Chama la bure kabisa

LONDON
ENGLAND


DIRISHA la uhamisho wa majira ya baridi limeshafungwa mwezi uliopita tu hapo, lakini makocha tayari tayari wameshaanza kukuna vichwa juu ya mastaa wapya wanaohitaji saini zao kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye ishu hiyo ya usajili kuna mastaa kibao ambao wamebakiza miezi michache tu kuachana na klabu zao wanazochezea kwa sasa kutokana na mikataba yao kuelekea ukingoni na kwamba itamalizika mwishoni mwa msimu.

Mastaa hao kwa sasa wanaweza kusaini mkataba ya awali na timu wanazohitaji wakisubiri ifike Julai Mosi ili kwenda kujiunga na timu hizo kwa uhamisho wa bure.

Lionel Messi, Sergio Aguero, Sergio Ramos na David Alaba ni baadhi ya masupastaa wa nguvu kwenye soka ambao mikataba yao itakwisha mwishoni mwa msimu huu na watakuwa wachezaji huru kwa ajili ya kunaswa bure kabisa.

Katika mchakato huo, hiki hapa kikosi matata kabisa cha mastaa unaweza kuwanasa bure kabisa na ukatamba kwenye soka na kubeba mataji kibao...


Gianluigi Donnarumma - kipa

Umri wake ndo kwanza miaka 22, kipa Mtaliano, Gianluigi Donnarumma amekuwa mchezaji muhimu kweli kweli kwenye kikosi cha AC Milan, ambako amecheza kwa miaka mitano hadi sasa.

Lakini, mkataba wa kipa huyo utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na tayari inaonekana kama vile maisha yake ya San Siro yanaelekea ukingoni huku Manchester United wakihusishwa na mpango wa kunasa saini yake.

Akiwa na uwezo wa kucheza kwa miaka 10 au 20 zaidi kutoka sasa, Donnarumma utakuwa usajili wa karne kama kutakuwa na timu itakayopata bahati ya kunasa huduma yake bura kabisa mwishoni mwa msimu huu.


Elseid Hysaj - beki wa kulia

Beki huyo wa Napoli, Elseid Hysaj, 27, kwa muda mrefu sana amekuwa kwenye rada za klabu za Ligi Kuu England, hususani Chelsea na Manchester United, ambazo zote zilionyesha dhamira ya kutaka saini yake mwaka 2018.

Hata hivyo, bei aliyokuwa akiuzwa beki huyo ilikwamisha uhamisho wake na tangu wakati huo timu zilikaa kimya kumfukuzia kabla ya sasa akielekea mwisho kabisa katika mkataba wake huko Naples.

Baada ya kukimbizwa na bei, beki huyo wa kimataifa wa Albania, aliyecheza mechi 55 za kimataifa, sasa anapatikana bure kabisa itakapofika mwisho wa msimu huu, hivyo timu hiyo zinaweza kunasa huduma yake.


Juan Bernat - beki wa kushoto

Beki wa kushoto Mfaransa, Juan Bernat, 27, mwisho wa msimu huu mkataba wake huko Paris Saint-Germain utafika tamati na hakuna uwezekano wowote wa mkali huyo kuongeza muda wake wa kubaki kwenye kikosi hicho.

Bernat alicheza mechi tatu tu msimu huu kwenye Ligue 1 kabla ya kupata majeruhi ya mguu.

Beki huyo yupo kwenye hatari ya kukosa msimu wote, lakini klabu hiyo bado ina matumaini ya kuvuna huduma bora kutoka kwake nkwa mechi chache zilizobaki kama atarudi uwanjani na kutamba tena endapo kama atakuwa hajaathirika ubora wake kutokana na kuwa majeruhi. Kama hatasaini dili jipya, basi Juan atakuwa mmoja wa mastaa watakaopatikana bure kabisa mwishoni mwa msimu huu.


Sergio Ramos - beki wa kati

Mmoja kati ya masupastaa wawili kwenye beki ya kati wanaounda kikosi hiki matata kabisa. Sergio Ramos, 34, ameripotiwa kujifungia kwenye mazungumzo na mabosi wa Real Madrid kwa ajili ya dili jipya.

Lakini, shida inakuja sehemu moja tu, Ramos anataka aongezwe miaka miwili kwenye mkataba mpya na mshahara wake ubaki vilevile, lakini Los Blancos hawapo tayari kutoa ofa kama hiyo kwa mchezaji aliyezidi umri wa miaka 30 na kwamba wao ofa yao ni ya mwaka mmoja tu.

Madrid wanamtaka Ramos abaki Bernabeu hadi anastaafu, hivyo wanaweza kubadili mtazamo wa sera yao, lakini kuna klabu kibao zinazosikilia suala hilo na zimejiandaa kumnasa bure beki huyo itakapofika mwisho wa msimu huu. Timu zinazoripotiwa kutaka saini ya mchezaji huyo ni Paris Saint-Germain na Manchester United.


David Alaba - beki wa kati

Supastaa wa Bayern Munich, David Alaba 28, ataachana na miamba hiyo ya Bundesliga mwishoni mwa msimu huu wakati mkataba wake utakapofika tamati baada ya mabosi wa klabu yake kushindwa kumshawishi abaki kikosini.

Alaba amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Real Madrid, huku klabu nyingine vigogo vikihitaji saini yake kama Manchester City, Chelsea na Liverpool.

Staa huyo wa kimataifa wa Austria bado ana mambo mengi anayoweza kufanya ndani ya uwanja, huku akiwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi ikiwamo kiungo mkabaji, beki wa kati, beki wa kushoto na wakati mwingine kwenye kiungo ya kati. Alaba ni kiraka, hivyo ukiwa na huduma yake kwenye kikosi anakupa machaguo tofauti.


Georginio Wijnaldum - kiungo wa kati

Supastaa wa Liverpoo, Mdachi Georginio Wijnaldum, 30, moyo wake umeshaamua kwenda kujiunga na Barcelona mwishoni mwa msimu huu.

Mabosi wa Anfield wamejiandaa kukabiliana na hali ya halisi baada ya jitihada zao za kumbakiza kiungo huyo kwenye kikosi chao kwa maana ya kumpa mkataba mpya kuonekana kugonga mwaka.

Hata hivyo, chochote kinaweza kutoka kwa kiungo huyo wakati mkataba wake ukielekea kufika ukingoni, huku majariwa ya kubaki au kutobaki kwenye kikosi cha Liverpool kutategemea na kile kitakachotokea huko Barcelona. Wijnaldum amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Jurgen Klopp huko Anfield, akiimarisha timu hiyo kwenye safu yake ya kiungo.


Angel Di Maria, kiungo wa kati

Supastaa kiungo mshambuliaji Angel Di Maria, 33, amekuwa kwenye kiwango moto kwelikweli tangu alipoachana na Manchester United na kwenda kujiunga na Paris Saint-Germain mwaka 2015. Mabingwa wa Ligue 1 wamejipanga kumwongezea mkataba mpya aendelee kubaki kwenye kikosi chao, huku mkewe staa huyo wa Argentina akisema kwamba atamshawishi mumewe abaki kwenye timu hiyo kama Lionel Messi atahamia Paris.

Lakini, baada ya mabao 86 katika mechi 246 alizocheza Di Maria akiwa na kikosi cha PSG na kufanikiwa kubeba mataji 12, hiyo inaweza kuwa ni mwisho wa mkali huyo wa zamani wa Real Madrid na kuamua kwenda zake kwingineko kujaribu bahati yake na kumalizia maisha ya soka.


Florian Thauvin - winga wa kulia

Winga huyo wa zamani wa Newcastle United, Florian Thauvin, 28, alirudi Marseille - mwanzoni ilikuwa kwa mkopo mwaka 2016 na tangu wakati huo amekuwa kwenye kiwango bora kwelikweli.

Ubora wake wa uwanjani umemfanya Thauvin kupata nafasi ya kuitumikia timu ya taifa ya Ufaransa kwenye mechi 10 na kufunga mabao 61 katika mechi 140 alizocheza kwenye Ligue 1, huku mabao sita akiwa ameyafunga katika mechi 18 alizocheza msimu huu.

Licha ya kuwa kwenye kiwango bora, mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2018, Thauvin anajiandaa kuachana na Marseille mwishoni mwa msimu huu kutokana na mkataba wake kufika tamati mwishoni mwa msimu huu, huku timu kibao zikihitaji saini yake ikiwamo Leicester City.


Memphis Depay - winga wa kushoto

Supastaa wa Kidachi, Memphis Depay mambo yake hayakuwa poa alipokuwa kwenye kikosi cha Manchester United huko Old Trafford, lakini amekuwa moto kwelikweli tangu alipojiunga na Olympique Lyon.

Kiwango bora anachokionyesha kwenye soka la Ufaransa liliifanya Barcelona kuhitaji huduma yake kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini dili hilo lilishindwa kukamilika.

Depay, 27, mkataba wake unakwisha mwisho wa msimu huu na kuna uwezekano akaachana na Lyon, huku safari ya Nou Camp ikipewa nafasi kubwa kwenda kuungana na kocha Mdachi mwenzake, Ronald Koeman.

Ukiweka kando ishu ya Barcelona, kiwango cha Depay alichoonyesha kwa miaka mitatu na nusu huko Ufaransa kimefungua njia kwa timu nyingi zinazotaka saini yake, ikiwamo mabingwa wa soka wa Italia, Juventus.


Lionel Messi - mshambuliaji

Pengine utakuwa unaishi kwenye miamba ndo usifahamu kwamba supastaa wa Barcelona, Lionel Messi mkataba wake unafika tamati mwishoni mwa msimu huu.

Gwiji hilo la Argentina, Messi mwenye umri wa miaka 33, alikaribia kuachana na Barcelona kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana, lakini aliamua kubaki Nou Camp kumalizia mwaka wa mwisho kwenye mkataba wake.

Hata hivyo, baada ya mkataba wa Messi kuvuja kwa kile alichokuwa akivuna huko Barcelona hilo limefanya timu vigogo tu wenye pesa za maana ndiyo wanaohangaika kutaka huduma yake. Manchester City na Paris Saint-Germain ndizo zinazotajwa kwamba zinakwenda jino kwa jino kwenye kunasa huduma ya mshambuliaji huyo.


Sergio Aguero - mshambuliaji

Baada ya kutamba kwa muongo mmoja huko Etihad, straika Sergio Aguero hatimaye anaweza kuachana na Manchester City mwishoni mwa msimu huu.

Staa huyo wa Kiargentina mwenye umri wa miaka 32 kwa sasa, kwa msimu huu mambo yamekuwa yamekuwa magumu akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara na maradhi mengine.

Hata hivyo, ataaondoka akiwa amefunga mabao 256 katika mechi 380, akibeba ubingwa wa Ligi Kuu England mara nne na pengie mwisho wa msimu huu atabeba taji jingine la England kabla ya kufungua mlango wa kutokea kutokana na mkataba wake kufika mwisho. Man City bado haina makali kwenye fowadi yake, licha ya Gabriel Jesus kujaribu kufurukuta. Kutokana na hilo ndio maana Man City wamekuwa wakihusishwa na Lionel Messi, ambaye atakuwa huru pia mwishoni mwa msimu.