CHAN 2009; KIKWETE ALIVYOWASHANGAZA WASAIDIZI WAKE

KATIKA marais wote waliopita wa Tanzania, hakuna asiyekuwa shabiki wa wazi wa michezo kumzidi Rais Jakaya Kikwete; Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Tanzania. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipenda michezo ya jadi na sanaa nyingine kama ushairi na sanaa za maonyesho.

Mzee Ali Hassan alikuwa mpenzi wa mchezo wa soka, ingawa sio kwa kiwango cha Jakaya. Mchango mkubwa wa Rais Benjamin Mkapa kwenye michezo ulikuwa ni kutuachia uwanja wenye jina lake ambao awali ulifahamika kama Uwanja wa Taifa.

Wakati tukifanya tafakari ya mashindano ya Chan ya mwaka 2009, ni muhimu pia kutazama mchango wa mtu aliyekuwa akishikilia nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini Tanzania wakati huo.

Hii ni kwa sababu, kama samaki huanzia kuoza kwenye kichwa, maana yake ni kwamba jambo zuri au baya kwa nchi mara nyingi huanzia katika ngazi za juu.

Katika gazeti la MwanaSpoti la jana, tuliona namna Rais Kikwete alivyosaidia kuletwa kwa aliyewahi kuwa kocha Taifa Stars, Marcio Maximo kutoka kwao Brazil; kuja kufanya kazi Tanzania.

Ni Kikwete ndiye aliyemwambia aliyekuwa balozi wa Brazil kusaidia kuleta kocha kutoka taifa hilo. Hata hivyo, Kikwete hakuanzia hapo.

Tukio la kwanza la Kikwete

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambao Kikwete alishinda kwa ushindi wa zaidi ya asilimia 80, wasaidizi wake walianza kuandaa hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Tisa lililoongozwa na Samuel Sitta.

Walipomaliza hotuba kuiandaa, walimpelekea bosi wao kuona kama ina vitu vyote alivyotaka viwe kwenye hotuba na kama anaweza kufanya marekebisho yoyote. Alichokifanya, kiliwashangaza wasaidizi wake.

“Alipoirudisha kwetu, ilikuwa na ‘section’ nzima kuhusu michezo. Katika hotuba yetu tuliyomwandalia, tuligusa maeneo mengi lakini hatugusa michezo kabisa. Kwa hiyo, ukiona eneo la michezo katika hotuba ya ufunguzi wa Bunge, ujue hilo ni eneo ambalo aliliweka yeye mwenyewe. Hilo linaweza kukupa picha ya ni kwa namna gani Rais Kikwete alikuwa anapenda michezo,” ameniambia Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa wasaidizi wa Rais Kikwete.

Ni katika hotuba hiyo ambapo Rais Kikwete alizungumzia kuhusu maumivu yake kwa timu za Tanzania kufanya vibaya katika michezo na kuahidi kwamba atakuwa tayari kumlipa mshahara kocha mkuu wa Taifa Stars na michezo mingine ili wapatikane walimu wataalamu wa kufanya kazi hizo.

Kwa sababu hiyo, ujio wa Maximo usingewezekana pasipo Kikwete na kwa maana hiyo mafanikio ya timu yaliyopatikana wakati huo yana mkono wake wa moja kwa moja.

Ilisaidia pia kwamba urais wa Kikwete ulikwenda pamoja na kuchaguliwa kwa Leodger Chilla Tenga kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Tenga ni mmoja wa wanamichezo wenye heshima kubwa hapa nchini. Fomu yake ya kugombea uongozi wa TFF alienda kuchukuliwa na kundi la wadau wa soka wakiwamo waandishi wa habari walioamini kwamba yeye anaweza kuwa kiongozi mzuri wa soka.

Tenga ni mhandisi kitaaluma, lakini alipata umaarufu mkubwa akiwa mchezaji wa soka katika klabu za Tanzania na pia kuwa nahodha wa Taifa Stars katika miaka ya nyuma. Wakati anaingia TFF, taasisi hiyo ilikuwa imetoka kuwa katika uhusiano usioridhisha na wadau mbalimbali ikiwamo serikali na wadhamini, na wadau walikuwa wamechoshwa na migogoro, majungu na fitina zilizokuwa zimetawala soka la Tanzania.

Kikwete alikuwa anamfahamu Tenga miaka 30 kabla hawajajikuta katika nafasi walizokuwa nazo wakati huo. Tenga pia alikuwa anamfahamu miaka mingi nyuma. Zilikuwepo tofauti za kimsingi baina ya wawili hao hasa kuhusu utendaji na vipaumbele, lakini ilikuwa bahati kwamba katika wakati mmoja, Rais wa nchi na yule wa TFF walikuwa ni watu wenye uelewa mpana, wanaojua michezo na waliokuwa wanakubalika kwa wadau.

Nguvu kubwa ya Tenga ilikuwa ni kwenye kuwapa watendaji nguvu kubwa za kimaamuzi.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF wakati wake, Frederick Mwakalebela alipewa mamlaka ya kiutendaji ya kutekeleza majukumu yake.

TFF ikaja kuwa na Ofisa Habari, Boniface Wambura, aliyekuwa akitoa taarifa za shirikisho karibu kila siku na ziliundwa kamati za TFF zilizokuwa zikishughika na masuala ya fedha, maadili, nidhamu, mashindano na mambo mengine.

Kwa hiyo, Tenga anaweza kusemwa kwamba ndiye mtu aliyeitengeneza TFF kuwa taasisi kwa namna ilivyo leo. Huko nyuma, enzi za kina Muhidin Ndolanga na wengine wakati huo TFF ikifahamika kama Chama cha Soka Tanzania (FAT), lilikuwa ikionekana kama taasisi ya mtu mmoja ambaye mambo mengi yalianzia na kuishia kwake. Katika miaka ya 1990 na hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati redio binafsi ziliporuhusiwa, ilikuwa kawaida kumsikia Ndolanga akijibishana redioni na waliokuwa watangazaji maarufu wa vipindi vya michezo wakati huo kama vile Abdallah Majura, Aboubakar Liongo na Maulid Kitenge.

Hakukuwa na nafasi ya kufanya hivyo kwa Tenga kwa sababu Wambura au Mwakalebela ndio waliokuwa wakitoa taarifa. Mfano huo wa TFF ulitokana na mwongozo wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kutaka timu na mashirikisho kuajiri wanataaluma wa masuala ya sheria, masoko na habari kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kila siku za mpira.

Kwa hiyo, wakati leo unawaona kina Haji Manara na Antonio Nugas wakitamba katika redio, mitandaoni na magazetini, chanzo chake ni wakati wa utawala wa kina Tenga.

Malipo ya makocha

Katika muda wote wa miaka minne ya Maximo kufundisha Tanzania, serikali ya Rais Kikwete ilikuwa ikimlipa mshahara yeye na msaidizi wake, Itamar Amorin aliyekuwa mwalimu wa viungo. Umekuwa ni utaratibu wa Maximo kuwa na walau Mbrazi mwenzake mmoja wakati anapopata kazi ya kufundisha. Mwaka juzi, alipata kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Guyana aliko sasa na amekwenda na msaidizi mwingine kutoka nchini kwake.

Kikwete pia alikubali kumlipa mshahara kocha wa timu ya taifa ya Netiboli kutoka Australia ambaye pia alinyanyua kiwango cha Tanzania katika mchezo huo kiasi cha kufikia kwenda kushindana katika mashindano ya kimataifa.

Somo kubwa katika tafakari ya Chan kwa mwaka 2009 ni kwamba ni mara chache sana mafanikio katika michezo huja pasipo ushirikiano wa kutosha baina ya wadau wa pande tatu yaani serikali, FA na wadau wa michezo kama vile wadhamini na taasisi nyingine.

Mafanikio ya Stars pia yalitokea kwa sababu ya udhamini wa kampuni ya Serengeti wakati ule.

Kwa mujibu wa Mwakalebela, Stars iliondoka kwenda Ivory Coast ikiwa na fedha za kutosha kiasi kwamba iliweza kujigharamia kwa gharama za ziada zilizojitokeza wakati ikiwa kule.

Kuna siku Stars ilijikuta imevaa jezi sawa na wapinzani wake na kwa sababu yenyewe ilipangwa kama timu ya ugenini, iibidi zitafutwe jezi mpya katika kipindi kifupi na zilipatikana kwa sababu TFF haikuwa na shida za kifedha wakati huo.

Je, unajua kina waliokuwa wachezaji muhimu wa Stars wakati huo na kwanini? Pia nini kilikuwa kinatokea uwanjani, nini wachezaji walikumbana nacho na kwa namna gani walipmbana na changamoto zilizokuwapo? Usikose kesho...!

ITAENDELEA


Imeandikwa na Ezekiel Kimwaga