CHAUBAYA - Bondia anayeikumbuka Sh300 ya matenga ya nyanya

Muktasari:
- Sir Nature anawahamisisha vijana katika suala la utafutaji, huku akiwakumbusha kuwa riziki ipo ndani ya miguu yao kama ilivyokuwa kijana wa Kisambaa kutoka Lushoto mkoani Tanga, Kalolo Amiri Chaubaya.
"RIZIKI ni popote mtu wangu zidisha, piga kwata. Na ofisi ni miguu yako tafuta utapata." Hiyo ni moja kati ya mistari iliyopo katika wimbo wa Ofisi ni Miguu ulioimbwa na mkongwe wa Bongo Fleva, Juma Kassim Kiroboto ambaye wengi wanamfahamu kama Juma Nature au Sir Nature akiwashirikisha Manzense Crew.
Sir Nature anawahamisisha vijana katika suala la utafutaji, huku akiwakumbusha kuwa riziki ipo ndani ya miguu yao kama ilivyokuwa kijana wa Kisambaa kutoka Lushoto mkoani Tanga, Kalolo Amiri Chaubaya.
Huenda akawa hana jina kubwa miongoni mwa mabondia wa ngumi za kulipwa nchini, lakini ni mmoja kati ya wanaotazamwa kwa jicho la tatu kutoka ndani ya akademi bora ya ngumi nchini, Mafia Boxing Gym kutokana na kuendelea kufanya vizuri huku akiweka alama kwenye mchezo huo.
Kalolo ambaye kwa sasa anamilikiwa na Mafia Boxing Gym ambao wanamiliki promosheni kubwa ya Mafia Boxing Promotions wakiwa na rekodi ya kuasisi kaulimbiu inayotumika kwenye mapambano yao ya "Knockout ya Mama", amekuwa mwiba kwenye uzani wa Super bantam.
Bondia huyo anashikilia mkanda wa ubingwa wa PST Tanzania huku akifanikiwa kuutetea mara moja dhidi ya Sihle Jelwana wa Afrika Kusini katika pambano la Knockout ya Mama ambalo lilifanyika Desemba 26, mwaka jana, kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mtandao wa Boxrec ambao unatumika kuhifadhi taarifa za mabondia, Kalolo yupo kwenye nafasi saba katika 10 bora ya mabondia wote Tanzania 'Pound 4 Pound' wakati kwenye uzani wake wa bantam akiwa anakamata nafasi ya tatu katika mabondia 51 akiwa na hadhi ya nyota mbili na nusu.
Bondia huyo ambaye anakamata nafasi ya 47 duniani katika mabondia 1133 wa uzani wake akiwa na mapambano 12, ameshinda 11 kati ya hayo sita kapiga watu kwa Knockout na sare mara moja huku akiwa hajawahi kupigwa na uwezo wake wa kushinda kwa Knockout ikiwa ni asilimia 54.
Kalolo ambaye alianza kucheza ngumi za kulipwa 2023, amefanya mahojiano na Mwanaspoti juu ya safari yake katika mchezo huo hadi kufikia hatua ya kuwa bingwa wa PST Tanzania kwenye uzani huo nchini.
Pia, anasimulia safari yake ya maisha hadi kuwa bondia wa ngumi za kulipwa akitokea Lushoto mpaka Tanga mjini kwa mama yake ili kutafuta maisha baada kushindwa kuendelea na elimu ya misingi akiwa darasa la nne kutokana na ugumu wa maisha.
"Shule nimeishia darasa la nne kwa sababu ya mazingira. Kipindi ambacho nasoma nilikuwa Lushoto. Unajua ukiwa unasoma shule unatakiwa uwe na mtu anayekuangalia kwa kila kitu kuanzia vifaa vya shule hadi chakula, lakini upande wangu ilikuwa tofauti," anasema bondia huyo.
"Lakini upande wangu hata aliyenipeleka shule simkumbuki alikuwa ni nani, alinipeleka shule kunikabidhi kisha akaondoka zake. Sikumuona tena ilifika wakati nilikuwa naenda shule na mfuko wa rambo.
"Sikuwa na sapoti yoyote ndiyo tatizo la kuacha shule. Nilikuwa nakaa kwa dada yangu ukirudi nyumbani unakuta umewekewa chai na chapati za jana zimekatwa kwa mtindo wa vipande vya mkate. Niliona siwezi kuishi maisha yale shule ilivyofungwa nikaelekea zangu Tanga kwa mama na shule sikurudi tena hadi jina langu likafutwa.
"Lakini siyo kwamba sikupenda shule, ila aina ya maisha niliyokutana nayo ndiyo yalinilazimisha niache shule na sababu ya kuelekea Tanga mjini kwa ajili kutafuta maisha."
SWALI: Tanga mjini ukawa unafanya shughuli gani?
JIBU: "Nilikuwa nafanya kazi ya kubeba mzigo katika soko la Mgandini. Nilikuwa nabeba masunduku ya nyanya, magunia ya viazi.
"Kuhusu kipato ukweli kilikuwa kigumu kwa sababu sanduku moja la nyanya nilikuwa nalibeba kwa Sh300. Kipato kilikuwa tofauti kwa sababu kwa siku naweza nikabeba mizigo mitano siku nyingine 10 ambayo pesa yote inakuwa Sh3,000 na hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu."
SWALI: Changamoto ilikuwa kitu gani kwenye kazi yako?
JIBU: "Kwanza ulikuwa umbali wa kutoka sokoni hadi barabarani, ilikuwa inachukua hadi nusu saa halafu muda wa kwenda ilikuwa asubuhi huku kula yangu ilitokana na kubeba mizigo, yaani nakula halafu ndiyo nitalipa baada ya kufanya kazi. Mara nyingi nilikuwa nakula mchana peke yake.
"Nitakula Sh1,000 mchana usiku nitanunua maandazi Sh500 halafu Sh1,500 naweka kwa kuwa nilipanga chumba...chai ya asubuhi nilikuwa siipati.
"Nilikuwa naweka (pesa) kwa sababu nilikuwa naishi kwenye nyumba ya kupanga japo kuwa baba na mama yangu walikuwa Tanga ingawa kwa historia niliyopewa na mama kwamba mzee alitengana na mama wakati nikiwa mdogo."
SWALI: Kitu gani kilikufanya uingie kwenye ngumi na kuacha kubeba mizigo?
JIBU: "Wakati nabeba mizigo niliwahi kuona pambano moja liliandaliwa na promota Ali Mwazoa alikuwa akicheza Allan Kamote. Ngumi nilikuwa sifuatilii na wala sikuwa na mpango wa kucheza ngumi.
"Nakumbuka nilikuwa nimekaa mabanda ya papa nikaona jalamba la michango linapitishwa kuangalia anayepigana ni Kamote. Nikaenda kuangalia pambano lake kule ndiyo nikaona wapo hadi kina Ibrahim Mafia. Nikajiuliza mbona wengine wadogo na wanapigana?
"Sasa baada ya kutoka hapo ndiyo nikaanza kutafuta sehemu za kufanya mazoezi na makocha. Nikakutana na kocha Hamadi akaanza kunifundisha, lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda ndiyo nikakutana na kina Kamote.
"Kamote ndiyo aliniambia niende kwenye gym yao nikajifunze akanishika mkono hadi Tangamano (Tanga) kuna gym kubwa ya kwao. Nikawa nafanya mazoezi hadi wakanichomeka kwenye mapambano ya fidhaa wakati huo bado naendelea kubeba mizigo.
"Unajua asubuhi nilikuwa sokoni nabeba mizigo jioni mazoezini hadi watu wa sokoni wakawa wananisema kwamba ngumi haziwezi kunipeleka popote, niendelee na kazi ya kubeba mizigo, lakini niliendelea kufanya (mazoezi) na mpango wangu wa kucheza ngumi huku nabeba mizigo.
"Nikawa nacheza ngumi za ridhaa naumia, lakini sina sapoti yoyote. Kuna siku kidole kikashtuka, kilipinda nikapiga hesabu ya hospitali ikawa haiwezekani kwa sababu sikuwa na pesa na watu ambao nawategemea walishaniambia niache ngumi.
"Binafsi sikutaka kuacha nikawa naendelea kwa sababu nilishacheza mapambano mengi ya ridhaa. Nikaendelea na mazoezi ila nilikuwa siwezi kwenda 'road work' asubuhi kwa sababu ya kazi zangu za kubeba mizigo.
"Lakini nashukuru Mungu kuna siku nilikutana na kiongozi wa Mafia, meneja Anatoli Wanah, sababu iliwekwa 'spearingi' kwa kocha Hamisi Mwakinyo kwao nikapewa Ibrahim Mafia tupigane raundi 10. Nilicheza vizuri.
"Kiukweli wakanishika mkono Mafia hadi leo nipo chini yao nafanya vizuri. Sifikirii kubeba mizigo tena nafikiria kucheza ngumi."
SWALI: Pambano gani ambalo huwezi kulisahau?
JIBU: "Nakumbuka kuna mapambano nilicheza na bondia Joshua David aliandaa promota Ali Mwazoa. Nilimpiga sana mpinzani wangu. Pambano likawekwa la marudiano tukatoka sare.
"Nadhani pambano lingine lilikuwa na Thato Bonokane.
Nilicheza mwaka jana katika pambano la 'Knockout ya Mama'. Thato ni bondia mkubwa mwenye rekodi kubwa maana ameshachukua mikanda mikubwa na nilitegemea kushinda knokout kutokana na maandalizi yangu, lakini pambano liliisha kwa pointi, hivyo siwezi kusahau."
SWALI: Baada ya miaka mitatu unajiona wapi?
JIBU: "Baada ya miaka mitatu chini ya usimamizi wa menejimenti yangu ya Mafia Boxing Promotions naamini nitakuwa mbali kwa sababu kuna mipango mikubwa inafanyika.
"Lakini nashukuru Mungu maendeleo nayopata sasa hivi sikuwahi kuhisi kama naweza kupata, maana mimi ndiyo Msambaa wa kwanza kuwa na kiwanja Dar es salaam na siyo kimoja yote ni sababu ya Mafia Boxing Promotions.
"Mipango mingine ambayo ipo kama nitaweza kufanya vizuri mwaka huu, basi nitapewa gari, ila jambo kubwa ambalo natamani ni kuja kuleta mikanda mikubwa Tanzania. Ndoto yangu siyo kuishia hapa nataka niende mbali zaidi kwa kuleta mikanda mikubwa.
SWALI: Wale waliokushauri uache ngumi sasa wanasemaje?
JIBU: "Sasa wanakubali nachofanya na wamekuwa wakinipa sapoti kubwa. Nawashukuru na wengine wamekuwa wakiomba niwasaidie mambo yao, lakini nimekuwa nikiwaambia bado najitafuta, nikifikia wakati wa kutoa basi siwezi kuwaacha japokuwa pesa za vocha ni kawaida, ila bado nawashukuru na wasichoke kuniunga mkono.
SWALI: Vipi kuhusu baba ambaye alikuacha mdogo na mama ila sasa una jina (kubwa)?
JIBU: "Kwanza yule mzazi wangu huenda pasipo yeye asingekuwepo. Nashukuru kwa sasa ananipa sapoti kubwa na pia namsapoti maana hata pambano langu la 'Knockout ya Mama' alikuja kuangalia na kunitia moyo, siwezi kufanya yaliyopita wakati wake.
"Lakini jambo ambalo siwezi kulisahau ni kwamba nimetoka mbali, sasa hivi naweza kumhudumia mama yangu kwa sababu kwake mimi ndiyo kila kitu. Siwezi kuacha kuushukuru uongozi wa Mafia umenibadilisha pakubwa sana."
Umejiandaa vipi na KO ya Mama Februari 22?
"Ninavyoongea na wewe muda huu ndiyo nimeingia kambini rasmi huku Kisarawe kwa ajili ya pambano la Februari 22, mwaka huu ambalo tutacheza Magomeni kwenye Ukumbi wa City Centre, mpinzani wangu Mussa Kananji kutoka Malawi ajipange," anasema Kalolo.