Dakika za jioooni, mabao yao yalivyoleta shangwe Ligi Kuu

HAIJAISHA hadi iishe kabisa. Ndivyo wanavyosema huko kitaa. Ukitaka kuamini hilo, njoo kwenye michezo na hasa soka ambao unafuatiliwa na wengi.

Kuna baadhi ya timu zinamaliza mchezo mapema tu kutokana na ubora wao na kuna zile ambazo ni lazima usubiri filimbi ya mwisho ya mwamuzi ndo uamini mechi imeisha, kwani lolote linaweza likatokea ndani ya dakika 90 za mchezo au zile za niongeza za mwamuzi.

Usiamini mchezo umeisha hadi filimbi ya mwisho. Kuna baadhi ya timu zimejikuta zikitoka na huzuni uwanjani kwa kufungwa mabao dakika za mwishoni na nyingine zikifurahia mabao ya jioni yaliyowapa pointi tatu muhimu au yaliyowaongezea idadi ya mabao.

Mwanaspoti linakuleta wachezaji waliofunga mabao dakika za jioni kuanzia dakika ya 90 na kuendelea na kuleta shangwe kwenye timu zao na kuziumiza nyingine.


PRISONS 1-1 MBEYA - HAMIS MCHA

Katika mchezo huu uliofanyika Septemba 9, Mbeya City walitanguliwa kwa bao la Hassan Nassor dakika ya saba,  lakini jioni kabisa dakika ya 90, Hamis Mcha aliisawazishia Prisons na mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.


YANGA 3-0 MTIBWA - AZIZ KI

Aziz Stephane Ki alifunga bao dakika ya 90+1 na kuiongoza Yanga kushinda mabao 3-0, mabao mengine katika mchezo huu uliofanyika Septemba 1, 2022 yalifungwa na Djuma Shaban kwa faulo nje ya 18 na Fiston Mayele.


PRISONS 1-1 NAMUNGO- FRANK MAGINGI

Ilikuwa siku mbaya kwa beki wa Namungo, Frank Magingi baada ya dakika 90 kujifunga na kuikoa Prisons kulala katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine Mbeya na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Shiza Kichuya ndiye aliyeanza kuifungia Namungo bao dakika ya 21.


SIMBA 5-0 MTIBWA- PAPE SAKHO

Katika mchezo huu uliofanyika Oktoba 30 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkapa Sakho alifunga bao dakika ya 90+1 na kuhitimisha ushindi mnono wa mabao 5-0 ambao Simba ilipata.


POLISI 1-1 DODOMA- COLLINS OPARE

Iddi Kipagwile alianza kuifungia Polisi Tanzania bao dakika ya 56 kwa penalti lakini dakika ya 90+4 Collins Opare aliikoa Dodoma Jiji kwa kuifungia bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika mchezo uliofanyika Novemba Mosi, 2022.


AZAM 2-1 DODOMA JIJI - IDRISA MBOMBO

Ismal Aziz alifunga kwa kichwa dakika ya 37 dakika tatu baadae Opare aliisawazishia Dodoma Jiji lakini wakati wengi wakiamini mechi hiyo iliyofanyika Novemba 9 mwaka jana ingemalizika kwa sare, Idrisa Mbombo akaibuka shujaa kwa kuifungia Azam bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 90+1.


POLISI 1-3 SIMBA - ZUBERY KHAMIS

Straika huyu wa Polisi Tanzania aliifungia timu yake bao la kufutia machozi dakika ya 90+1 katika mchezo uliofanyika Novemba 27, 2022 kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.


AZAM 3-2 COASTAL UNION- IDDI NADO

Wakati hadi dakika nane za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika mechi hiyo kuwa sare ya mabao 2-2 lakini dakika ya 90+9 Iddi Nado aliwainua vitini mashabiki wa Azam baada ya kufunga bao la ushindi katika mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Novemba 27 uwanja wa Azam Complex. Hili ndilo bao la jioni zaidi kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa msimu huu.


SINGIDA 3-0 NAMUNGO- AMISS TAMBWE

Tambwe aliifungia bao la tatu Singida Big Stars dakika ya 90+3 katika mchezo uliofanyika Desemba 12 mwaka jana.


GEITA 2-2 MTIBWA- GEORGE WAWA

Moja ya mechi iliyokuwa ya kuvutia sana na hadi dakika 90 wenyeji Geita Gold walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Desemba 2. Hata hivyo, zilipoongezwa dakika tatu za nyongeza ikawa balaa kwao kwani Mtibwa Sugar walisawazisha dakika ya 90+2 baada ya beki wa Geita, George Wawa kujifunga akiokoa kwa kichwa krosi iliyopigwa na Adam Adam.


SINGIDA 1-2 COASTAL- DEUS KASEKE

Dakika ya 90+7, Deus Kaseke alifungia bao la kufutia machozi Singida United katika mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Desemba 7 kwenye uwanja wa Liti.


MTIBWA 1-1 NAMUNGO- KONNOU PATERNE

Wakati hadi dakika 90 Mtibwa Sugar ikiwa ina matumaini ingeondoka na pointi zote tatu katika mchezo huu lakini mambo yalibadilika dakika za nyongeza baada ya Konnou Paterne kuisawazishia Namungo kwa kichwa dakika ya 90+2.


RUVU 0-2 IHEFU- MICHAEL AIDAN

Mchezo huu uliofanyika Desemba 16 kwenye Uwanja wa Azam Complex, dakika ya 90 Michael Aidan aliizawadia bao la pili Ihefu bada ya kurudisha mpira vibaya kwa kipa wake Hussein Masalanga aliyeteleza na mpira huo kumpita na kujaa wavuni.


MBEYA 1-2 DODOMA JIJI- TARIQ SEIF

Dakika ya 90+5 Seif aliifungia Mbeya City bao la kufutia machozi mchezo uliofanyika Desemba 18.


AZAM 6-1 MBEYA- CLEOFACE MKANDALA

Aliifungia Azam bao la sita dakika ya 90+2 katika mchezo uliofanyika Desemba 31 kwenye uwanja wa Azam Complex.


GEITA 1-1 POLISI- SALUM ALLY

Ally aliikoa Polisi Tanzania na kipigo baada ya kuisawazishia bao dakika ya 90 na kuufanya mchezo huo uliofanyika Januari 20 mwaka huu kumalizika kwa sare ya bao 1-1.


PRISONS 1-2 IHEFU- RAPHAEL DAUD

Wakati wengi wakiamini mchezo huu utamalizika kwa sare, lakini Daud alibadili matokeo dakika ya 90 kwa kuifungia Ihefu bao la pili kwa kichwa katika mchezo uliofanyika Januari 21 uwanja wa Sokoine.


KMC 1-3 NAMUNGO- IBRAHIM MKOKO

Mkoko aliifungia Namungo bao la tatu dk 90+5 katika mchezo uliofanyika Januari 24 kwenye uwanja wa Uhuru huku mchezaji huyo akifunga hat-trick siku hiyo.


MTIBWA 2- 1 DODOMA JIJI- SEIF KARIHE

Dakika ya 90+3, Seif Karihe aliifungia Dodoma Jiji bao la kufutia machozi, Februari 2 kwenye uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro.


SIMBA 1- 1 AZAM - ABDALLAH HERI SEBO

Azam walionekana kuukamata mchezo huu uliofanyika Februari 21 lakini jioni kabisa mambo yakageuka baada beki wa timu hiyo Sebo kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa kichwa wa Kibu Dennis dakika ya 90.


RUVU 0- 1 KAGERA- HAMIS KIIZA

Dakika ya 90 Hamis Kiiza' Diego' aliifungia bao Kagera Sugar na kuipa pointi tatu muhimu katika mchezo huo uliofanyika Februari 24 kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.


SINGIDA 3-0 POLISI TANZANIA - AMISS TAMBWE

Ammis Tambwe aliifugia bao timu yake dakika ya 90 na kuiongoza  Singida Big Stars kushinda mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika April 7 uwanja wa Liti Singida.


YANGA 5-0 KAGERA SUGAR- AZIZ KI

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz Stephan Ki alikamilisha hat-trick yake siku hiyo kwa kufunga penalti dakika ya 90 katika mchezo uliofanyika April 11 kwenye uwanja wa Azam Complexi. Mabao mengine yalifungwa na Mayele na Benard Morrison.


SIMBA 3-0 RUVU SHOOTING- PAPPE SAKHO

Sakho alimaliza shughuli ya kuishusha daraja Ruvu Shooting kwa kufunga bao la tatu na la jioni dakika ya 90+3 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex ambao Simba ilishinda mabao 3-0. Sakho pia alifunga bao la pili dakika ya 72 na lingine lilifungwa na Clatous Chama dakika ya 30.


YANGA 4-2 DODOMA JIJI- MUDATHIR YAHYA

Katika mchezo huu uliofanyika Mei 13 kwenye uwanja wa Chamazi, Mudathir Yahya aliifungia bao la nne Yanga dakika ya 90+4 na kuhitimisha karamu ya mabao katika mchezo huo ambao Yanga ilitangaza ubingwa msimu huu. Mabao mengine yalifungwa na Mudathir mwenyewe, Farid Mussa na Musonda.