Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DENZEL: Kiba kanikutanisha na Jakaya Kikwete

Muktasari:

  • Denzel anasema nyota wa muziki wa Bongofleva, Ali Kiba ni mmoja wa mastaa aliobahatika kuwapigisha tizi na kuwapa maujuzi ya namna ya kuboresha viwango vyao kimwili kupitia mazoezi, lakini kupitia kwake akabamba dili la kuwa mkufunzi wa mazoezi wa Rais mstaafu Jakata Kikwete.

ILIPOISHIA, jana katika mahojiano maalumu na mkufunzi wa mazoezi ya viungo katika gym, Godfrey Mkinga  maarufu kanma Denzel Trainer alizungumzia namna alivyowarejeshea kasi uwanjani mastaa wa Yanga, Clatous Chama na Pacome Zouzoua pamoja na Mohammed Hussein 'Tshabalala' wa Simba, lakini leo anagusia alivyokutana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye amemuajiri, ratiba za mazoezi yake na mengi mengineyo... TWENDE PAMOJA


KIBA AMKUTANISHA NA JK

Denzel anasema nyota wa muziki wa Bongofleva, Ali Kiba ni mmoja wa mastaa aliobahatika kuwapigisha tizi na kuwapa maujuzi ya namna ya kuboresha viwango vyao kimwili kupitia mazoezi, lakini kupitia kwake akabamba dili la kuwa mkufunzi wa mazoezi wa Rais mstaafu Jakata Kikwete.

"Sikukutana kwanza na Rais Kikwete, nilitangulia kukutana na Ally Kiba ambaye ndiye aliyekwenda kunikutanisha na Rais Kikwete, na Kiba nilimtafuta sana hapa nchini ikashindikana. Kuna wakati nikaambiwa anakwenda Afrika Kusini huko ndio naweza kupata nafasi ya kuonana naye," anasema Denzel.

"Kweli nikasafiri mpaka Afrika Kusini na kufanikiwa kuonana naye nikampa wazo langu akakubaliana nalo na hapo ndipo tukaanza safari ya kumpa mazoezi. Baadaye ndiyo Kiba sasa akanikutanisha na Rais Kikwete akimuelezea nilivyompa ubora wa mwili wake kupitia mazoezi na kuanzia hapo naye akafurahia wazo hilo na kuanza kumpa mazoezi na hata kuajiriwa mbele yake (Kiba)."

Anasema kwa sasa ni mwalimu wa mazoezi wa kiongozi huyo mstaafu na familia yake.

"Sitapenda kuongelea sana kwa undani juu ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, lakini kikubwa naweza kusema kwamba huyu ndiye ameniajiri kumpa mazoezi pamoja na familia yake. Mbali na kuwafundisha watu wengine, lakini nimeajiriwa kwake," anasema.

"Unapoajiriwa na mtu kama mstaafu Kikwete huwezi kuajiriwa na mtu mwingine, lakini ninachoweza kufanya ni kuwa mwalimu wa wengine kwa muda wa ziada kama ambavyo nafanya."

Mkufunzi huyo anasema pamoja na mambo mengine aliyofurahishwa nayo katika maisha, lakini kufanikiwa kukutana na Rais huyo mstaafu na kuaminiwa kuwa mwalimu wake wa mazoezi ni jambo kubwa kwake.

"Kitu ambacho kimewahi kunivutia zaidi ni kukutana na Rais Kikwete na familia yake kwa ujumla. Rais Kikwete kama mnavyomuona wakati wote ana tabasamu, ni mtu mcheshi sana," anasema Denzel.

"Anapenda sisi tuliokuwa chini tuinuke kimaisha, ana upendo kwa watu wa rika zote, anapenda kutumia muda mwingi kutukumbusha kuishi kwa nidhamu na kutomdharau mtu yeyote bila kujali nafasi uliyo nayo, haya ni mambo nimejifunza sana kwa Rais Kikwete na familia yake.

"Na sio Rais Kikwete tu hata mkewe naye anaishi maisha hayohayo ya upendo. Nakumbuka moja ya kauli anayopenda kunikumbusha ni kwamba nisiizoee kazi yangu, nisifanye kazi kwa mazoea. Utaona uzito wa haya maneno kwenye maisha yetu hasa sisi vijana.

"Namshukuru Mungu kazi hii imenipa manufaa makubwa. Cha kwanza ambacho naweza kukitaja mapema ni kuwa mkufunzi wa Rais mstaafu Kikwete, mkewe Mama Salma na familia yake. Ni kitu ambacho sikuwahi kukiota hapo kabla."


RATIBA YA MAZOEZI IKOJE?

Denzel anasema katika kazi yake kuna ratiba na mpangilio wa mambo yanayohusiana na hilo.

"Unajua siyo kwamba siku nzima unatakiwa ufanye mazoezi. Mazoezi unaweza kufanya mara moja tu kwa siku. Hapo utachagua wewe ni asubuhi, mchana au jioni kulingana na muda wako," anasema.

Kuhusu idadi ya watu anaowapigisha tizi, mkufunzi huyo anasema: "Inategemea. Unajua nina wanafunzi wengi naweza kufundisha siyo chini ya watu 10 kwa siku. Wapo wengine wa makundi ya watu wengi. Kwa hiyo inategemea."

Mwanaspoti lilipofika nyumbani kwa Denzel lililazimika kumsubiri kwani kuwa kwake mwalimu wa mazoezi ana wanafunzi mpaka nje ya nchi akiwafundisha kwa njia ya mtandao.

"Nafundisha wanafunzi Tanzania na hata nje ya Tanzania mfano nina wanafunzi Marekani, Uingereza, Pakistan huwa wananipigia video call tunaanza mazoezi. Wao wanalipa Dola 500 kwa wiki na wanatakiwa kulipa kwa miezi mitatu kama hawa wa hapa nyumbani. Kila mmoja ana muda wake na wote wanapata saa moja ya kufanya mazoezi," anasema.


MAZOEZI YA PESA YAPO

Kuna mazoezi ya Denzel yanafurahisha sana, kama unapenda pesa kama bosi mmoja ambaye anatoka mikoa ya Kasazini utafurahi.

Kuna zoezi ambalo hukaa nyuma ya gari linalokuwa linatembea eneo la kuwekea mizigo na mlango ukiwa wazi, kisha anashika noti na kumtaka mwanafunzi wake kukimbia kuwahi kunyakua fedha hizo huku anatamka maneno moja moja.

"Yale ni mazoezi pia mwanafunzi anatakiwa kukimbiza lile gari kila noti akifanikiwa kuichukua inakuwa yake, lakini sharti ni moja zile zinakuwa Sh200,000, akifanikiwa kuzimaliza zinakuwa za kwake na akishindwa hata noti moja anatakiwa kuzirudisha zote," anasema Denzel.

"Wale ambao nawapa mazoezi ya kukimbia na gari wanakuwa ni wale ambao wanataka kupunguza uzito na siyo wagonjwa na unajua nafanya hivi ili kuwapa elimu pia kwamba hakuna pesa inayopatikana bila kujituma. Kwa hiyo hata wale wanatakiwa kujituma ili wazipate zile fedha zote.

"Naipenda kazi, napenda pia ninaowafundisha wafanikiwe. Inawezekana napata riziki, lakini kikubwa kwanza ni kuwafanya wale naowafundisha wafikie malengo na sioni kuchoka kuwahudumia watu."


CHANGAMOTO YA KAZI

Kila kazi ina fursa na changamoto zake, lakini kwa upande wa changamoto Denzel anayo moja, ingawa anaichukulia poa.

"Sitaki kuwa muongo changamoto ya kazi yangu ni ndogo ndogo, labda ni juu ya muda. Labda utamwambia mwanafunzi aje mtaanza mazoezi saa 1:00 asubuhi akaja saa 1:30 asubuhi yaani hiyo wala siyo kubwa sana," anasema.

"Unajua wanafunzi wangu wana majukumu yao kwa hiyo ratiba za maisha zinaingiliana, unatakiwa kuwaelewa lakini usiwe ndio kila siku unachelewa. Wanafunzi wangu wengi wanajitambua na najivunia kuwa nao."


KUFUNDISHA WASICHANA

Mkufunzi huyo ana wanafunzi wa aina tofauti na ni wa kila jinsia, isipokuwa upande wa wanawake anateswa zaidi na wasichana kuliko kinamama watu wazima.

"Kwanza sipendelei kuwafundisha wasichana sana. Unajua wasichana wengi wanaona mazoezi ni kujikomaza na utakapomwabia hapa ongeza (kasi) anaona unamtesa," anasema.

"Wapo wengine wanashindwa kufuata utaratibu mzuri wa mazoezi. Leo anaweza akaja, kesho asije sasa kupata matokeo halisi inakuwa changamoto. Napenda kufanya kazi na watu ambao wanataka kupunguza uzito wa mwili hasa kinamama au hawa wenye changamoto ya afya ambao wanakuwa na umakini mkubwa wa mazoezi utakayowapa.

"Napenda kufanya kazi na wachezaji wa mpira kama hawa ambao wanajua wanataka kujiimarisha kwa namna gani. Sina nia mbaya, labda ni wasumbufu, hapana. Lakini napenda kufanya kitu kwa malengo na nione matokeo.

"Nikiwa kwenye kazi yangu mimi ni mkali na huwa mkali ili uone uchungu wa ada yako unayolipa. Unapopambana na mtu mwenye uzito mkubwa anakuwa na matamanio ya kupungua hata kama ni msichana, lakini awe kwenye malengo ya kupungua."


HILI HATALISAHAU

Katika maisha kila mtu kuna tukio ambalo hawezi kulisahau, kwa Denzel anaikumbuka ishu ya kwenda nyumbani kwa mwanafunzi wake wa kike bila mume wa mwanamke huyo kujua na kilichomkuta ndicho asichokisahau.

"Kuna tukio lilitokea miaka ya nyuma. Kwa kweli liliniumiza sana. Nilikuwa na mwanafunzi ambaye ni mama akaniita kwake na wakati huo sikuwa nimeweka utaratibu kwamba nikija kukufundisha kwako, basi ni lazima watu wa familia wafahamu kwamba tutakuwa na ratiba ya mazoezi na niikute familia yako pia hapo nyumbani. Sasa huo utaratibu sikuwa nimeuweka," anaelezea.

"Nilikwenda kwenye nyumba moja hivi na mumewe hakuwa na taarifa kama nitakwenda. Wakati tupo kwenye mazoezi na huyo mama akaingia mumewe na kunikuta, alifoka sana. Akanifukuza vibaya akaniambia hataki kuniona nyumbani kwake na kama nikirudi pale atanifunga. Iliniumiza sana ile hali. Ilinitesa kwa muda."

Kuanzia siku hiyo mwalimu huyo ameweka utaratibu wa kabla ya kwenda mwanafunzi wake ambao ni lazima ufuatwe.

"Baada ya pale na mpaka sasa kwa mwanafunzi ambaye ananihitaji kwenda kwake kumpa mazoezi lazima famili yake ijue na nipate uhakika kwamba inajua ili kuondoa mambo kama haya. (Ile hali) haikuwahi kujirudia tena na yule dada ni mwanafunzi wangu mpaka leo."

Hata hivyo, Denzel anasema upande wa familia yake hajawahi kupata tatizo kutokana na kazi anayoifanya.

"Sipati shida na kazi yangu kuhusu familia yangu. Mimi sijaoa, lakini nina mtoto mmoja ambaye anakwenda kutimiza mwaka wa tatu mwakani, ila sikai na mama watoto wangu. Naishi na mama, dada zangu na mjomba," anasema.

"Mtoto wangu nilimpa jina la Denzel. Halikuwa jina langu, lakini kwa kuwa nimeishi na kujulikana kama Denzel nikaona nimpe mwanangu jina ambalo halikuwa baya. Hili jina lina maana kwamba ni mfinyango wa mchanga wenye baraka, ambao hauwezi kuingiliwa na kitu chochote kibaya au maadui."


BIBI MWANAFUNZI ALIYEFARIKI

Katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Denzel kumewahi kuwapo kwa picha ya bibi mtu mzima aliyekuwa mmoja wa wanafunzi wake na bahati mbaya Mei 11, 2024 alitangazwa kufariki dunia, taarifa iliyowahuzunisha wengi waliokuwa wanafuatilia namna alivyokuwa anapewa mazoezi.

Akimzungumzia bibi huyo, Denzel anasema: "Kwanza Kuna kitu nataka jamii ifahamu, wanafunzi wanaokuja hapa wote huwa nawachukulia kama watoto wangu hata kama wapo ambao wamenizidi umri. Hata ukiwa na miaka 50 hata zaidi ya hapo ukiwa darasani unakuwa kama mtoto mdogo wa kawaida. "Kitu cha kwanza huwa nazingatia akili ya yule mwanafunzi, natakiwa niende naye vipi kulingana na umri wake, maradhi  na changamoto yoyote ya afya kama anayo. Kwa hiyo kwa watu wazima wenye umri mkubwa unatakiwa kumsaidia kwa busara  na hekima, hususan yule bibi ambaye unamzungumzia.

"Yule alishakuwa mtu mzima, lakini ili uweze kumsaidia alihitaji michezo ili akili yake iweze kufanya kazi vizuri na kuyapokea yale unayomfundisha kirahisi. Nilikuwa najua ni namna gani niweze kwenda naye, nikawa namuandalia programu ambayo haitamkwaza kwa umri na hata changamoto alizonazo.

"Kwa hiyo zilipokuja taarifa za kifo chake zilinishtua  na kuniumiza. Ulikuwa msiba mkubwa kwangu kwa namna nilivyokuwa naye. Bahati mbaya sana alipoteza uhai wakati ambao alianza kuimarika kutokana na mazoezi aliyokuwa anayapata. Kuna wakati mwishoni aliniambia umenisaidia sana mwanangu kwa mazoezi niliyokuwa nampa."


HUYU NDIYE DENZEL

Denzel anasema aliacha kufanya kazi benki ili kujiajiri na kujikuta akiangukia kuwapigisha watu mazoezi ambayo sasa yanamlipa na anaifurahia kazi.

"Kazi hii niliianza miaka mitano au sita iliyopita. Kabla ya kuwa mwalimu nilikuwa nafanya kazi kwenye benki moja hapa nchini kisha nikaona niachane nayo ili nijiajiri  niwe mkufunzi wa mazoezi," anasema.

Hata hivyo, anasema haikuwa rahisi kwenda kujiajiri kwani alipitia kipindi kigumu cha ukata mtaani hadi akatamani kurudi kwenye ajira.

"Nilipoacha kazi nilisota kidogo. Nilihangaika sana. Kuna wakati nilitamani kuajiriwa tena, nilijaribu kwenda kuomba kazi tena benki mbalimbali lakini nikakosa na baadaye ndio nikajipata kupitia hii taaluma."

Akizungumzia gharama za mazoezi yake anasema, "Ada ni moja tu kwa watu wote. Unatakiwa uwe na Sh1,200,000 ambayo utailipa kwa miezi mitatu kabla ya kuanza na tunafanya mazoezi kila siku kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa."

Hata hivyo, anasema kwa kina Pacome kwa kuwa huwa hawawezi kupatikana muda wote wanalipa vipindi ambavyo wana nafasi kulingana na ratiba zao na mara nyingi huwa ni mara mbili kwa wiki.

"Hapo vipindi viwili kwa wiki na kila kipindi wanalipa Sh150,000 kwa siku."