Clara na DNA ya Ronaldo Al Nassr

JUNI 22, 2022 mchezaji nyota wa kike kutoka Tanzania, Clara Luvanga aliposti picha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram akiwa anatazama kitu kupitia darubini ndogo ya mkononi na kuandika maneno yaliyoonyesha namna anavyomkubali supastaa wa Kireno, Cristiano Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or ya mwanasoka bora wa dunia.

Wakati Luvanga anaweka posti hiyo, Ronaldo alikuwa amerejea nyumbani Manchester United akitokea Real Madrid huku Luvanga alikuwa zake Tanzania na hakuwa hata akijua kama inaweza kutokea siku moja akacheza klabu moja na supastaa huyo pamoja na kwamba yeye anacheza soka la wanawake na CR7 kwa wanaume.

Kwenye posti hiyo, Luvanga aliandika maneno yasemayo, "Luvanga CR29 x CR7=☠☠⚽️". Clara alijiona kama CR7 vile na ndio maana hata vifupisho vya majina yake vya "CL" akavibadili kidogo na kuandika "CR" ili kufanana na vya mchezaji huyo ambaye alionyesha wazi kuvutiwa naye.

Nani anaijua kesho? Waswahili hupenda kusema kuwa ni fumbo, muda mwingine ni vizuri kuamini tu kile unachoona kuwa kinawezekana na kuendelea kukipigania pengine Mungu atafungua neema zake juu yako na kufanikisha malengo yako.

Clara ameendelea kung'ara licha ya changamoto nyingi ambazo alikumbana nazo, ikiwemo ile ambayo ilimfanya kutoonekana tena uwanjani kwa kipindi kirefu (ilifichwa) ili kumlinda mchezaji huyo ambaye alikumbana na unyanyasaji mwingi akiwa na timu ya taifa ya wanawake katika ngazi tofauti, wengi wakihisi kuwa ni mwanaume kutokana na mwonekano wake na mambo makubwa ambayo alikuwa akiyafanya uwanjani.

Hata hivyo, viunzi hivyo aliviruka na hatimaye alirejea tena uwanjani akiwa na njaa zaidi ya kukimbizana na ndoto zake na mara hii haikuwa nyumbani tena Tanzania, alipata shavu la kwenda Hispania akitokea Yanga Princess.

Agosti 2023, Luvanga alitia saini ya kujiunga na timu ya daraja la Pili ya Hispania ya Dux Logrono na wakati huo Ronaldo alikuwa ametimiza miezi minane ya kucheza soka la kulipwa Saudia baada ya kufanya uamuzi mgumu wa kuondoka Manchester United kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag ambaye alikuwa akimsugulisha benchi.

Licha ya kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, Clara alianza na moto wake huko Hispania kiasi cha kucheza kwa kipindi kifupi mno ndipo Al Nassr ya wanawake ambayo ilikuwa kwenye ujenzi wa kikosi chake ilipovutiwa na mshambuliaji huyo na kuamua kumsajili.

"Sikuelewa nini kinaendelea zaidi ya kumshukuru Mungu, lilikuwa ni jambo kubwa sana kwangu na familia yangu kupata nafasi ya kwenda Saudia tena katika klabu ambayo kwa wanaume anaichezea Ronaldo," anasema mchezaji huyo.

Kitendo cha Clara kutokea Hispania ambako ligi ilikuwa ikiendelea, kilimfanya kuwa moto wa kuotea mbali na moja kwa moja aliingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya wanawake ya Al Nassr na kugeuka kuwa Ronaldo wao.

Huku Ronaldo alikuwa akikiwasha kwa wanaume kwa kufunga mabao kila uchao, upande wa pili kwenye ligi ya wanawake, Clara naye alikuwa akijibu mapigo kwa kuwapa raha mashabiki wa Al Nassr.

Nyota hao, wakajikuta kila mmoja anakuwa kinara wa mabao upande wake. Clara tayari kazi ameimaliza ambayo ni kuisaidia Al Nassr kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa wanawake, vita iliyosalia mbele yake ni kwenye ufungaji bora ambapo anaongoza akiwa na mabao 11 huku ikisalia michezo miwili.

Kwa upande wanaume, Ronaldo anaonekana kuwa bado na kibarua cha kufanya kutokana na utofauti mkubwa wa pointi (12) uliopo baina ya Al Nassr (56) na Al Hilal (68) ambao wanaongoza msimamo wa ligi hiyo. Kwa wafumania nyavu, Ronaldo anaongoza akiwa na mabao 23, amemzidi mabao matatu Aleksandar Mitrovic wa Al Hilal.


UVUMILIVU UMEJIPA

Haikuwa kazi rahisi kwa Clara kufika Saudia na kati ya mambo ambayo yamembeba ni pamoja na uvumilivu huku akiamini wakati wa Mungu ni wakati sahihi zaidi wa milango kufunguka na kila kitu kuwa sawa.

"Siwezi kusema nimefika hapa kwa akili na uwezo wangu wa kibinadamu, siku zote nimekuwa nikiamini kwenye subira ambayo huendana na uvumilivu," anasema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga Princess na kuongeza;

"Ujue ni ndoto yangu kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania na nashukuru Mungu nimelifanikisha hilo tena nimepata nafasi ya kuwa kwenye moja ya mataifa ambayo kwa sasa yanazungumzwa zaidi kimpira."


WASIKIE WADAU

Kutoka kwenye uwanja wa maoni ya wadau mbalimbali kwa kile ambacho alikiposti miaka miwili iliyopita, Jackson Hatibu aliandika,"Oiii Luvanga unaweza kuanza kuwatazama wapinzani wako wa baadaye kwenye timu za Ufaransa na kwingineko......utafakari namna utawafanya."

Rizzy Mohammed aliandika, "Hatimaye leo unacheza timu moja na Ronaldo, muache Mungu aitwe Mungu @claraluvanga14."



WASIFU WAKE

Jina Kamili: Clara Cleitus Luvanga

Kuzaliwa: Februari 25, 2005 (Umri 19)

Mahali:  Tanzania

Nafasi: Mshambuliaji

Timu: Al Nassr

Jezi: 9