Deus Kazoka kutoka Ligi ya Championship hadi Uarabuni

HATA mwenyewe haamini zali alilokutana nalo lililomweka katika orodha ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi akiwa hajatokea klabu kubwa tena akiwa ni kipa.

Huyu kipa wa zamani wa Pamba Jiji na TSC Academy, Deus Kazoka akiwa ni mmoja wa nyota wanaocheza soka la kulipwa akikipiga Al Hilal United ya Umoja ya Falme za Kiarabu (UAE) kwa kandarasi ya mwaka mmoja.

Kazoka ambaye ni mwenyeji wa Mwanza alizungumza na Mwanaspoti hivi karibuni na kuweka bayana safari yake ya kutoka timu ya Ligi ya Championship hadi Uarabuni kupeperusha bendera ya Tanzania akisimulia pia changamoro anazokutana nazo huko na mikakati aliyonayo.


SAFARI YA AL HILAL

Kazoka anasema mchongo wa kwenda Umangani alipewa na Said Khamis, nyota wa zamani wa Mbao FC kabla ya kutimkia Uarabuni anakoishi, na akiwa huko alisikia kwamba timu hiyo inahitaji kipa.

“Aliniambia nami nikawaambia mabosi wangu wa timu ya Rock Solution ambao waliniruhusu kuja Falme za Kiarabu kujiunga na timu hii iliyonipa mkataba wa mwaka mmoja,” anasema Kazoka.

“Hadi sasa nimefanikiwa kuchezea timu tatu kwetu Tanzania ambazo ni TSC Academy ya Mwanza, Pamba FC kwa sasa Pamba Jiji inashiriki Championship na Rock Solution ambayo iko Ligi ya Mkoa.”

Hata hivyo, jambo la kushangaza kwa mchezaji huyo ni kwamba hana wakala hadi sasa, bali ana timu ya wasimamizi ambao kazi yao kubwa ni kusoma mikataba anayoingia na klabu na kumshauri.

“Nilipofika hapa maisha yalikuwa magumu sana. Kama unavyojua hali ya hewa ya Tanzania maeneo mengi joto ni la kawaida ukiacha Dar es Salaam, lakini baada ya kuja huku hali ilikuwa mbaya kwani kuna joto kali kitu ambacho sikukizoea awali na siku ya kwanza ya mazoezi nusura nishindwe maana joto lilikuwa kali,” anasema mchezaji huyo.

“Mazoezi yalikuwa magumu lakini nashukuru nilijikaza nikamaliza salama.”€


KABLA YA MKATABA

Anasema alipofika hakufikia kutia saini moja kwa moja mkataba, bali jamaa walitaka afanye majaribio kabla ya kumwaga wino. “Ni kweli wakati nafika sikusajiliwa moja kwa moja, bali nilifanya majaribio ambayo yalikuwa magumu. Nilifanya mazoezi baadaye nikacheza michezo zaidi ya mitatu na kwenye michezo hiyo nilijiapiza kujituma na kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu, baadae nikafanikiwa kupewa mkataba,”  anasema Kazoka.

“Tangu nimesajiliwa hapa Al Hilal United nimecheza mchezo mmoja wa ligi hadi sasa nikiwa kikosi cha kwanza na kabla nilicheza michezo sita ya kirafiki.Tangu nije nimecheza michezo saba.”


BONGO NA UARABUNI

Akizungumzia maisha ya Tanzania na Uarabuani, nyota huyo anasema kuna tofauti kubwa kwa ligi, kwani maandalizi ya mechi yanakuwa tofauti, viwanja vinavyotumika na mambo mengine.

“Huko Bogo tunachukulia vitu vya kawaida tofauti na huku maandalizi ya timu ndio msingi wa kupata matokeo bora,” anasema

“Kama hatuna mazoezi jioni au usiku nikiamka mapema asubuhi nafanya mazoezi ya tumbo, kisha nakunywa chai baada ya hapo napumzika kwa muda mrefu, kisha kuanzia majira ya saa moja usiku naingia kufanya mazoezi binafsi siku yangu inakua imekwisha.”€

Kuhusu ishu za ushirikina katika soka kipa huyo mwenye umri wa miaka 26 anasema imani hizo hazipo.

“Huku hawaamini hata kidogo imani hizo wenyewe wanaamini kila kitu kinatoka kwa Mungu kwani kila kiwanja huku kina msikiti kwa ajili ya watu kuswali wakati wote kwa vile waumini wengi ni Waislamu. Viongozi pamoja na wachezaji wanaamini katika dini na wanapewa muda wa kutosha kusali,” anasema na Kazoka.

Akizungumzia imani hiz katika mazingira ya ligi za hapa nchini, Kazoka anasema: “Sijawahi kwenda kushiriki ushirikina ili nicheze kwenye maisha yangu ya soka badala yake huwa ninakwenda kanisani kumuomba Mungu anipe nguvu za kuhakikisha natimiza ndoto zangu za kucheza soka la kulipwa na nimefanikiwa.”

Anasema uchawi wa soka ni uwekezaji, maandalizi mazuri ikiwamo usajili wa maana na kufanya mazoezi pamoja na kujituma kwa wachezaji na sio imani za kilozi zinazochangia kuharibu picha nzuri ya mchezo na klabu au wachezaji wanaoendekeza imani hizo.

“Kama uchawi unalipa katika soka au michezo mingine, ile mikoa na nchi inayotajwa kuwa mahiri kwa mambo hayo zingekuwa zikitamba kwa kubeba mataji kibao, lakini kwa vile soka ni sayansi mambo yamekuwa kinyume na wanaoamini mambo hayo waachane nayo hayasaidii.”


CHANGAMOTO

Kazoka anasema kama kuna vitu vilivyomkata stimu mwanzoni ni majaribio makali kutokana na hali ya hewa, lakini lugha ya mawasiliano nayo japo alikabiliana navyo na sasa anaona freshi tu.

“Siku yangu ya kwanza ya majaribio ndio sitaisahau maana ilikuwa ngumu kwani mazoezi yalikuwa magumu mno na sijawahi kuyapata kokote. Kutokana na ugumu uliokuwepo nilitamani niache kucheza nirudi zangu nyumbani lakini nilipokumbuka ugumu wa maisha niliouacha katika familia nilipambana hadi nikafanikiwa kupita,” anasema.

“ Huku kiukweli wanatumia Kiarabu, lakini nashukuru Mungu kwamba kuna wakalimani pia wanaozungumza Kiingereza, hivyo binafsi nawasiliana na wenzangu kwa kutumia lugha hiyo na kuendelea na maisha kama kawaida, japo wakalimani wakiwa mbali inakuwa mtihani kwangu.”


KUTOBOA KIMATAIFA

Akizungumzia namna ambavyo mchezaji anaweza kutoboa, Kazoka anasema: “Asikwambie mtu kufanikiwa kucheza soka nje ya Tanzania ni ngumu sana na lazima uwe na mtu ambaye atakushika mkono upite ufanye nini ndio uweze kutoboa. Kukaa mbali na nyumbani ina ugumu mkubwa inatakiwa ujitolee na bila kupata msimamizi mzuri ni ngumu kutoboa.

“Ni kweli maisha yangu yamebadilika sana tangu nije huku, maana nimejuana na watu wengi. Nimejua vitu vingi tangu nifike huku na hata maisha kiuchumi yamebadilika kiukweli, hivyo namshukuru Mungu kwa kila jambo.”