fatuma anasema, licha ya Tanzania kutokuwa na vifaa vingi vyenye uwezo wa kuwasaidia makipa haina maana sio wazuri.

“Ni kweli changamoto hiyo ipo ila ninachojua hata ukiwa na kifaa kimoja unaweza kumfanya kipa akawa bora, kikubwa kwanza ni yeye mwenyewe kujitambua na kujua ana malengo gani aliyojiwekea, tunao makipa wazuri na wanafanya pia vizuri nchini.”