Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dube: Upepo umegeuka, mjipange vizuri

Muktasari:

  • Ile kauli ya usimkatie mtu tamaa ndio imetokea kwa Dube baada ya kusota kwa muda mrefu hadi kuanza  kufunga mabao kuanzia mchezo wa TP Mazembe uliopigwa Lubumbashi, DR Congo ulioipa Yanga pointi muhimu kwenye Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika.

MAISHA yanabadilika haraka sana pale Yanga, kwani wiki chache zilizopita ilikuwa ukiwatajia mashabiki wa timu hiyo jina la mshambuliaji Prince Dube ni kama unawaumiza mioyoni. Wengi walishindwa kuelewa kipi kilimkumba Mzimbabwe huyo.

Ile kauli ya usimkatie mtu tamaa ndio imetokea kwa Dube baada ya kusota kwa muda mrefu hadi kuanza  kufunga mabao kuanzia mchezo wa TP Mazembe uliopigwa Lubumbashi, DR Congo ulioipa Yanga pointi muhimu kwenye Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hivi sasa raha ndani ya Yanga imerudi, lakini kama kuna kitu kinawapa furaha zaidi mashabiki wa timu hiyo, basi ni kuona inashinda kisha Dube anapofunga.

Nyuso za tabasamu za mashabiki wa Yanga na Dube zinaonekana, jambo linaloashiria kwamba mshambuliaji huyo baada ya kuwa kwenye shimo la mateso sasa amebadili upepo.


UKAME WA MABAO

Baada ya kuanza kufunga mwanzoni kwenye mechi za mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hata mechi za Ngao ya Jamii alipotoa asisti na kufunga, ghafla mambo yalibadilika kwa Dube akikutana na ukame wa kufunga kwenye ligi.

Nyota huyo alicheza mechi 11 za ligi bila kufunga bao, ongeza na mechi tatu za Ligi ya Mabingwa zikiwemo mbili za makundi na moja ya mtoano.

Ukame huo ulikuwa unawapa wakati mgumu mashabiki kujiuliza kipi kimemkumba mshambuliaji huyo aliyesajiliwa akitokea Azam ambako alionekana  anakuja kufanya makubwa eneo la ushambuliaji.


JUHUDI ZAKE

Kitu cha pili kilichowaumiza mashabiki ni namna Dube licha ya ukame huo, lakini hakuchoka kujitafuta kwani aliendelea kupigania nafasi huku makocha wakimpa nafasi kwenye mechi.

Huko mazoezini, wakati Dube akikumbana na ukame wa kufunga kwenye mechi, hali ilikuwa tofauti akiwa katika maandalizi kwani alikuwa akifunga kama kawaida hali ambayo iliwafanya makocha wake kuendelea kumwamini wakimpa nafasi.

MABAO YAMERUDI

Safari ya ubora wa Dube ilianzia Lubumbashi dhidi ya TP Mazembe alipoanza kurudisha mabao, akiifungia Yanga bao katika sare ya 1-1 na mabingwa hao wa soka Tanzania kuvuna pointi ya kwanza kwa bao la straika huyo alilofunga dakika za mwishooni.

Baada ya bao hilo Dube ni kama amezaliwa upya ambapo mechi nne zilizopita za ligi alifunga mabao matano ikiwemo hat trick Yanga ikishinda 3-2 dhidi ya Mashujaa.

Hat trick hiyo ni ya kwanza katika ligi msimu huu.Mchezo uliofuata dhidi ya Tanzania Prisons, Yanga ilishinda 4-0 na Dube akafunga bao moja,  akiendeleza moto huo tena dhidi ya Dodoma Jiji Yanga iliposhinda 4-0, lakini akaondoka bila bao mbele ya Fountain Gate wakati Yanga ikishinda 5-0.


TABASAMU LIMEREJEA

Mabao hayo yamerudisha tabasamu la mashabiki wa Yanga majukwaani na sasa wamekuwa na kiu ya kuona mabao ya mshambuliaji huyo ambapo kila akifunga wimbo wao unakuwa mmoja tu ‘Dube...Dube...Dube...Dube’ wakifurahia ushindi wake.

Wakati Yanga ikitengeneza mashambulizi mashabiki wamekuwa wakihanikiza wenzake kumpasia Dube ili aendelee kufunga, ambapo hali hiyo ilikuwapo pia msimu uliopita walipokuwa wanataka kiungo Stephanie Aziz KI apewe nafasi kufunga ili awe mfungaji bora, na akafanikiwa.


USHIRIKIANO    NA WENZAKE

Tazama namna Dube alivyo na ushirikiano na wenzake kwenye safu ya ushambuliaji, ambapo amekuwa anatoa nafasi kwa wenzake kama Clement Mzize kufunga na yeye kupewa asisti.

Beki na nahodha wa Yanga, Dickson Job aliwahi kusema kitendo cha straika huyo kuanza kufunga kimewakosha kwa kuwa wanaamini ni mchezaji mzuri mwenye ushirikiano na kila mmoja.


MTEGO NI HUU

Kitu kinachotakiwa kufanyika sasa ambacho ni kama mtego wa Dube ni kama ataendelea kufunga zaidi kwa kuwa tayari hali ya kujiamini imesharejea akiwa ameshafunga mabao matano.


MSIKIE RAMOVIC

Dube aliyeanza kufunga kwenye ligi akiwa chini ya kocha Sead Ramovic akimzungumzia mshambuliaji huyo anasema anafurahishwa na mwendelezo wa mshambuliaji huyo namna anavyojituma na hata kufunga kwenye kikosi hicho akisisitiza anapaswa kujituma zaidi.