Championship mechi nne za uamuzi mgumu

Muktasari:

  • Kuanzia katika vita ya kupanda Ligi Kuu na ile ya kupigania kutoshuka daraja, hakuna wepesi kutokana na kuhusisha timu nyingi ambazo zimepishana tofauti ndogo ya pointi hadi sasa wakati ligi hiyo ikiwa imetimiza raundi 26.

Kwa hatua iliyofikia, Ligi ya Championship inalazimisha kila timu kukaa mkao wa kula vinginevyo itajikuta ikiishia kutazama wengine wakimaliza kwa shangwe msimu huu.


Kuanzia katika vita ya kupanda Ligi Kuu na ile ya kupigania kutoshuka daraja, hakuna wepesi kutokana na kuhusisha timu nyingi ambazo zimepishana tofauti ndogo ya pointi hadi sasa wakati ligi hiyo ikiwa imetimiza raundi 26.


Timu tano zinazoshika nafasi za juu kila moja ina nafasi ya kupanda Ligi Kuu moja kwa moja kutegemeana na nafasi ambayo ipo na idadi ya pointi ambazo imeachwa na wapinzani wao kulingana na msimamo wa ligi ulivyo.


Ken Gold ndio kinara ikiwa na pointi 60, Pamba ipo nafasi ya pili na pointi zake 55, nyuma yake zikiwepo Biashara United na Mbeya Kwanza ambazo kila moja ina pointi 53 wakati huo TMA iko nafasi ya tano ikiwa na pointi 51.


Ushindi katika mechi moja na sare mbili katika mechi nne ambazo KenGold imebakiza ni matokeo ambayo yataifanya  kutinga Ligi Kuu msimu ujao, lakini hata ikipata ushindi katika mechi mbili itajihakikishia tiketi ya kuwepo kwenye daraja hilo la juu zaidi kwa ligi za soka nchini.


Lakini ukiondoa Ken Gold, Pamba, Biashara United, Mbeya Kwanza na TMA kila moja ina kibarua kigumu cha kusaka nafasi ya kupanda moja kwa moja kwa kuhakikisha inapata ushindi kwenye mechi zake, huku ikilazimika kuombea mabaya kwa wengine.

MECHI ZA KIBABE
Kinara KenGold imebakiza mechi nne ambazo ni dhidi ya Mbuni na TMA ambazo itacheza ugenini na mbili za nyumbani dhidi ya FGA Talents na Polisi na Pamba ina mbili za nyumbani dhidi ya Polisi na FGA na ugenini ni dhidi ya TMA na Mbuni.


Biashara United iliyopo nafasi ya tatu,ina mechi dhidi ya Green Warriors na Cosmopolitan na ugenini ni Transit Camp na Pan African na Mbeya Kwanza imebakiza moja tu ugenini dhidi ya Cosmopolitan na ina tatu nyumbani dhidi ya Pan African, Green Warriors na TMA imesalia na mechi tatu ugenini dhidi ya Copco na tatu ugenini dhidi ya Mbeya City na KenGold.


Mechi mbili zinaonekana kuwa ngumu zaidi na pengine zikachangia kuamua hatima ya timu katika mbio za mwishoni za kuwania kupanda daraja.


Michezo hiyo ni baina ya TMA na KenGold na mwingine ule wa TMA dhidi ya Pamba hmbazo zitachezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Ushindi wa mechi hizo kwa TMA unaweza kuwezesha ipande Ligi Kuu au kucheza hatua ya mtoano ya kusaka nafasi kwenye ligi (play off) lakini pia kinyume chake, matokeo mazuri katika mechi hizo yanaweza kuzibeba KenGold na Pamba.


Cosmopolitan kuamua wababe Arusha
Kitendo cha Pamba na KenGold kuwa na mechi mbili ambazo zitacheza Arusha, kinafanya jiji hilo kuwa katika nafasi nzuri ya kuamua timu ipi inapanda au inakwama kati ya vinara hao wawili wa msimamo.


Mechi dhidi ya TMA inaonekana zinaweza kuwa ngumu zaidi kwa Pamba na KenGold ikiwa muda ambao zitacheza, wenyeji bado watakuwa na uwezekano wa kupanda. Timu ya Cosmopolitan nayo ina nafasi kubwa ya kuamua mbio wa kusaka kupanda Ligi Kuu kwa vile ina mechi mbili dhidi ya Mbeya Kwanza na Biashara United ambazo nazo zipo kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi ya Championship.


RUVU SHOOTING MIUJIZA TU
Maajabu ya ngamia kupenya tundu la sindano ndio pekee yanayoweza kuiokoa Ruvu Shooting iliyopo mkiani mwa msimamo wa ligi kubaki Championship kwani uwezekano nii finyu.


Hadi sasa Ruvu Shooting inashika mkia ikiwa na pointi 11 ambazo ni nne pungufu ya zile za Pan African iliyopo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 15.


NANE ZANUSURIKA
Timu nane kati ya 15 zinazoshiriki ligi ya Championship, hazipo katika nafasi za chini wale katika nafasi za hatari zinazowaweka katika uwezekano wa kushuka daraja.


Uwepo wa mechi zinazokutanisha timu zilizo nafasi za chin, unaziweka salama KenGold, Pamba, TMA, Mbuni, Biashara United, Mbeya Kwanza, Mbeya City na Polisi Tanzania kubaki Championship.

HESABU NZITO
Kocha wa Pamba, Mbwana Makata alisema kuwa kwa sasa wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi zao zote nne zilizobakia.


“Ligi ilipofikia ni pagumu na namna pekee ya kupanda Ligi Kuu ni kupata ushindi katika michezo yetu minne iliyobaki. Ni mechi ngumu lakini tuna imani tukijiandaa vyema tutamaliza vizuri,” alisema.


Kocha wa TMA, Maka Malwisi alisema  hawakati tamaa na watahakikisha wanapambana vilivyo mechi zilizobaki wakiamini wanaweza kumaliza juu.