Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Buriani Doye Moke, nenda kipa wa boli

MOKE Pict

Muktasari:

  • Juzi, Alhamisi usiku zilizagaa taarifa za kushtusha na kusikitisha juu ya kifo cha kikatili kilichompata kipa aliyewahi kutamba na klabu za Majimaji Songea, Simba na Yanga kabla ya kustaafu na kujikita kwenye biashara za madini.

KIFO kimeumbwa, lakini hakizoeleki. Kifo kinauma kwa vile kinatengenisha wapendanao. Na bahati mbaya ni kwamba kifo hakikwepekwi.

Juzi, Alhamisi usiku zilizagaa taarifa za kushtusha na kusikitisha juu ya kifo cha kikatili kilichompata kipa aliyewahi kutamba na klabu za Majimaji Songea, Simba na Yanga kabla ya kustaafu na kujikita kwenye biashara za madini.

Video na picha zinazoumiza zinazomuonyesha kipa huyo aliyekuwa na mwili jumba na aliyejipatia umaarufu mkubwa kwa uwezo wake langoni. Ni ukatili unaodaiwa kufanywa na watu waliodhani ni mhalifu na kumchoma moto kama wahalifu wengine waliojaza mitaa ya DR Congo baada ya kundi ya M23 kuwaachia wahalifu waliokuwa wanashikilia na vyombo vya dola. Kufikia hatua ya kumchoma moto binadamu mwenzake aliye hai hadi kuteketea kwa moto kama nyama za mishkaki ni uhayawani uliopitiliza.

Lakini ndio hivyo, kipa wa bolu, Doye Moke ameondoka kama utani, tena ikiwa ni saa 48 tu kabla ya Dabi ya Kariakoo iliyopangwa kupigwa jana, haijapigwa pale  Kwa Mkapa. Dabi alizocheza enzi za uhai wake mara kadhaa akiwa na uzi wa Simba kisha Yanga hadi alipostaafu 2003.

MOKE 01

Hakuna neno zuri la kumpa mkono wa buriana mwamba huyo zaidi ya kumwambia Tangulia Doyi...tangulia kamanda...sisi tupo nyuma yako, kwa vile ‘Kila Nafsi itaonja mauti’ na sisi ni wa Mola na Kwake tutarejea.

Kama mmoja ya waandishi wa habari wa michezo nchini, niliwahi kufanya mahojiano maalumu na kipa huyu nje ya hoteli ya Lamada, Dar es Salaam zaidi ya miaka 10 iliyopita na aliweka bayana kazi alizokuwa akifanya baada ya kustaafu soka na hata muonekano wake kipindi hicho ulionyesha kile alichokimaanisha. Ebu endelea.


BIASHARA YA MADINI

Doye Moke katika mahojiano hayo alisema tangu alipostaafu baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa, aliamua kuwekeza nguvu zake katika biashara za kununua na kuuza madini kwenye nchi za Afrika.

Nyota huyo aliyeibebesha taji la ubingwa wa Ligi ya Muungano, Majimaji mwaka 1998 alisema amejikita katika shughuli hiyo kwa fedha za soka.

Alisema japo soka halikumpa fedha nyingi, lakini kidogo alichopata aliweka akiba inayomfanya aishi maisha mazuri akifanya biashara hiyo akishirikiana na nduguze.

Mzaliwa huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, aliyeanza kucheza soka tangu shule ya msingi na kucheza soka la kulipwa akiwa na miaka 17 tu katika timu ya Muungano ya Bukavu, alikuwa akiuza madini chini ya kampuni yake iitwayo GFK Limited, yeye akiwa ndiye mkurugenzi akinunua madini kama almasi na dhahabu toka DR Congo na kuuza Tanzania na nchi nyingine za Afrika na kumfanya awe mtu wa kusafiri. Moke alisema kabla ya kufanya biashara hiyo alijikita katika biashara nyingine mara alipotundika daluga mwaka 2003. Hata hivyo hazikumlipa kama biashara yake ya sasa.

MOKE 02

Mkali huyo aliyewahi kuwika pia na timu za Aspwara, Rayon za Rwanda na Afya Sport ya Goma aliwakumbusha wachezaji wanaoendelea kukipiga kwamba wawe makini na kile wanachovuna katika soka kwa ajili ya manufaa ya baadae.

“Tulipokuwa tukicheza fedha hazikuwepo kama leo. Hata hivyo baadhi yetu tulikuwa na fikra za mbali ndio maana leo tunaishi vyema, kwa wanaocheza sasa ni wajibu wao kukumbuka kesho yao kwa kujiwekea akiba,” alinukuliwa Moke  katika mahojiano hayo.


ALIPOTOKA

Doyi Moke alizaliwa Oktoba 4, 1967 Bukavu, Zaire (sasa DR Congo) akiwa ni mtoto wa sita kati ya 10 wa familia yao.

Shule ya msingi aliisoma College Alfajiri kisha Atenend Banda Sec kabla ya kusomea Diploma ya Lugha ya Kifaransa.

Kisoka alianza kucheza tangu kinda akidakia timu za shule na kutwaa mataji ya mashindano ya shule nchini humo, akimtaja kocha Gabie Mugimbi kuwa ndiye aliyekivumbua kipaji chake. Moke alikiri alivutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Ufaransa, Michel Platin na kuitaja klabu yake ya kwanza ya kulipwa kuwa ni Muungano aliyotwaa nayo taji la Ligi ya Mkoa wa Bukavu mwaka 1987.  Baada ya kung’ara na timu hiyo kocha wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu alimuona na kumpeleka Rwanda kuichezea ASPWARA 1989 kabla ya kutua Rayon Sport kwa muda na kurudi DR Congo kuichezea Afya ya Goma.

MOKE 03

Baadae alitua Vital’O ya Burundi na kufanya mambo makubwa akiwapiku makipa wanne aliowakuta kikosini ikiwemo mmoja, Ramadhani Ally aliyemsusia jezi alipopewa nafasi mara ya kwanza kikosini.

Alisema anakumbuka kocha alimpa nafasi katika mechi dhidi ya wapinzani wao Port Louis walioifunga mabao 2-0 na kujihakikishia namba akiipa ubingwa na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika 1992.

Alisema aliachana na Vital’O  1995 aliposhuhudia mchezaji mwenzake, Kamala Jeff akipigwa risasi na waasi wa Burundi mpakani mwa nchi hiyo na DR Congo na kuamua kuachana na soka ili aende Afrika Kusini kusaka maisha.  “Hata hivyo, nilipofika Tanzania nikiwa naelekea Sauzi, nilikutana Mackenzie Ramadhani (kipa wa zamani wa kimataifa wa Mrundi aliyetamba na Simba miaka ya 1980), aliyenishawishi kuendelea na soka na kunikutanisha na kocha Nzoysaba Tauzany, aliyenisajili kuichezea Majimaji aliyokuwa anaifundisha,” alisema.

Alisema hakuamini alipopokewa kama ‘mfalme’ mjini Songea na viongozi akiwemo RC aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda akitaja dau alilosajiliwa likiwa Sh 700,000.  Baada ya kuipa ubingwa wa Muungano 1998 kutokana na kumaliza Ligi ya Tanzania Bara wakiwa watatu nyuma ya Yanga na Simba, mwaka 1999 alihama na kutua Simba aliyoichezea kwa mafanikio kabla ya kusajiliwa Yanga. Alisema aliamua kuachana na Simba baada ya ‘kuzikwa’ fedha za usajili na mmoja wa viongozi na kuhamia Yanga mwishoni mwa  2000 na kuichezea hadi 2003 alipoenda Rayon Sport na kustaafu huko.

Alisema tangu alipostaafu alikuwa mshauri wa Yanga na wachezaji walioitumikia, sambamba na kumpiga tafu shemejie, Henry Kalekwa anayemiliki timu ya Sofapaka ya Kenya.  Enzi za uhai wake, Moke alikuwa anapenda kula wali kwa kisamvu na kunywa bia ya Safari, huku akisema kati ya klabu zote alizochezea Vital’O na Yanga ndizo bomba kwake.

Alisema mbali na kuichezea, pia alikiri alikuwa shabiki mkubwa wa Yanga, Arsenal na TP Mazembe, huku akidai anapenda kuogelea na kubadilishana mawazo.

MOKE Pict

ISHU YA HUJUMA

Moke aliyemtaja Mbwana Samatta anayecheza kwa sasa PAOK ya Ugiriki kama nembo ya Tanzania katika soka la kulipwa kwa kipaji kikubwa alichonacho, alisema ndani ya soka amekumbana na mambo mengi.

Alitaja mojawapo ni tuhuma alizodai kubambikiwa Simba akidaiwa kuihujumu timu hiyo dhidi ya Yanga katika mechi iliyochezwa mwaka 2000 ambapo Yanga walishinda 2-0 kwa mabao ya ‘Bwana Harusi’ Idd Moshi.

“Jambo hilo linaniuma hadi sasa na ndilo lililonifanya niichukie Simba kwa vile uongozi uliamua kunipakazia baada ya kuumbua kwa wanahabari juu ya kunizika fedha zangu za usajili,” alisema katika mahojiano hayo.

Juu ya mechi ngumu enzi akicheza, Moke alisema ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2001 akiichezea Yanga na Highlander ya Zimbabwe iliyochezwa Harare ambapo Yanga ilishakata tamaa baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani.

“Naikumbuka kwa namna nilivyowaapia Wanayanga waliokata tamaa na kutishwa na kauli ya kocha wa Highlander aliyetutaka tusisumbuke kuwafuata kwao kwa maana tulikuwa tunajisumbua tu,” alisema.

Alisema, hata hivyo aliwapa moyo wenzake na kwenda kufanya vitu adimu uwanjani na kuisaidia Yanga kushinda mabao 2-0 na kusonga mbele.

Moke alimtaja Mohammed Husseni ‘Mmachinga’ kama mshambuliaji aliyekuwa akimnyima raha walipokuwa wakikutana enzi akikipiga Majimaji na baadae Simba kabla ya kucheza naye Jangwani na kupumua. Buriani Doyi Moke, nenda kamanda msalimie Patrick Mafisango. Kwa hakika tutakukumbuka kwa kazi kubwa ya kuwapa burudani mashabiki wa Simba na Yanga