Prime
Coastal Union V Simba… Hesabu za akili!

Muktasari:
- Simba ina dakika 90 za hesabu kwa sababu, ikitoka hapo, kituo kitakachofuata ni Dabi ya Kariakoo itakayiopigwa wikiendi ijayo pale Kwa Mkapa.
KIKOSI cha Simba kipo ugenini jijini Arusha na jioni ya leo itaikabili Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Hizo ni dakika 90 za hesabu kali na za akili kwa timu zote, hususani Simba iliyopo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu.
Simba ina dakika 90 za hesabu kwa sababu, ikitoka hapo, kituo kitakachofuata ni Dabi ya Kariakoo itakayiopigwa wikiendi ijayo pale Kwa Mkapa.
Kumbuka Simba ilipoteza mechi ya kwanza mbele ya watani wao wa jadi ambao jioni ya jana walikuwa uwanjani jijini Mwanza kuvaana na Pamba Jiji huku zikitofautiana pointi nne. Kama Yanga imepata ushindi itakuwa na maana imeongeza pengo la pointi ikifikisha 58, saba pungufu na ilizonazo Simba yenye 51, licha ya kuwa na michezo miwili mkononi ambayo hata kama itashinda itafikisha 57 tu.
Kwa wenyeji Wagosi wa Kaya, pambano hilo hata kwao ni la hesabu kwa vile inahitaji ushindi ili kujiweka pazuri katika mbio za kumaliza katikati ya msimamo, kwani kwa sasa in pointi 24 baada ya mechi 21 na ikiteleza kwa Simba itatoa nafasi kwa timu zilizopo nyuma yao kuwapiku na kujiweka pabaya kwa vile pointi ilizonazo na zilizopo mkiani zinatofautiana kidogo.
Katika mchezo wa duru la kwanza, Simba iliduwazwa na Coastal kwa kulazimishwa sare ya 2-2, Wagosi wakichomoa dakika za jioni na kama sio mwamuzi Japhet Smart kumaliza pambano wakati Coastal ikiwa katika shambulizi la kusaka bao la tatu, mambo yangekuwa mengine.

Simba inajua mtego wa mchezo huo, ikifanya makosa tu ya kudondosha pointi, itakuwa kama inaendelea kujimaliza katika mbio za kutaka kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliyoukosa kwa misimu mitatu mfululizo sasa mbele ya Yanga watakaokutana nao wiki ijayo katika Dabi ya Kariakoo.
Katika mechi 10, zilizopita baina ya timu hizo, Simba imeshinda mechi saba, Coastal ikiwa imetoka patupu, ikiambulia sare tatu tu ikiwamo iliyopita ya 2-2 pale KMC Complex.
Ukiondoa sare mbili zisizo na mabao, lakini Simba ina rekodi nzuri ya kufunga mabao mbele ya Coastal kwani imevuna mabao 24 wakati wagosi hao wakifunga matano tu katika mechi hizo 10 zilizopita.
Coastal inatakiwa kujipanga sawasawa kuizuia Simba, ambao ina hasira ya kutoka kulazimishwa sare ya 2-2 nyumbani na Azam, lakini ikiwa na kumbukumu ya kuwahi kupigwa 7-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika mechi iliyopigwa Novemba 21, 2020.
Ukuta wa Coastal utakuwa na kazi ya kuwazuia mastaa wawili wa Simba, wanaongoza kwa ufungaji kwa Wekundu Jean Charles Ahoua mwenye mabao 10 na asisti sita na mshambuliaji Lionel Ateba mwenye mabao nane na rekodi zinaonyesha katika mechi tano zilizopita, Simba imefunga jumla ya mabao 12 na ukuta wao kuruhusu matatu tu.

Simba itakayowakosa kipa Moussa Camara na beki mzoefu, Che Malone Fondoh walioumia kwenye mchezo dhidi ya Azam, itatakiwa kuwazuia mshambuliaji Maabad Maabad mwenye mabao matano akiwa ndio kinara wa ufungaji ndani ya timu hiyo, akifuatiwa na winga Mkenya Abdallah Hassan aliyefunga mabao mawili lakini pia akiwa ni mfungaji wa bao moja kati ya mawili kwenye sare ya mwisho baina ya timu hizo, akimtungua kiufundi Moussa Camara.
Hata hivyo, kwa mechi tano zilizopita, Coastal imeonekana kuwa butu eneo la ushambuliaji kwa kufunga mabao mawili tu, huku yenyewe ikifungwa matatu na mechi tatu kati ya hizo ikitoka na clean sheet kitu kinachonyesha mechi itakuwa ngumu kwa timu zote. Kipa Chuma Ramadhani ataendelea kusimama katika milingoni ya Coastal, huku Aishi Manula au Ally Salimu wakitarajiwa kuanza kwa upande wa Simba.
Coastal inayonolewa na kocha Juma Mwambusi, imeonekana kucheza mpira wa kujilinda zaidi kitu kinachoweza kuwapa ugumu Simba kuipenya ngome ya timu hiyo, ingawa kwa aina ya uchezaji wa mabeki wa Coastal, kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana penalti kwa leo, kwani Simba ina wachezaji wajanja ambao wakiguswa kidogo hujiangusha akiwamo Kibu Denis na Shomary Kapombe.

Kocha wa Simba Fadlu Davids, akizungumzia mchezo huo, alisema ni mechi ambayo wanahitaji kushinda vizuri ili kurudisha hesabu zao sawasawa kwenda kuchukua ubingwa huku akigoma kabisa kuiweka Yanga kwenye hesabu za mchezo huo lakini akimtaja Maabad.
"Tunakwenda kukutana na Coastal Union, hii ni mechi ngumu ukizingatia wapinzani wetu ni timu nzuri isiyotabirika, imebadilika mara ya mwisho tulipokutana nao walikuwa chini ya kocha wa muda lakini sasa ina kocha mwingine na anaonekana ameiimarisha timu yake," alisema Fadlu.
"Tunahitaji kushinda ili tuweke hesabu zetu sawasawa, tulifanya makosa ya kuangusha pointi kwenye mchezo uliopita, Coastal Union ina wachezaji wazuri kuna yule Maabad ni mshambuliaji mwenye nguvu na akili lakini wana viungo wazuri, sitaki kuiweka mechi ya dabi kwenye mchezo huu, tutapambana kwanza na Coastal Union."
Beki na nahodha wa timu hiyo, Shomary Kapombe alisema tayari wamefanya maandalizi ya kutosha ili kushinda mchezo huo na kujitengenezea mazingira mazuri ya kutimiza malengo ambayo ni kutwaa ubingwa.
Kwa upande wa kocha wa Coastal, Juma Mwambusi alisema mchezo huo hutakuwa mrahisi kutokana na mahitaji ya timu zote hivyo wamejipanga kuhakikisha wanabakiza pointi tatu muhimu ambazo zitawasogeza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
"Tuko tayari kupambana na Simba kwa sababu tunajua ubora wao upo sehemu gani na madhaifu yao pia yapo sehemu gani hivyo naamini mchezo utakuwa mzuri," alisema Mwambusi aliyeipokea timu hiyo bada ya Mkenya David Ouma kutimuliwa mwanzoni mwa msimu huu.

Mwambusi alisema morali kwa wachezaji ipo juu kutokana na matokeo iliyopata katika mechi mbili za mwisho, lakini matokeo ya jijini Dar es Salaam walipolazimisha sare mbele ya Simba na anaamini wanaweza kupata ushindi nyumbani.
Coastal 5 zilizopita
Namungo 0-0 Coastal
Coastal 0-0 Azam
Pamba Jiji 2-0 Coastal
Mashujaa 0-0 Coastal
Coastal 2-1 JKT TZ
Tano zijazo
v Dodoma Jiji (ugenini)
v Kagera Sugar (ugenini)
v Yanga (ugenini)
v Singida BS (nyumbani)
v KenGold (nyumbani)
Simba 5 zilizopita
Simba 2-2 Azam
Namungo 0-3 Simba
Simba 3-0 TZ Prisons
Fountain 1-1 Simba
Tabora Utd 0-3 Simba
Tano zijazo
v Yanga (ugenini)
v Mashujaa (nyumbani)
v JKT Tanzania (ugenini)
v Pamba Jiji (nyumbani)
v KMC (ugenini)
Matokeo yaliyopita
2011-2012
Coastal 0-1 Simba
Simba 2-1 Coastal
2012-2013
Coastal 0-0 Simba
Simba 2-1 Coastal
2013-2014
Coastal 0-0 Simba
Simba 0-1 Coastal
2014-2015
Simba 2-2 Coastal
Coastal 0-0 Simba
2015-2016
Simba 1-0 Coastal
Coastal 0-2 Simba
2019-2020
Coastal 1-2 Simba
Simba 8-1 Coastal
2020-2021
Simba 2-0 Coastal
Coastal 0-0 Simba
2021-2022
Coastal 0-7 Simba
Simba 2-0 Coastal
2022-2023
Coastal 0-3 Simba
Simba 3-1 Coastal
2023-2024
Simba 3-0 Coastal
Coastal 1-2
2024-2025
Simba 2-2 Coastal
Coastal ?? Simba