Prime
CARLOS: Hivi ndivyo dili la Kibu Yanga lilivyokuwa

Muktasari:
- "Hizo zilikuwa ni propaganda tu Kibu alikuwa tayari amesaini mkataba na Simba na nakumbuka akiwa Norway walikuwa wanataja kuwa atatambulishwa na Yanga Wiki ya Mwananchi"
- "Siku zote nimekuwa nikizungumza wazi kuwa ni shabiki wa Simba. Licha ya kufanya kazi na Yanga"
JANA katika mahojiano na Carlos Sylivester 'Mastermind' ambaye ni meneja wa mastaa kibao wanaocheza Ligi Kuu Bara alizungumzia mambo mengi, ikiwamo maisha na ofa zinavyomfuta nahodha wa Simba, Mohammed Tshabalala, leo anagusia ishu za straika wa timu hiyo, Kibu Denis na nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto... fuatana naye!
KIBU KWENDA YANGA
Dirisha kubwa la usajili lililopita kulikuwa na tetesi nyingi kwa mshambuliaji huyo wa Simba ambaye licha ya kutokuwa na msimu mzuri akifunga bao moja msimu ulioisha, lakini aliziingiza timu vitani akihusishwa na Simba na Yanga, na meneja wake anatoa ufafanuzi kuhusiana na hilo.
"Shida ya Tanzania mambo yakienda kombo huku, wanalazimisha kumhusisha mchezaji upande mwingine. Ndio Kibu alikuwa na nafasi ya kwenda Yanga kwa sababu ni mchezaji, lakini Simba walikuwa tayari wameshamalizana na mchezaji huyo mapema, isingekuwa rahisi kwao kumaliza dili hilo," anasema na kuongeza:
"Hizo zilikuwa ni propaganda tu Kibu alikuwa tayari amesaini mkataba na Simba na nakumbuka akiwa Norway walikuwa wanataja kuwa atatambulishwa na Yanga Wiki ya Mwananchi kitu ambacho sio rahisi kwa sababu alipewa asilimia 100 ya kitu alichokuwa anakitaka."
Anasema labda ingekuwa kama ilivyotokea kwa Yusuf Kagoma, japo hana uhakika, lakini mchezaji alipata nafasi ya kuzungumza na timu zote mbili na kupewa mkataba wa awali, hilo lingewezekana, lakini kwa Kibu ilikuwa vigumu kwa sababu alikuwa na mkataba mpya ambao hajautumikia hata kidogo.
"Mpira umeshakuwa biashara sasa, hivyo mbali na uwezo wa uwanjani nje ya uchezaji unatakiwa kujiongezea thamani mwenyewe wachezaji wanatakiwa kubadilika na kujitengenezea mazingira mazuri ya ukubwa wao nje ya uwanja."
UTANI WA KIBU MITANDAONI
Licha ya Kibu kutajwa kuwa bora na kuwaniwa na klabu mbalimbali msimu uliopita, lakini msimu huu hana bao hata moja Ligi Kuu tangu alipofunga mara ya mwisho kwenye mchezo dhidi ya Yanga akiifungia timu yake bao la kufutia machozi kwenye kipigo cha mabao 5-1, na utani juu yake umekuwa mwingi mitandaoni, ila unaambiwa mwenyewe wala hajui kama anataniwa.

"Kama kuna kitu ambacho huwa Kibu hana muda nacho ni mambo ya mitandaoni, na hata kukaa na simu muda mrefu hayo mambo hana. Ukiona ameshika simu, basi kuna mtu anamtafuta atawasiliana naye na kuweka simu pembeni na kuendelea na mambo yake," anasema Carlos.
"Kuhusu sakata lolote linalomhusu nikiliona na nikaona linaendana na ukweli, ndio huwa namshtua na anaweza akaniuliza ni nini hicho, mbona mimi sijaona au kusikia, ndipo atakapoingia mitandaoni kutafuta. Muda mwingi yeye simu yake ni kuzungumza na familia yake, hana muda na mambo ya mitandaoni, hivyo wanaomzodoa wanabaki nayo wenyewe."
Anasema kama wasimamizi pia hawaumizwi na kutofunga kwake wakifurahia nafasi anayopata ya kucheza, licha ya baadhi ya watu kushindwa kumkubali.
"Makocha wangapi wamepita Simba na umeona namna ambavyo wamekuwa wakimuamini na kumpa namba. Hili kwetu ndio muhimu, lakini pia mbali na kutofunga ni mchezaji ambaye anakimbia dakika nyingi uwanjani. Kwa maana hiyo mbali na kufunga amekuwa akifanya vitu vingi uwanjani."
MWAMNYETO ALIPWA VIZURI
Kwa Mwamnyeto huu msimu wake wa nne ndani ya kikosi cha Yanga tangu alipojiunga nayo 2020/21 akitokea Coastal Union, na misimu miwili ya mwanzo alikuwa panga pangua, lakini baada ya ujio wa Ibrahin Hamad 'Bacca' na Dickson Job amepoteza namba kikosi cha kwanza.
Jambo hilo hata katika uongezwaji wake wa mkataba mwanzoni mwa msimu huu halikuwa la kipaumbele sana, lakini unaambiwa Yanga ilitoa pesa ndefu.

"Sisi sio watu wa mitandao katika usajili wa beki wa kati uliosumbua msimu uliopita Mwamnyesho ni miongoni mwao. Simba walikuwa wanamhitaji kwa gharama kubwa waajiri wake Yanga pia walikuwa wanahitaji kuendelea naye na klabu nyingine kubwa kama AS FAR ya Morocco ilituma ofa, lakini pesa yao haikuwa nzuri," anasema Carlos.
"Sio kama inavyozungumzwa ni kweli hakuwa na msimu mzuri kutokana na kukosa nafasi ya kucheza, lakini alisajiliwa kwa dau zuri ambalo lilidabo kila kitu na naweza kusema kwa sasa kwa Yanga Mwamnyeto ndio mchezaji wa ndani ambaye analipwa zaidi mshahara."
TIMU ZISISAJILI BILA MSIMAMIZI
Kumekuwa na chagamoto nyingi kwa wachezaji kujikuta wanaingia kwenye shida za kimkataba na kuishia kufungua kesi wakihitaji kusaidiwa kutokana na mikataba kuwa tofauti na makubaliano waliyofikia na klabu na hilo amelitolea Carlos anasema inatokana na wachezaji kukosa usimamizi makini.
"Mfano kuna klabu mkataba wake ni wa Kiingereza, lakini pia mchezaji anakubaliana na timu kwa njia ya simu, anatumiwa mkataba. Anachojua ni yeye kujaza sehemu ya jina na sahihi yake huku sehemu ya mkataba akiiachia klabu unafikiri nini kitafuata hapo," anasema.

"Wachezaji wengi akili yao ni fedha ya usajili na mshahara kumbe kwenye mkataba vipengele vina sehemu muhimu ...ukiondoa hizo mbili kuna vitu vingine muhimu zaidi. Mimi ni wakala nina shahada ya pili ya biashara, lakini bado huwa naambatana na mwanasheria kwa sababu sielewi. Licha ya uelewa wa kusoma mkataba lakini bado naamini uwepo wa mwanasheria ni muhimu kwa nini mchezaji asione umuhimu wa wakala."
Anasema anaamini timu zinatambua kuwa mchezaji ni muhimu kwa sababu ndiye anayecheza, lakini zisikubali kukubaliana na wachezaji wakati wa usajili akisisistiza kwamba zile kubwa ambazo zinajitambua zinatakiwa kuzungumza na mchezaji ambaye ana usimamizi na kama hana zimsisitize atafute.
"Wachezaji wengi wanahofia kutoa fedha kwa wasimamizi lakini hawafahamu kuwa ni muhimu. Kupanga ni kuchagua kama hawaoni umuhimu basi waendelee kuzunguka kufuatilia kesi zao," anasema.
"Mawakala pia wanatakiwa kuzingatia fedha wanazochukua kutoka kwa wachezaji hawatakiwi kujinufaisha wao kwanza. Wachezaji wanapitia mazingira magumu safari, kulala sehemu isiyo salama, lakini pia kupambana kwa dakika 90... wanastahili kupata kitu bora na sio kunyonywa."
Anasema mawakala wanatakiwa kuwasaidia wachezaji na sio kutumia vipaji vyao kujinufaisha, huku akisisitiza kuwa ni vyema kupata fedha, lakini si kuwakandamiza wachezaji kwani kuna wachezaji wanaopata fedha, lakini kuna watu hawatibiwi, hawaendi shule, hawali kuna wazazi hawalipi kodi hivyo wazingatiwe wapate kipato kikubwa.
MENDES ILA MINO FRESHI
Katika kila jambo linalofanywa na binadamu mwenye ndoto ya kufikia mafanikio, halikosi mfano yaani kuwa na mtu ambaye unamtazama ili kufikia mafanikio yake kama anavyoeleza Carlos kuwa licha ya kupachikwa jina la Mendes, yeye ana mtu anamtazama na kutamani kupita njia anazopitia.

"Huwa wanapenda kuniita Mendes ambaye ni wakala maarufu wa wachezaji, Jorge Mendes, lakini Mino Raiola (hayati) kwangu alikuwa bora zaidi... Mungu aendelee kumpumzisha mahala pema peponi," anasema
"Mendes pia nampenda kutokana na namna anavyoishi vizuri na wachezaji wake kama anavyothibitisha staa Cristiano Ronaldo amekuwa akimtaja kuwa sio wakala tu, bali ni baba yake... hii ni kutokana na namna anavyoishi nao."
Anasema Mendes anaishi na wachezaji kama watoto zake na yeye ndiye njia anazopita, hivyo anamtazama kama wakala wake bora na anatamani kupita nyayo zake.
SIMBA, YANGA
Simba na Yanga ndizo klabu kubwa na zenye mashabiki wengi kwenye soka la Tanzania kutokana na mafanikio ziliyopata na zimekuwa na utani kwenye matokeo na mafanikio zinayopata si rahisi kufanya nazo kazi kama haujasimamia misingi kutokana na utani wa jadi, lakini kwa Carlos ni tofauti.
"Simba na Yanga wana utaratibu kwenye masuala ya usajili ambao umepitishwa na kamati za utendaji ama bodi zao za wakurugenzi ambazo sio rahisi kuzibadilisha, hivyo inatulazimu kupita nazo kama zilivyo. Naweza kusema hiyo ni moja ya changamoto tunayokutana nayo tunapoingia mkataba na timu hizo," anasema Carlos.
"Ni kweli naweza kumpeleka mchezaji wangu kwenye moja ya timu hizo kwa kuangalia ubora wake na kutaka mkataba aweze kupewa gari na nyumba, lakini utaratibu wao hauruhusu kufanya hivyo kutokana na kuwa na vipaumbele vyao kwa wachezaji wa ndani na wa kigeni."

Anasema kwa upande wake changamoto hiyo haijamuwia vigumu kwani ana wachezaji Simba ambayo pia hairuhusu wachezaji wa ndani kulipiwa nyumba, lakini kuna wachezaji wake wanafanyiwa. Lakini upande wa gari pia wachezaji wake wamepata, vivyo hivyo kwa Yanga.
"Wakati mwingine viongozi wanaamua kuondoka kwenye utaratibu wao na kuamua kuingia kwenye mfumo wa namna maisha ya soka yanavyokwenda, wakishindwa kufanya hivyo wanaweza kukosa wachezaji wanaotamani kuwa nao kutokana na ubora walionao," anasema.
"Mabadiliko hayo pia yanategemea na aina ya usajili unaotaka kufanyika, kwani kuna usajili mwingine na mimi naweza kupiga hata goti ili dili likamilike, lakini kuwa mwingine natafutwa, mfano usajili wa Kazi (Hussein) hata kukubalika kutua kwenye klabu hiyo hata sisi tulishtuka ikabidi tukubaliane na matakwa ya klabu hiyo."
KAZI KAGOMA KUNG'OKA SIMBA
Licha ya mengi kuzungumzwa dirisha dogo la usajili huku ikidaiwa ofa nyingi zilitumwa Simba kumhitaji beki wa kati, Hussein Kazi kwa mkopo ikiwemo timu ya KMC ikielezwa kuwa Simba wamemgomea meneja wa mchezaji huyo, mwenyewe anafafanuzi sakata lilivyokuwa.

"Simba ilikuwa tayari kumtoa kwa mkopo, lakini mchezaji mwenyewe alikataa akiweka wazi kuwa bado anaiona nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba.
"Na ili jambo la kumtoa mchezaji kwa mkopo liweze kukamilika na kwenda sawa, ni lazima mchezaji awe tayari. Timu haiwezi kumlazimisha baada ya kukataa na mimi sikuwa na namna ya kufanya zaidi ya kumuacha tuone nini amekiona na atakifanyia kazi kwa namna gani."
KUSIMAMIWA NA CARLOS PITA HUMU
Sio wachezaji wote wanaocheza Ligi Kuu Nara wanao wasimamizi na ndio maana kumekuwa na wimbi kubwa la kesi zinazohusu masuala ya mikataba kutokana na wengi kukosa uelewa wa kuisoma na kujikuta wanajifunga bila wao kufahamu, kama anavyodai Carlos ambaye anataja sifa za kumsajili mchezaji ili aweze kumsimamia.
"Ubora wa mchezaji, nidhamu na maisha ndani na nje zaidi ya uwanja. Huku ndio huwa nazingatia kwa sababu nidhamu ya nje ya uwanja ndio inaangaliwa zaidi, mfano unaenda kumtazama unaambiwa huyu mchezaji ni mzuri sana, lakini ni mlevi hivyo hiki kitu kinashusha na kumharibia mchezaji," anasema.
"Inanichukua muda sana kumfuatilia mchezaji ili niweze kumsajili, nataka kuona ana tabia gani na ndipo naweza kumkaribisha ili niweze kufanya naye kazi."

Anasema kiwango cha mchezaji hata kiwe bora vipi mambo ya nje ya uwanja lazima yatamshusha, kwani hakuna mchezaji ambaye anaweza akawa na tabia mbaya nje ya uwanja kama kulewa au kukesha kumbi za starehe bado akawa na ubora.
"Ukimpata mchezaji ambaye anajitambua unakuwa na usimamizi mzuri na bora kama ambavyo najivunia wachezaji wangu wamekuwa bora nje na ndani ya uwanja huwezi sikia Tshabalala au Mwamnyeto anafanya mambo ya ajabu nje ya uwanja," anasema Carlos.
NI SHABIKI WA SIMBA
Licha ya kufanya kazi na timu mbalimbali ikiwemo Yanga ambao ni watani wa Simba, Carlos anasema kuwa hajawahi kujizuia kwenye ushabiki wake kwa Mnyama, lakini kwenye masuala ya kazi hana ushabiki na ndio maana amekuwa akifanya na timu zote.
"Siku zote nimekuwa nikizungumza wazi kuwa ni shabiki wa Simba. Licha ya kufanya kazi na Yanga sijawahi kuendekeza ushabiki kwenye masuala ya kazi, mfano nakumbuka mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (FA) nilizungumza na Erick Johora ambaye pia namsimamia nikamwambia mchezo huo utampandisha thamani anatakiwa kupambana, akanihakikishia hataruhusu kufungwa," anasema Carlos.

"Wakati huohuo nikazungumza na Kibu nikimsisitiza kuwa anatakiwa kufunga kuisaidia timu yake kuendelea hatua inayofuata na kuwatakia kila la heri kila mmoja. Nimekaa naangalia mpira dakika 90 bao 1-1 muda wa mikwaju ya penalti Johora alifanikiwa kuokoa penalti mbili kama sijakosea na kuisaidia Mashujaa kuendelea hatua inayofuata, nilifurahi mchezaji wangu kafanya vizuri, lakini matokeo yaliniumiza sana."
WACHEZAJI WAKE
Baadhi ya wachezaji ambao Carlos anawasimamia ni pamoja na Mohammed Husein 'Tshabalala', Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Hussein Kazi wote Simba ilhali upande wa Yanga ni Bakari Mwamnyeto, Aboubakar Khomeini; Singida Black Stars kuna Najim Mussa anayecheza kwa mkopo Namungo; Zawadi Mauya anayecheza kwa mkopo KenGold huku Dodoma Jiji yupo Reliant Lusajo; Mashujaa ni Erick Johora; Coastal Union ina Charles Semfuko; KMC ni Juma Shemvuni. Hao ni baadhi tu kwani asilimia kubwa ana wachezaji katika timu nyingi za Ligi Kuu Bara kasoro Azam FC.
