EXCLUSIVE: ISHU YA HARUNA NIYONZIMA NA SIMBA

Muktasari:

NYUMA ya pazia, katika maisha yake ya nje ya uwanja, kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima ni binadamu wa kipekee sana. Katika matamshi yake matano, neno Mungu halikosekani kinywani mwake, amekuwa mtu wa kushukuru kwa kila jambo linalotokea maishani yake.

NYUMA ya pazia, katika maisha yake ya nje ya uwanja, kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima ni binadamu wa kipekee sana. Katika matamshi yake matano, neno Mungu halikosekani kinywani mwake, amekuwa mtu wa kushukuru kwa kila jambo linalotokea maishani yake.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika nyumbani kwake Mikocheni B, Niyonzima anaonyesha uhalisia wa maisha yake nje ya kazi yake ya soka.

Kiungo huyo ni mkarimu, busara na subra ya kujibu maswali mepesi na magumu ili mradi kuepuka kuwakwaza wageni wake na kutoa ushirikiano mkubwa licha ya maswali mengine kuonekana kutokuwa tayari kuyajibu.

MOYO WAKE NI YANGA TU

Anasema Yanga ipo moyoni mwake kutokana na kuwa timu iliyomkaribisha kwa mara ya kwanza (2011) kucheza soka nchini hivyo anachukulia kama ni nyumbani.

“Ndio maana nachukulia Tanzania nyumbani kwa pili kama ilivyo Rwanda ndio maana nawekeza vitu mbalimbali vinavyosimamiwa na wake zangu kwasababu mimi sina muda wa kufanya hivyo,” anasema.

ISHU YA SIMBA

Anasema haukuwa uamuzi mwepesi kukubaliana na ofa ya Simba, kutokana na namna anavyoiheshimu Yanga, ila ilimbidi kutokana na soka kuwa kazi inayofanya aendeshe maisha yake.

“Kwa namna ambavyo naiheshimu Yanga mkataba wangu kwenda Simba, sikuusaini Tanzania, kwasababu sikuondoka Yanga kwa kuichoka ama kuichukia isipokuwa soka kwetu wachezaji ni kazi inayofanya tuendeshe maisha ndio maana tunaangalia maslahi;

“Najua kitendo hicho kiliwachukiza wengi na ndio maana wengine walichoma hadi jezi na sio kwamba nilikuwa nafurahia kuona hayo, isipokuwa nilijua waliumia na waliniona ni msaliti bila kujua kwamba ni kazi nafanya hivyo kwa ajili ya maisha ni kweli naipenda kazi yangu lakini kwa upande mwingine lazima vitu vingine viendelee,” anasema.

PRESHA ILIKUWA KUBWA

Anasema presha aliyoipitia wakati wa usajili wake kwenda Simba haitajirudia katika maisha yake na hatamani kuona mchezaji mwenzake anakumbana na hali hiyo, kutokana na namna ambavyo alikosa amani.

“Ilikuwa presha kubwa sana na ndio maana nilichelewa kujiunga na timu, nilikuwa nawaza nikitua kwenye ardhi ya Tanzania, mashabiki wa Yanga watanichukuliaje kwa namna nilivyokuwa naangalia yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, lakini kwa kuwa mpira ni kazi yangu nilimuomba Mungu anisaidie na alinisaidia;


“Ngoja niliweke vizuri hili ambalo watu wanadhani nilishindwa kuonyesha kiwango nikiwa Simba, nilikuwa na majeraha niliyotoka nayo Yanga na niliwaambia kabisa viongozi wa Simba jambo hilo, baadaye nilipokaa sawa nilicheza,” anasema.

Kiungo huyo anafichua siri ya kudumu kucheza soka la Tanzania, kwamba haimaanishi kuwa bora kuliko wengine, bali amemudu presha iliyopo na amejifunza kuishi utamaduni wa wenyeji wake.

“Mungu amenisaidia kufanya kazi zangu kwa nidhamu ya juu, siwezi kuacha kusema ukweli kwamba soka la Tanzania lina presha kubwa hasa Yanga na Simba, ambazo zimebeba ushindani halisi wa soka,” anasema.

KUREJEA YANGA

Anasema aliamua kurejea Yanga kwasababu akiwa Simba, alitamani kufanya hivyo ili kurejesha amani ya mashabiki wake wa Yanga, jambo analosema anamshukuru Mungu alilitimiza hata akija kuondoka ana amani ya moyo.

“Japokuwa watu wanaojua mpira waliniunga mkono na walinitia moyo nizidi kupambana, binafsi niliona ni hekima kurejea Yanga kwa ajili ya kutengeneza na wale ambao walikuwa na kinyongo, angalau kwa sehemu naona wapo sawa nashukuru Mungu,” anasema.

Nje na kutengeneza amani, anasema viongozi walimsajili upya kwasababu anaamini waliiona huduma yake inafaa, hivyo hakusita kukubaliana nao.

“Katika maisha yangu napenda kufanya kazi kwa bidii mtu anaponipa pesa yake, sipendi kula pesa ya mtu bure na soka nalipenda kwasababu Mungu kanipa kipaji hicho, hivyo lazima nikiheshimu,” anasema.

MIAKA NANE VPL

Huu ni mwaka wa tisa anacheza Ligi Kuu Bara, anaielezea kwamba ina ushindani na ni kati ya ligi bora Afrika Mashariki na Kati, huku akishuhudia jinsi alivyoviona vipaji vikubwa.

“Ligi hii ina ushindani mkubwa, kuna vipaji vya hali ya juu wachezaji wengi wanajua mpira, maana kuna tofauti ya kucheza mpira na kujua mpira, wengi wanaujua mpira, labda ninachoweza kuwashauri waamue kwenda kujaribu maisha nje na mipaka ya nchi yao.

Niyonzima akiwa na waandishi wa Mwanaspoti, Clezencia Tryphone (kushoto) na Olipa Assa (kulia) nyumbani kwake Mikocheni B, Dar.

Mfano wapo wengi wameamua kutoka kama Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Chilunda, Himid Mao na wanafanya makubwa nchi nyingine, nadhani waache malengo ya kucheza Simba na Yanga kuona ndio mwisho wao, hata mimi nimecheza timu zote kubwa Rwanda APR na Rayon Sports lakini niliamua kuja kutafuta changamoto mpya;

“Tageti yangu ilikuwa kwenda nje ya Afrika, lakini maneno mazuri ya Abdallah Bin Kleb nilipata ushawishi wa kuja kuichezea Yanga, yule ni zaidi ya kiongozi namchukulia kama mzazi ama kaka yangu hadi kesho tunaheshimiana,” anasema.

Anasema ndani ya miaka nane, anaifurahia zaidi miaka sita ambayo alicheza Yanga kwa mafanikio ya hali ya juu ambapo alichukua mataji ya Ligi Kuu Bara mwaka 2011, 2013, 2015, 2016 na 17 na kuhamia Simba.

“Furaha yangu ni kuona nimecheza Yanga kwa miaka sita mfululizo, huku nikiisaidia kuipa timu yangu mataji ya Ligi Kuu, Kagame, Mapinduzi na ASFC na tulikuwa tunafanya vyema michuano ya Caf,” anasema.

Pamoja na kuipa Yanga mafanikio makubwa, Simba nako ameacha alama ya kuchukua taji la Ligi Kuu mara mbili mfululizo na ASFC, ambavyo vitabakia kwenye kumbukumbu ya maisha yake ya soka.

FILAMU, MUZIKI

Mbali na soka Niyonzima amecheza filamu ya ‘The Ring’ anaweka wazi kwamba ni kazi anayoipenda na ataendelea kuifanya kadri atakavyopata muda.

“Filamu hiyo imebeba uhalisia wa wanaume wengi kama watu watapata muda wa kuifuatilia kwa umakini itawafunza, bado haijaisha tutaendelea kuirekodi, pia ninaimba muziki naingia studio narekodi na nimewahi kufanya kolabo na mwanamuziki wa Rwanda anaitwa Jay Pole wa Hip Hop;

“Pia kuna nyimbo ambayo nimeitoa mwenyewe nimemuimbia mama yangu mzazi ambaye nimekaa naye kwa muda mrefu baada ya baba yangu kufariki dunia miaka mingi, hiyo nyimbo inaelezea mapenzi yangu kwake kwa namna ambavyo ametulea, kwani kwetu tumezaliwa 12, wanaume wanne wote tunacheza mpira na wanawake wanane, mimi ni wa nane kuzaliwa,” anasema.

ANAONGEA LUGHA SITA

Anasema anazungumza lugha sita zinazomsaidia kwenye mambo mbalimbali ambazo ni Kifaransa, Kiingereza, Kiswahili, Kilingala, Kiganda na Kirwanda na kwamba anaendelea kujifunza nyingine.

“Nina mpango wa kufanya vitu mbalimbali baada ya kustaafu soka ndipo itajulikana faida ya kuzungumza lugha mbalimbali ninazozizungumza kwasasa na nyingine nikiendelea kujifunza, labda kitu wasichokijua watu napenda kufanya vitu tofauti ipo siku vitaonekana kwa matendo,” anasema.

SIO STAA

Niyonzima anapenda kuishi maisha ya kawaida yenye uhuru ingawa anakiri kuna wakati mwingine anajikuta analazimika kuvaa kofia ili akifika sehemu aondoe ‘atensheni’ ya watu kumkusanyia kijiji.

“Kiukweli sipendi kuishi maisha ya kuigiza, wao ndio wananiona staa, lakini najikuta inaniwia vigumu hata nikitoka na familia najikuta watu wanajikusanya ndio maana nalazimika kuvaa kofia ili wasinijue kirahisi, ila sio maisha ninayopenda kuyaishi kwani binadamu wote tupo sawa tumetofautiana kazi,” anasema Niyonzima.

MKE WA PILI

Kuna kipindi picha za harusi yake zilivuja na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, analizungumzia hilo kwamba ameoa mke wa pili ambaye ni Mrwanda mwenzake isipokuwa alifungia ndoa hapa nchini.

“Mke wangu mkubwa anajua nimeoa sema niliamua kukaa kimya baada ya kila mtu kuzitafsiri kama anavyopenda zile picha na sio kila kitu cha kujibizana mitandaoni, niliona kunyamaza ni busara zaidi ili mradi nimezingatia dini yangu inasema nini, kwani nina hofu ya Mungu,” anasema.

NI KOCHA

Ni mchezaji anayejipambanua kufikiri nje ya boksi, kwani licha ya kuendelea kucheza lakini amejiongeza kwa kusomea ukocha sasa ana Leseni C na anaisaka Leseni B.

“Nina malengo ya kufanya vitu tofauti maishani hapo baadaye, ndio maana nimesoma ukocha nina leseni C, nataka kuisomea B, miaka ijayo Mungu akitujalia uzima ninayoyaongea yataonekana kwa matendo ndipo watanielewa,” anasema.

NAHODHA TIMU ZA TAIFA

Amekuwa nahodha wa timu za taifa za Rwanda (U-17, U-20 na ya wakubwa, Amavubi) na kwamba anaheshimu sana kitambaa hicho.

“Nimebahatika kuwa nahodha wa timu zangu za taifa, hilo ni kutokana na kutanguliza nidhamu ndani na nje ya uwanja, nimekuwa muumini wa kuwahi kazini kwangu kwani natambua kwamba ndio kazi inayofanya nitunze familia yangu,” anasema.

KAGERE WA AINA GANI

Anatufichulia jinsi alivyo straika wa Simba, Meddie Kagere ambaye ni Mnyarwanda mwenzake kwamba ukiacha upambanaji wake ni mcheshi ambaye kama una matatizo unaweza ukayasahau kwa muda.

“Kagere ni kaka yangu, pia tunacheza timu moja ya taifa ya Rwanda licha ya kuwa nahodha wake tunaheshimiana, kwanza napenda upambanaji wake jinsi anavyojituma kufanya kazi zake, nje na hapo ni mcheshi sana ukikaa naye unaweza ukawa unacheka kila wakati tofauti na wanavyomchukulia,” anasema.