ERIK WEIHENMAYER: Mlemavu wa macho aliyeweka rekodi ya dunia
Muktasari:
- Mlima huu uliopo katika milima ya Himalaya katika mpaka wa Nepal na jimbo la Tibet la China una urefu wa futi 29,031.7.
MWANZONI mwa Juni, 2001 vyombo vingi vya habari katika medani ya michezo vilijadili kile kilichoonekana kama maajabu ya mtu asiyeoona kabisa, Erik Weihenmayer wa Marekani kuwa mtu wa kwanza asiyeona kupanda hadi kileleni mwa mlima mrefu kabisa duniani wa Evarest.
Mlima huu uliopo katika milima ya Himalaya katika mpaka wa Nepal na jimbo la Tibet la China una urefu wa futi 29,031.7.
Mlima wa Kilimanjaro ambao ndio mrefu kabisa barani Afrika una urefu wa futi 19,341).
Kwangu hayakuwa maajabu na nilimkumbuka mwalimu wangu mmoja nilipokuwa Shule ya Msingi miaka ya 1950. Alituambia mafunzo makubwa ya maisha na dunia mtayakuta mkianza maisha nje ya shule na mengine mtayaona kama miujiza.
Kumbukumbu ya huyu mwalimu ilinijia nilipoanza kuwa karibu na watu wenye ulemavu na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Ulemavu Zanzibar.
Kwa kukaa na kufanya kazi nao pamoja niliona mengi ambayo kama hujayaona utasema ni hekaya ya kufurahisha baraza.
Kwa mfano alikuwepo jamaa mmoja wa kiume akiitwa Kali aliyekuwa haoni kabisa. Alifanya kazi kwanza kama mwogozaji simu (opereta) kwa njia ile iliyokuwa na laini 20 hadi 30 katika sanduku katika Ofisi ya Idara ya Majenzi.
Pia alikuwa anasomesha chuo (madrasa), fundi wa saa, umeme na vyombo vya moto kama charahani, pasi na mashine za kusagia nyama au matunda.
Mwingine ni mwanamama Zuleikha alikuwa Mbunge wa Tanzania kwa tiketi ya viti maalum kwa watu wenye ulemavu kutoka mwaka 2000 hadi 2005.
Huyu aliweza kumtambua mtu kwa mwendo au harufu, alikuwa mpishi mzuri na siku moja alinishangaza pale alipoweza kuzitambua noti za dola ya Kimarekani, Rupia ya India, Riyal ya Omani, Dirham ya nchi za Ghuna na za Kenya na thamani yake kwa kuzigusa tu.
Hata nilipokwenda Marekani 1986 nilikutana na Wilma Ralph aliyekuwa na ulemavu wa miguu na kutumia magongo hakuwa mdogo, lakini akaja kuwa bingwa wa dunia wa mbio za mita 100 katika michezo ya 1960 ya Olimpiki iliyofanyika Rome, Italia.
Sasa nizungumzie hayo utayaona kama maajabu ya Erik Weihenmayer ambaye licha ya kukosa nuru ya macho ameonyesha ulimwengu mambo makubwa.
Erik ambaye sasa ana miaka 57 amepata umaarufu kama mtunzi wa vitabu, mwanaharakati, alizaliwa Septemba 23, 1968 ni mwanariadha wa Marekani mwenye kuvutia wasikilizaji na mwanamichezo anayependa michezo yenye sulubu kama kupanda milima.
Alipoupanda Mlima Everest wakati ule alikuwa mmoja wa watu 150 waliokuwa wamepata mafanikio hayo, lakini ndio mtu wa kwanza ambaye haoni kuweza kufanya hivyo. Ilimchukua siku 38 kuifanya safari hiyo.
Kabla ya kufanya safari ya kwenda kuupanda Mlima Everest, Erik alikuwa ameshapanda milima midogo midogo katika nchi mbalimbali.
Erik alianza kupoteza nuru ya macho akiwa na miaka 13 na baada ya miaka mitatu akawa haoni kabisa, lakini alipojikuta katika hali hiyo alikuwa akisema kukosa nuru ya macho sio kutoona njia ya mafanikio.
Kti ya michezo aliyoipenda tungu mdogo na kuendelea nayo hadi alipokaribia umri wa miaka 50 ni kupigana mieleka.
Alipoacha kucheza mieleka alikuwa mwalimu wa mchezo huo katika jiji la Phoenix, Marekani.
Erik ameandika vitabu vingi na kati ya vilivyokuwa maarufu ni Touch the Top of the World: A Blind Man’s Journey to Climb Farther Than the Eye Can See (Gusa eneo lilio juu kabisa la dunia: Safari ya kufikia pale ambapo nuru ya macho haioni).
Kitabu hiki kinachovutia kila ukurasa kimechapwa katika lugha mbalimbali katika nchi saba. Vile vile kimetenegenezewa filamu yake. Erik amepata tuzo katika nchi mbali mbali kwa ujasiri wake na kuwa mfano wa kuwahamasisha watu wenye ulemavu kutokata tamaa ya maisha.
Katika mwaka 2023 Erik alikuwa mmoja wa watu walioshiriki kutengeneza mchezo wa sinema uitwao Maisha ni Kupanda Mlima.
Ninaamini maelezo ya maisha kuonyesha filamu za michezo ya watu kama Erik na wengine wengi wa aina yake waliyofanya makubwa hapa nchini na nje yanaweza kusaidia sana kuwashajiisha watu wenye ulemavu, hasa watoto, kujiamini na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini. Simulizi hizi ni vizuri kuzungumziwa katika shule na kupewa kipaumbele katika vyombo vya habari ili viwape uelewa mzuri watu wenye ulemavu kwamba kuwa na ulemavu sio kikwazo kikubwa cha maisha.