Dakika za mwisho ikiaga msimu
Muktasari:
- Geita Gold na Kagera Sugar ndiyo timu pekee zilizojihakikishia kucheza Ligi Kuu Bara moja kwa moja msimu wa 2026-2027, baada ya miamba hiyo kuonyesha ushindani mkali tangu mwanzo wa ligi, zikimaliza nafasi ya kwanza na ya pili.
PAZIA la Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, linafungwa rasmi leo Ijumaa baada ya kudumu kwa siku 252, tangu ilipoanza Oktoba 10, 2025, huku vita kali kwa sasa ikibakia kwa timu zinazoshuka daraja na zile za kucheza 'Play-Off'.
Geita Gold na Kagera Sugar ndiyo timu pekee zilizojihakikishia kucheza Ligi Kuu Bara moja kwa moja msimu wa 2026-2027, baada ya miamba hiyo kuonyesha ushindani mkali tangu mwanzo wa ligi, zikimaliza nafasi ya kwanza na ya pili.
Katika mechi 29, ilizocheza Geita Gold inayofundishwa na Kocha Zubery Katwila imeshinda 23, sare tano na kupoteza moja ikiongoza na pointi 74 na kikosi hicho kilishuka daraja msimu wa 2023-2024.
Baada ya kuichapa Stand United mabao 3-1, Geita Gold itahitimisha msimu nyumbani kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita kwa kuikaribisha Bigman FC, yenye kumbukumbu ya kutoa sare ugenini ya mabao 2-2, dhidi ya African Sports ya mjini Tanga.
Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili na pointi 71, baada ya kuichapa Gunners ya Dodoma bao 1-0, itahitimisha msimu huu kwenye Uwanja wa Kaitaba, ikiikaribisha Mbeya Kwanza iliyochapwa 1-0, dhidi ya kikosi cha maafande wa Polisi Tanzania.
Gunners iliyochapwa bao 1-0 na Kagera Sugar, itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro kucheza dhidi ya Polisi Tanzania inayoshika nafasi ya tatu na pointi 63, ikijihakikishia kucheza mtoano (play-off) ya kuisaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara.
Maafande wa Polisi Tanzania watakutana na Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya nne na pointi 60, katika mechi ya Play-Off kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya timu zote kukusanya pointi ambazo hazitafikiwa na wengine.
Mbeya Kwanza iliyouzwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi kwa msimu wa 2024-2025, ilishuka daraja msimu wa 2021-2022, baada ya kikosi hicho kuburuza mkiani mwa nafasi ya 16 baada ya kukusanya pointi zake 25.
Msimu huo, Mbeya Kwanza ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28 na kwa sasa inapambana ili kurejea Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Kwa upande wa Polisi Tanzania msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25 baada ya kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya jijini, Mbeya, wenyeji KenGold baada ya kuichapa B19 FC mabao 3-1, itacheza dhidi ya maafande wa Transit Camp, yenye kumbukumbu nzuri baada ya mechi ya mwisho kuifunga Mbuni ya jijini, Arusha mabao 4-3.
Songea United iliyoichapa Hausung FC mabao 4-0, mechi ya mwisho, itahitimisha msimu kwenye Uwanja wa Majimaji Ruvuma kwa kucheza dhidi ya Barberian FC inayokabiliwa na presha ya kushuka daraja, licha ya kuifunga TMA FC ya Arusha mabao 2-1.
African Sports ya Tanga inayopambana kuepuka janga la kushuka daraja, baada ya sare ya mabao 2-2, dhidi ya Bigman FC ya Lindi, itakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga kucheza na Stand United yenye kumbukumbu ya kuchapwa na Geita Gold 3-1.
Kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF Kigamboni jijini Dar es Salaam, B19 FC iliyochapwa na KenGold mabao 3-1, mechi ya mwisho Mbeya, itahitimisha msimu kwa kucheza dhidi ya Mbuni ya Arusha, iliyotoka kuchapwa pia na maafande wa Transit Camp 4-3.
TMA FC iliyoshangazwa mechi iliyopita kwa kuchapwa nyumbani mabao 2-1 na Barberian FC itaikaribisha Hausung FC ya Njombe ambayo tayari timu hiyo imeshuka daraja baada ya mwenendo mbovu, ikiwa mkiani mwa msimamo na pointi zake tisa tu.
Hausung imepanda daraja msimu huu na kushiriki Ligi ya Championship baada ya kuongoza kundi A na pointi 25, ikiungana na mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2024-2025, Gunners FC ya Dodoma, iliyoongoza pia kutoka kundi B na pointi 35.
Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, katika mechi 29, ilizocheza imeshinda tatu tu, sare tatu na kupoteza 23, ikiwa mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi tisa na itacheza Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu wa 2026-2027.
Kocha Mkuu wa Hausung FC ya Njombe, Selemani Kitunda Simota 'Guardiola' alisema sababu ya timu hiyo kufanya vibaya hadi sasa katika Ligi ya Championship ni kutokana na kukosa wachezaji wazoefu, jambo lililochangia kwa wao kushuka daraja.
"Sababu kubwa iliyochangia sisi kushuka daraja ni kutokana na aina ya wachezaji tuliokuwa nao tangu mwanzo wa msimu huu, asilimia 90 hawana uzoefu na Championship tofauti na timu nyingine, tumejifunza kutokana na makosa," alisema Kitunda.
Aidha, Kitunda alisema mechi ya leo ya mwisho ni ya heshima kwao na wanataka kuitumia kupata matokeo mazuri, licha ya morali ya wachezaji wa kikosi hicho kushuka, kutokana na matokeo mabaya waliyopata tangu kuanza kwa msimu wa 2025-2026.