Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Coastal Union V African Sports… Dabi inayowaumiza vichwa

TANGA Pict

Muktasari:

  • Kama ilivyo kwa Simba na Yanga kuwa moja ya dabi maarufu nchini na Afrika kwa ujumla, huko Tanga kuna dabi ya kihistoria ambayo hata hivyo ni muda mrefu  haijapigwa na kuwakata stimu mashabiki wa soka wa huko.

ACHANA na mashabiki wa Simba na Yanga wanaojadili Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa kutoka Machi 8 kisha kupelekwa Juni 15 na wikiendi iliyopita ikapelekwa Juni 25 kumaliza ile sintofahamu ya ‘Hatuchezi’ na ‘Tutacheza’, huko Tanga nako kuna watu wanaiota dabi.

Kama ilivyo kwa Simba na Yanga kuwa moja ya dabi maarufu nchini na Afrika kwa ujumla, huko Tanga kuna dabi ya kihistoria ambayo hata hivyo ni muda mrefu  haijapigwa na kuwakata stimu mashabiki wa soka wa huko.

Dabi hiyo inayootwa na Wagosi wa Ndima sio ya timu za Kariakoo, bali ni Dabi ya Tanga inayohusisha Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ na African Sports ‘Wanakimanumanu’. Hii ni moja ya mechi zinazovutia hisia za mashabiki katika eneo la Kaskazini mwa Tanzania kutokana na ushindani wa kihistoria.

Timu hizo zina mizizi ya muda mrefu katika soka la Tanzania na kwa kumbukumbu ilipigwa mara ya mwisho katika Ligi Kuu 2015-2016 wakati African Sports ilipopanda daraja kabla ya kushuka sambamba na Coastal na Mgambo JKT zikiweka rekodi timu tatu za mkoa mmoja kushuka kwa mpigo msimu mmoja.

Kama hujui Coastal Union inayobebwa na jezi zenye rangi nyekundu na nyeupe kama za Simba ilizaliwa 1948 tofauti na Wanakimanumanu ambao ni wakongwe zaidi, kwani timu hiyo ilizaliwa Novemba 18, 1936 na imekuwa ikinasibishwa na Yanga, japo inatumia rangi za bluu na nyeupe.

Timu hizo ziliwahi kuweka rekodi ya aina yake 1988 zilipotwaa mataji yote makubwa nchini, Coastal ikibeba ubingwa wa Ligi ya Bara na Sports kunyakua taji la Ligi Kuu ya Muungano, ambayo imerejeshwa kwa jina la Kombe la Muungano, lakini ikiwa haina ule mzuka wa zamani ambapo bingwa alikata tiketi ya michuano ya Klabu BIngwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika).

Mwanaspoti ilifunga safari mpaka Tanga kujua ni sababu zipi hasa za dabi hiyo kupotea katika kipindi cha miaka 10 na hapa Ofisa Habari wa Coastal Union na wazee wa timu zote mbili wanatupa sababu.


TA 04

         

AINA ZA DABI

Wengi wanafahamu kuwa mechi inachezwa uwanjani tu, lakini Ofisa Habari wa Coastal Union, Abbas El-Sabri anasema kuwa kwa Tanga mechi ilikuwa haianzii hapo tu.

“Tanga Derby ndio ilikuwa kubwa kuliko hata ya Kariakoo, ndio maana utasikia kulikuwa na hadithi kwamba mpira ulipasukia uwanjani au mtu kufukiwa baharini. Hizo zilikuwa dabi za nje ili timu (mtu) yake ipate ushindi.

“Dabi ya Tanga ina vionjo vingi zaidi kuliko ya Mzizima au Kariakoo, maana yake hapo wazee walikuwa wakitafuta ushindi nje ya uwanja,” anasema.

“Lakini pia ukija kwa mashabiki wao African Sports walikuwa na kikundi chao cha Kimanumanu chenyewe kinapambania kundi la Coastal Union ambayo ilikuwa inaongozwa na shabiki maarufu ambaye alikuwa akiitwa Bwana Kaka. Alikuwa anavaa nguo flani hivi kama nyekundu, kila upande ulikuwa na nyimbo zao.

“Sisi klabu yetu ina alama ya mbwa kwa hiyo kuna nyimbo flani walikuwa wakiziimba zinatukera sana. Walikuwa wanaimba hivi ‘kijibwa koko hicho kinatembea na Wazungu charinga nini’. Kwa hiyo ni vitu ambavyo vilikuwepo na viliunganisha mkoa wetu.”

TA 03

AFRICAN SPORTS CHANZO

Akiizungumzia African Sports, El-Sabri anasema: “Hizi ni timu za wanachama na mara nyingi watu wanajitoa zaidi maana yake hakuna faida ambayo wanaitegemea. Kilichoifelisha African Sports ni ile hali ambayo ilikuwepo na sasa imepungua.

“Kitendo hicho ambacho kimesababishwa na vijana wa sasa ndicho kilichosababisha kutorudi kwenye zama zao, lakini naamini watakuwa sawa.

“Kama msimu huu imenusurika kushuka daraja tena Daraja la Pili. Kwa hiyo wameanza kujipanga upya kuhakikisha kuwa wanapambana kwa namna yoyote kurudisha timu Ligi Kuu.

“Kinachofanya mambo yaharibike zaidi ni hili tabaka la vijana wa sasa ambao wamekuwa wazito kujitoa kwa asilimia kubwa kuliko wazee wetu walivyofanya.

“Kama Afrcan Sports haipo kwenye msimamo wa ligi basi hakuna dabi ya Tanga kwa sababu hawa wote ndio wanaoleta msisimko wa hiyo mechi hasa wakiwa katika shindano moja.”


NINI KIFANYIKE?

El-Sabri anasema kabla ya msaada kutoka nje ya Tanga kufika klabu hizo pamoja na wanachama wake wajipange kujisaidia wenyewe kwanza kuziinuaili kurejesha sifa iliyopotea. “Watu wa Tanga wenyewe wanatakiwa kuungana ili kuisaidia timu kusalia katika mashindano. Hata kwa Coastal Union imefanyika na hivi karibuni African Sports pia walisaidiwa ili timu isishuke Daraja la Pili.

“Ndio maana wataendelea kubaki Championship, kwa hiyo nguvu iliyotumika kuibakisha ndio iliyopangwa kuhakikisha inapanda Ligi Kuu. Na hiki ndicho kinachopaswa kufanyika yaani Tanga yenyewe iendelee kuungana na kuwa kitu kimoja. Kwa sasa mpira ni ufundi, juhudi na pesa.”


UCHUMI KUTETEREKA

Ofisa huyo anazungumzia ishu ya uchumi akisema kama ilivyo kwa dabi zingine zinapochezwa wafanyabiashara wanavyonufaika hata Tanga ilikuwa hivyo pia wakati huo.

“Kwanza ile wiki ya dabi kunakuwa na tambo kwenye masoko, barabarani au sehemu zenye mkusanyiko wa watu unaweza kuona namna kunavyoamka.

“Sasa hivi ni kama kumekuwa na kulala kwa mkoa kwa sababu ikiwepo dabi inaamsha vitu vingi. Kuna watu wanatoka Korogwe, Handeni, Lushoto au Mombasa hawa wote wanatumia pesa kufika hapa,” anasema El-Sabri.

“Wakija hapa watalala hotelini, watakula maana yake (wafanyabiashara) watafanya kazi na wataingiza kipato na ule mkusanyiko wa watu sehemu moja unafungua mianya ya biashara nyingine nyingi na masoko yanapatikana...huenda Tanga ingekuwa kubwa zaidi ya hapa.”


KARIA, MNGUTO

Ofisa huyo anasema viongozi wakubwa wa soka kuishabikia Coastal Union hakumaanishi kwamba timu hiyo inapata wepesi kama wengi wanavyodhania katika masuala ya uendeshaji.

“Kuna kitu nikiweke sawa ambacho huwa nakutana nacho sana, mfano raisi wa TFF (Wallace Karia) ni mwanachama kweli wa timu yetu na kila tukio muhimu anakuwepo,” anasema.

“Kwa hiyo uwepo wake pale TFF unatupunguzia vitu vingi kama klabu kwa sababu sisi hatuwezi kulalamikia chochote ni kama vile umezibwa mdomo, ni kama vile baba yako akiwa ni kiongozi huwezi kulalamika na kila mtu anaamini wewe una kila kitu.

“Watu wengi wanatuona kama watoto wa mwisho wa TFF kama tunadekezwa, kwa hiyo hata ukilalamika hakuna anayekusikiliza, kuna mambo yanatokea na huna wa kumlalamikia, wakati baba ndio mkuu.

“Kuna muda mnasema kabisa hivi baba anaona kwamba hapa tunaonewa, mbona kakaa kimya, unaona ngoja unyamaze uache lakini uwepo wa viongozi hao umetuamsha tunahisi kama tuna deni ndio maana tulifurahi kushiriki kimataifa na ikawa kama zawadi ya heshima kwao.

“Ila kusema kwamba wanatumia mamlaka yao kunufaisha nyumbani ni uongo. Sisi watu wa Tanga hatuna kabisa tabia hizo tunapenda haki. Kama wangefanya hivyo basi tungekuwa tunashika nafasi ya kwanza.”

TA 05

MASHABIKI BALAA

Kuhusu mashabiki, El-Sabri anasema licha ya kuwa African Sports haishiriki Ligi Kuu, lakini mashabiki wake wameshindwa  kuwashabikia wapinzani wao hata wacheze mashindano gani. “Kila timu ikija kucheza na Coastal Union hiyo ndio inakuwa ya African Sports na wanawapa mbinu zote za jinsi ya kutupiga sisi mfano tulicheza mechi ya Kombe la FA msimu uliopita hapa Mkwakwani,” anasema.

“JKT walipokewa na wenyeji wa hapa Tanga wakaandaliwa chakula na kila kitu, wakapewa mbinu za wapi waingie ili waweze kutufunga. Kwetu tunaona ni vitu vya kawaida.

“Lakini bahati mbaya ukiwa juu huwezi kumfanyia ubaya alie chini. Kwa hiyo tunatamani kumvuta mwenzetu aje. Tunawasaidia kwa kuwavuta wachezaji ambao kwetu hawapati nafasi basi tunawapeleka kwa mkopo African Sports wakaongeze nguvu.

“Ingawaje ni tofauti kidogo sisi roho zetu zimekunjuka kidogo na tumeamua kuwasaidia wenzetu ili nao waweze kurudi katika ubora wao.”

TA 02

SPORTS ZAIDI

Katika timu yoyote ile huwa kuna upande wenye mashabiki wengi kuliko mwenzake, na hapa El-Sabri anasema African Sports waliwazidi.

“African Sports ndio iliyoanza kuzaliwa kuliko sisi wao walianza 1938 sisi 1948. Wametupita miaka 10, lakini mafanikio ndio yanayotenganisha maji na mafuta.

“Yaani kadri siku zinavyozidi kwenda klabu yenyewe ilikuwa inahakikisha inajitanua kwa sababu sisi sio timu ya Tanga tu ila ukanda wote wa pwani kuanzia Tanga, Mombasa, Bagamoyo. Kwa hiyo tulijizolea mashabiki eneo kubwa,” anasema.

“Hiyo ikaifanya klabu yetu kuwa na mashabiki wengi ambao wanaichangia ili kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya kukuza na kujiendeleza. Kwa hiyo ukigawanya unapata nusu African Sports na Coastal Union.”


URITHI

Katika suala la urithi, mambo ni tofauti na El-Sabri anaeleza kuwa zamani familia za Tanga zilikuwa kama sio Coastal Union, basi ni African Sports kwa hiyo mtoto akizaliwa anarithi.

“Sisi sio mashabiki wa Coastal Union, ila wazee wetu ndio mashabiki kwa hiyo tuliridhi kutoka kwa wazazi, hivyo mimi nakuwa timu fulani kwa sababu ya baba, anasema El-Sabri.

“Hii imekuwa asili yetu na wachache ndio wakahama ila ni kosa... unaonekana kama muasi, hiyo inakwenda haibadiliki unakuwa umewekwa alama kabisa...hakuna kuhama.

“Kuna watu iliwaathiri yaani alikuwa Coastal Union halafu wazee wake ni African Sports. Kwa hiyo wanapokuja kugombea mambo ya uongozi huwa anakataliwa kwa sababu wanahisi si  mwenzao.

“Ndio maana unakuta shabiki wa hizi timu mbili hata awe Ulaya au wapi atabaki kuwa hivyo, hawezi hata kuwa Simba au Yanga. Sisi tunaweza kuisaidia timu nyingine kwa sababu ya kuwachangamsha na sio kuhamia.”

TA 01

MATUKIO HATARI

El-Sabri anasema yapo matukio ambayo anayakumbuka kwenye mechi za Dabi ya Tanga yaliyofanywa na wazee kabla ya mechi.

“Dabi ya wazee ndio iliacha historia kubwa nyingi, lakini ninazozikumbuka ni mbili na yalitokea matukio ya kushangaza. Kwanza ni mpira kupasuka uwanjani.

“Mpira ulikuwa unaingia golini upande wa Coastal Union. Kwa hiyo kabla ya kufika ulipasuka katikati ya uwanja. Kwa hiyo huo ulikuwa ushindi wa dabi ya wazee nje ya uwanja.

“Lakini pia kuna tukio maarufu sana ambalo linazungumzwa la mmoja kati ya shabiki wa African Sports ambaye alikubali kufukiwa ili timu yake iweze kupata ushindi,” anasema.

“Sasa baada ya timu kupata ushindi watu wakasahau kule kama kuna mtu wamemfukia ili wakamtoe. Kwa hiyo baada ya mechi kuisha na watu wakafurahia ushindi mpaka usiku ndio wanakumbuka.

“Kwa hiyo mpaka kumpata baharini usiku watu hakuna kwa hiyo akabaki pekee yake tayari alijua umauti unakuja kwa sababu kulikuwa hakuna mbadala maana yake wangemuacha basi angefunikwa na maji. Unaweza kuona jinsi ilivyokuwa hatari. Ukiona imeshinda Coastal Union ujue wazee wa African Sports ndio wamezidiwa nguvu.

“Matokeo ya nje ya uwanja ndio yanasababisha timu kushinda au kushindwa, kwa hiyo matukio yaliyokuwa yanatokea yalikuwa yanaonyesha ukubwa wa wazee wa klabu husika.”


HAWAITAKI DABI

El-Sabri anazungumzia upande wa pili wa Dabi ya Tanga akisema: “Kutokuwepo kwa African Sport katika ligi kweli tunahema maana mchakamchaka wake unakuwa mzito, tukichezaga nao tu ujue mechi tatu au nne mbele tutakuwa na matokeo mabaya.

“Kwa sababu wanatuonea sana nje ya uwanja wenzetu wale... hiyo ‘idara’ wako vizuri sasa matokeo yake unakuwa hutamani kabisa kukutana nao.

“Sisi tunawatambia sana sasa hivi. Tunawaambia kabisa kwamba hatuko nao sawa kabisa, licha ya kuwa waliwahi kutusumbua ila tumekuwa kaka zao.”

Hata hivyo, anasema licha ya kutoitaka dabi hiyo, lakini wameimisi sana.

“Kwa kweli tumeikumbuka sana, hata mara ya mwisho tulivyocheza tuliiona ladha flani inaanza kujirudia ...unaona kabisa watu wanapenda mechi zile.

“Pamoja na Coastal Union kuwepo katika ligi na African Sports kushiriki Championship, lakini bado unaiona nguvu ya Dabi ya Tanga bado haijawahi kufunikwa na mashindano yoyote yale.”


COASTAL, SIMBA

Ofisa huyo anagusia ukaribu uliopo baina ya Coastal Union na Simba.

“Zamani ndio ilizoeleka hivyo kwa sababu ya rangi tu wazee wetu walikuwa wana ukaribu na Simba kutokana na sababu zao binafsi ikiwemo mfanano wa jezi.

“Lakini hata African Sports na Yanga zamani walikuwa karibu kwa sababu ya rangi pia, ila ukweli ni kwamba timu hizi zote zinashiriki ligi na hatuwezi kuwa maadui. Kwa hiyo tuna ukaribu wa kawaida tu.”


WENYE TIMU ZAO

Mmoja wa wazee maarufu wa African Sports, Abuu Kitwana anasema: “Enzi hizo sisi ndio tulikuwa tunatamba ukiangalia hawa (Coastal Union) wamezaliwa 1948 sisi 1938, ni watoto wadogo kwa hiyo lazima waogope kucheza na sisi.”

“Tuko Daraja la Kwanza ila hawataki kusikia mechi na sisi kwa sababu bila ya changamoto wanajua tukirejea huwa tunafanya kweli.

Shabiki wa Coastal Union, Shaffi Ali anasema hajachanganya Simba au Yanga kama walivyo wengi.

“Katika mji wetu wa Tanga tunapocheza dabi ya Coastal Union na African Sports huwa inaleta mvuto sana, mkoa pia unajaa watu wengi kushuhudia dabi.

“Japokuwa African Sports ikija tu Ligi Kuu ujue inakuja kutusumbua mwaka 2015 ilipopanda tu ilitushusha na sisi hatuwaombei warudi maana hata dabi huwa wanabahatika kutufunga.