Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Clatous Chama anavyoendeleza makali Singida Black Stars

CHAMA Pict


AKIWA na umri wa miaka 34, kutokana na kuzaliwa Juni 18, 1991 katika jiji la Lusaka Zambia, Clatous Chota Chama ameendelea kuthibitisha kwa mara nyingine kwa nini jina lake linapaswa kuendelea kuimbwa katika soka la Tanzania.


Safari yake kutoka Zambia na kutua Tanzania kucheza klabu za Simba, Yanga hadi sasa Singida Black Stars, imekuwa ya kupanda na kushuka. Hii inatokana na nafasi anayoipata katika timu alizopita, huku akiweka heshima yake katika michuano ya CAF alipoonyesha kiwango kikubwa akiwa Simba kwa kuivusha kwenye nyakati ngumu.


Uzoefu wa Chama kwenye michuano ya CAF haujaja ghafla. Simba ilipomtoa Zambia na kutua ardhi ya Bongo msimu wa 2018-2019, alifanya makubwa na kikosi hicho kilichocheza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza msimu huo baada ya muda mrefu kupita.

Uwezo aliouonyesha akiwa Simba, uliwavutia RS Berkane walioamua kumsajili Agosti 16, 2021, hata hivyo, hakudumu sana, akarejea Simba kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huohuo 2021-2022.

Aliitumikia tena Simba hadi mwisho wa msimu wa 2023-2024 alipohamia Yanga na huko amecheza kwa msimu mmoja pekee 2024-2025, akatua Singida Black Stars msimu huu 2025-2026.

CHAM 05

Kwa sasa, chini ya Kocha Miguel Gamondi, raia wa Argentina, miguu ya Chama imekuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Singida Black Stars ambacho kwa mara ya kwanza kimefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Siyo kufuzu tu, bali timu hiyo imevuna alama moja na bao moja ikiepuka gundu ililokuwa nalo Namungo iliyocheza makundi ya michuano hiyo 2020-2021 bila kufunga bao wala kupata pointi, jinamizi lililoendelezwa na Azam FC iliyopo Kundi B ikiwa imeshapoteza mechi mbili hadi sasa.

Katika safari ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Black Stars imeziondoa Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1 na Flambeau du Centre ya Burundi kwa jumla ya mabao 4-2.

Kati ya mabao hayo saba yaliyofungwa na Singida Black Stars, Chama amehusika kwenye matatu, akifunga mawili na kutoa asisti moja. Unaweza kusema Chama ameibeba Singida Black Stars mabegani kwani hadi kufikia hapo, ana mchango wake mkubwa katika kufunga au kutengeneza nafasi za mabao.

CHAM 04

AANZIA KOMBE LA KAGAME

Akiwa na jezi ya Singida Black Stars, Chama alianza kung’ara mapema msimu huu kwenye Kombe la Kagame, mashindano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 2 hadi 15, 2025. Singida Black Stars ilitwaa ubingwa na Chama akabeba Tuzo ya Mfungaji Bora wa mashindano hayo.

Licha ya kukosa mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Ethiopian Coffee, lakini alifunga mabao matatu katika mechi nne zilizofuatia alizocheza dhidi ya Kenya Police, Garde Cotes, KMC na Al-Hilal.

Katika nusu fainali dhidi ya KMC, Singida ilishinda 2-0. Bao la kwanza lilifungwa na Chama dakika ya 45. Andre Cyrille Koffi alihitimisha kwa bao la dakika ya 64.

Kwenye fainali dhidi ya Al-Hilal, Chama aliibuka shujaa. Alifunga mabao yote mawili ya ushindi wa 2-1, dakika ya 19 na la ushindi dakika ya 58, baada ya Al-Hilal kusawazisha kupitia Abdel Raouf dakika ya 31.

CHAM 02 (1)

KIMATAIFA HAKUPOA

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Rayon Sports nchini Rwanda, Chama alipiga faulo iliyozaa bao la ushindi wa 1-0 lililowekwa kimiani na Marouf Tchakei kwa kichwa. Licha ya kutofunga wala kutoa asisti katika mechi ya marudiano dhidi ya Rayon jijini Dar iliyomalizika kwa ushindi wa 2-1, Chama alikuwa sehemu ya kikosi kilichoanza siku hiyo na kuifanya Singida kuvuka.

Dhidi ya Flambeau du Centre, Chama alifunga bao kwenye sare ya 1-1 ugenini nchini Burundi. Kisha akamalizia kazi kwenye marudiano kwa kufunga tena katika ushindi wa 3-1. Singida ikafuzu makundi.

Katika mechi ya kwanza Singida ilipoteza kwa mabao 2-0 ugenini mbele ya CR Belouizdad ya Algeria, huku Chama na mastaa wengine wakipambana kwa jasho na damu bila mafanikio kuepuka kipigo hicho kilichotokana na mabao ya dakika za mapema.

Iliporudi nyumbani, Chama akishirikiana tena na mastaa wenzake akiwamo Khalid Aucho ambayo aliikosa mechi ya kwanza ya makundi na walifanikiwa kuchomoa bao dakika za jioni kwa mkwaju wa penalti ya Tchakei na kuiheshimisha timu hiyo kuepuka aibu ya kufuata nyayo za Namungo.

CHAM 02

BARA KAZI ILEILE

Hadi sasa Singida Black Stars imecheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara. Chama alikosa mechi ya kwanza dhidi ya KMC, baada ya hapo akauwasha dhidi ya Mashujaa na Pamba Jiji.

Katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, licha ya kutoasisti moja kwa moja, lakini mpira wa kona aliopiga ulimkuta Marouf Tchakei ambaye shuti lake lilizuiwa kisha Elvis Rupia akaifungia Singida. Hapo alihusika kwa mbali kidogo.

Katika sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, Chama alifunga bao la Singida kwa mpira wa faulo dakika ya 31. Pamba ikasawazisha dakika ya 50 kupitia Kelvin Nashon.

CHAMA

MECHI 10, MABAO 6, ASISTI 1

Msimu huu hadi sasa Singida Black Stars ikiwa imecheza mechi 12 za mashindano tofauti ambayo Kombe la Kagame (5), Kombe la Shirikisho Afrika (4) na Ligi Kuu Bara (3), Chama amecheza mechi kumi, akihusika kwenye mabao saba kati ya 17 yaliyofungwa na timu hiyo. Amefunga sita na asisti moja.


KAULI YAKE

"Nimefurahi kujiunga na Singida, kwa sasa Singida ni timu kubwa, si Tanzania tu, bali hata nje. Ni muda sasa wa timu kujitambulisha zaidi kimataifa.”

Kuhusu malengo yake, Chama anasema: “Kikubwa naangalia malengo ya klabu kwa sababu ndiyo lengo kuu kwa wachezaji wote, kisha kupitia malengo hayo, mchango wangu utaonekana."