Prime
Vifaa vilivyo katika rada za Simba, Yanga

Muktasari:
- Fountain iliyokuwa ikijitetea isishuke daraja na Stand ikipambana kutaka kurejea katika Ligi Kuu tangu iliposhuka msimu wa 2018-2019 na matokeo yameibeba Fountain kwa kushinda jula ya mabao 5-1.
MSIMU wa Ligi ya Bara ulifungwa juzi kwa mechi ya marudiano ya mtoano kati ya Fountain Gate ya Ligi Kuu na Stnd United ya Championship zilizovaana mjini Babati, Manyara.
Fountain iliyokuwa ikijitetea isishuke daraja na Stand ikipambana kutaka kurejea katika Ligi Kuu tangu iliposhuka msimu wa 2018-2019 na matokeo yameibeba Fountain kwa kushinda jula ya mabao 5-1.
Pamoja na kwamba msimu mpya umefungwa na sasa klabu zinaanza kujipanga kwa msimu wa 2025-2026, lakini tayari kelele za usajili zimeanza. Hakuna timu inayotaka kupitwa. Vita ya kuwania mataji msimu ujao imeanza mapema sio tu kwa mazoezi na mikakati ya ndani, bali mbio za usajili wa vifaa vipya. Wakati timu nyingi bado zinaangalia namna ya kumaliza msimu huu kwa heshima, Simba na Yanga zimeamua kuusoma wakati.
Kivipi? Zimeamua kuingia sokoni mapema kwa ajili ya kujenga vikosi kwa ajili ya mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika kwa hesabu zisemazo: “Mafanikio yanapikwa kabla msimu haujaanza.” Usajili wa mapema unamaanisha muda wa kutosha kwa wachezaji wapya kujenga uelewano, kufahamu mifumo ya kocha na kuingia kwenye falsafa ya timu.
MSINGI WA HARAKATI
Sababu kubwa ya kuanza mapema harakati hizo ni dhamira ya kutawala ndani na kufika mbali zaidi kimataifa. Timu hizo zimejihakikishia nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya Yanga kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo ikimaliza ligi ikiwa na pointi 82 dhidi ya 78 za Simba iliyomaliza ya pili, huku Azam au Singida Black Stars zikikata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kushika nafasi ya tatu na nne mtawalia.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids na Miloud Hamdi aliyekuwa Yanga kabla ya kuondoka hivi karibuni, walishawasilisha ripoti kuhusu maeneo ya kuboreshwa. Wameomba wachezaji wa viwango vya juu wakiwa na sifa za tabia zinazolingana na maono ya klabu.
SIMBA
Kwa upande wa Simba, Fadlu anaamini kikosi kinahitaji kuboreshwa maeneo manne - kiungo wa kuzuia, kiungo wa kushambulia, mshambuliaji wa kati, na beki wa kati mwenye kasi na uamuzi wa haraka.
Upungufu huo ulijitokeza zaidi kwenye mashindano ya kimataifa, ambapo Simba ilionekana kukosa uimara wa kimkakati hasa inapokutana na timu za Afrika Magharibi na Kaskazini.
Ripoti ya Fadlu inaeleza Simba inahitaji mchezaji wa kusimama mbele ya walinzi kuwasoma wapinzani na kupoza presha kabla haijafika langoni. Pia, ameomba namba 10 mwenye ubunifu wa hali ya juu siyo kusambaza pasi tu, bali kuamua matokeo ya mechi kwa ubora katika sekunde chache. Hali hiyo inakwenda sambamba na ombi la mshambuliaji mpya. Licha ya uwepo wa Leonel Ateba na Steven Mukwala na nyota chipukizi kama Valentino Mashaka, Simba inahitaji straika mwenye uzoefu aliyekutana na presha za soka la Afrika na anayefunga bila kutumia nafasi nyingi.
Lakini anahitaji kipa mpya mzawa wa kumpa changamoto Moussa Camara kama ataendelea kusalia kikosini kutokana na kuondoka kwa Aishi Manula ambaye msimu mzima aliwekwa benchi, huku Ally Salim na Hussein Abel wakishindwa kumtikisha Camara. Lakini kuna kiungo mshambuliaji mkali zaidi ya Jean Charles Ahoua anayetakiwa kuongeza nguvu eneo hilo kwa wachezaji walioonekana wangeweza kumsumbua kama Awesu Awesu ni kama vile wamechemka.
YANGA BILA AZIZ KI
Yanga inakabiliwa na changamoto kutokana na kuondokewa na kiungo tegemeo, Stephane Aziz Ki ambaye amejiunga na Wydad Casablanca. Aziz Ki si mchezaji wa kawaida, alikuwa injini ya timu, kiongozi uwanjani na mtu wa matokeo.
Kuondoka kwake ni pengo kwani kunahitaji mtu mwenye tabia, maono na ukomavu kama wake. Kocha Hamdi aliomba mbadala wa Aziz KI mapema kabla ya kutimkia. Lakini si Aziz Ki tu, Yanga inahitaji mshambuliaji mwingine wa kati kutokana na sintofahamu ya hatma ya Clement Mzize ambaye anahusishwa na klabu kadhaa za nje.
Vilevile kutokana na kutokuwepo kwa uhakika kwenye beki ya kulia hasa kutokana na majeraha ya muda mrefu ya Attohoula Yao Hamdi alitaka mchezaji wa nafasi hiyo asajiliwe.
Yanga pia inahitaji mbadala wa Khalid Aucho ambaye mkataba wake uliisha na tayari ameongezwa mpya wa mwaka mmoja. Katika mechi za kimataifa, uzoefu na uimara wake umetegemewa sana. Kwa kuongezewa mkataba, mbadala wake lazima awe tayari kuanza kusoma ramani mapema wakati Mganda huyo akielekea ukingoni kuishi Jangwani.
SOKO LILIVYO
Majina mengi yameanza kutajwa. Baadhi yao ni haya:
Feisal Salum ‘Fei Toto’: Kiungo wa Azam FC anayewaniwa kwa nguvu na timu zote mbili. Simba imeshatuma ofa mezani, lakini Yanga iko tayari kufunguka zaidi. Tayari kuna taarifa kuwa ofa ya mshahara wa Sh40 milioni kwa mwezi imewekwa mezani.
Imourane Hassane: Kiungo mkabaji kutoka Loto Popo ya Benin, aliyewahi kupita Uswisi. Simba inamtazama kama nyongeza bora kwa safu ya kiungo wa ulinzi.
Damaro Camara: Kiungo wa Singida Black Stars ambaye ametajwa kuwa na utulivu mkubwa na uelewa wa mchezo. Yanga wanamwona kama suluhisho la namba 6 au 8.
Ibrahim Keita: Beki wa kulia wa TP Mazembe, anayetajwa kuwa tayari kujiunga na Ligi Kuu. Yanga imemwekea mezani ofa ya miaka miwili. Hata hivyo Keita tayari ameshanyakuliwa na Esperance iliyomwahi mapema kabla ya Yanga kufanya mambo na sasa Yanga itakomaa tu na Yao wakati ikijianmga kivingine kwa nafasi hiyo ya beki wa kulia ambao bado ina Israel Mwenda na Kibwana Shomari mbali na Dickson Job ambaye amewahi kutumikishwa huko na makocha wa Yanga.
Koimizo: Nyota wa ASEC Mimosas, anayelengwa na Yanga kama mbadala wa Aucho.
Gibril Sillah: Winga mahiri wa Azam FC ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni. Timu zote mbili zinamezea mate uwezo wake mkubwa wa kupiga krosi zenye madhara.
Jonathan Sowah: Mshambuliaji kutoka Singida Black Stars. Simba wanamtaka, lakini Yanga na Kaizer Chiefs pia wako mbioni.
Henock Inonga: Beki wa kati wa FAR Rabat aliyewahi kung’ara Simba. Anatajwa kuwindwa na Yanga.
USHINDANI, MAHITAJI MAPYA
Katika kipindi cha nyuma, Simba na Yanga zilifanya usajili mwingi wa majina makubwa lakini bila muunganiko wa kiufundi. Sasa wanabadilika. Wanafuata hesabu za kisayansi kwa kufanya ‘scouting’, data, umri, matumizi ya GPS tracker na psychology za wachezaji kabla ya kusaini mikataba. Hii ndiyo sababu ripoti za makocha zimepewa uzito mkubwa. Hakuna tena usajili kwa presha za mitandaoni. Falsafa imebadilika usajili wa kimkakati, wa kusaidia kocha kutimiza malengo yake.
VITA YA MIKATABA
Msimu wa usajili unakuja ukiwa na uzito wake. Tofauti na miaka iliyopita, sasa timu hazisubiri kuona nani anaondoka kisha waanze kusaka mbadala. Wanajua mapema, wanapanga mapema, na wanatekeleza mapema. Katika dunia ya kisasa ya soka, kilicho cha mapema ndicho kinachoshinda.
Mashabiki wakae mkao wa kula. Vita ya mchezaji bora si tu uwanjani imehamia kwenye meza za mikataba, katika simu za usiku wa manane, na kwa mawakala wanaofanya kazi kwa saa 24. Je, nani atashinda vita ya sokoni? Muda ndio utatoa majibu.